Tuesday, August 22, 2017

MAMLAKA MAJI SAFI NA USAFI WA MAZINGIRA KUPINGA MAHAKAMANI HOJA YA BARAZA LA MADIWANI MBINGA

Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wakiwa kwenye kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika Agosti 17 mwaka huu kwenye ukumbi wa Umati mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, imesema kwamba ipo tayari kwenda Mahakamani kupinga hoja iliyopitishwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo juu ya ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya halmashauri ya wilaya hiyo, ambazo zinatarajiwa kujengwa katika eneo la Ndengu lililopo katika kata ya Nyoni wilayani humo.

Vilevile MBIUWASA wameeleza kuwa wakiwa kama wadau wakubwa wa eneo hilo katika suala la uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji hawajashirikishwa katika mchakato huo ili waweze kutoa ushauri wao kama eneo hilo linafaa kwa shughuli hizo za ujenzi au la.

Kauli hiyo ilitolewa na Meneja wa Mamlaka hiyo, Patrick Ndunguru wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake akieleza kuwa ni lazima wazingatie sheria ya athari za mazingira ya mwaka 2004 na wao wakiwa kama wadau wakubwa walipaswa washirikishwe kwanza kabla ya hoja hiyo kupitishwa katika vikao vya Madiwani.


“Kwenye huu mchakato walipaswa watushirikishe kwanza, ujenzi ukianza pale tayari watu wengi watavutiwa kwa ajili ya kuwekeza na mji utaanza kuwa mkubwa na uzalishaji taka na uharibifu wa mazingira utakuwa mkubwa, hatukubaliani na maamuzi haya siku zote uwekezaji mkubwa unapofanyika kama huu ni lazima kufanyike tathimini ya athari za mazingira ukizingatia kwamba eneo lile ni muhimu limeangukia karibu na vyanzo vya maji ambavyo ndiyo tegemeo kubwa kwetu”, alisema Ndunguru.

Alisema kuwa itashangaza leo kuona mji mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga unaenda kujengwa kwenye eneo la Ndengu ambalo mazingira yake na vyanzo vya maji vimehifadhiwa kwa muda mrefu ili kuweza kuzalisha maji safi na salama kwa wingi kwa ajili ya kulisha wakazi wa mji wa Mbinga.

Ndunguru alisema kuwa hapo awali kulikuwa na watu wakiishi kwenye eneo hilo lakini walichukua jukumu la kuwahamisha kwa gharama kubwa ili kuweza kutunza vyanzo hivyo visiweze kuharibiwa na kwamba itashangaza kuona kama serikali itakubaliana na suala hilo la kwenda tena kuweka makazi kwa kujenga miundombinu ya ofisi za halmashauri hiyo.

Maamuzi hayo ya ujenzi wa ofisi za halmashauri ya wilaya ya Mbinga yalifikiwa Agosti 17 mwaka huu katika kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa, baada ya uwepo wa mvutano mkubwa uliodumu kwa masaa kadhaa kati ya Madiwani hao na Watendaji wa halmashauri hiyo juu ya wapi ofisi hizo zitajengwa.

Awali zilipopigwa kura kwa lengo la kukubaliana kwamba ujenzi huo ukafanyike katika eneo la Kiamili lililopo katika kata ya Kigonsera, Madiwani hao walikataa na kukubaliana kwamba zipigwe kura kwa mara ya pili kwa kuchagua kati ya eneo la Maguu, Ndengu na Matiri.

Zilipopigwa kura kwa mara ya pili kuchagua maeneo hayo ndipo waliweza kupitisha eneo hilo la Ndengu ambalo lilishinda kwa kura 24, likifuatiwa na Matiri kwa kura 9 na Maguu kwa kura 1 huku kura mbili zikiharibika kati ya wapiga kura 36 waliokuwepo katika kikao hicho.


Kwa ujumla halmashauri ya wilaya ya Mbinga imefikia hatua ya kuhama katika ofisi zake za awali zilizopo mjini hapa na kwenda kujenga miundombinu mingine mipya ya wilaya hiyo katika eneo lingine, baada ya kugawika na kuizaa halmashauri nyingine ya mji wa Mbinga ambayo ndiyo inapaswa kutumia majengo hayo yaliyopo sasa mjini hapa.

No comments: