Mganga mkuu wa Manispaa ya Songea, Mameritha Basike akimjulia hali mgonjwa Mary Lupindu ambapo mgonjwa huyo ni wa kwanza kufanyiwa upasuaji katika kituo cha afya Mjimwema Songea. |
Na Mwandishi wetu,
Songea.
UTEKELEZAJI wa sera ya afya katika kuendelea kuimarisha
utoaji wa huduma ya afya kwa wananchi kituo cha afya Mjimwema kilichopo katika Manispaa
ya Songea mkoani Ruvuma umeanza kufanyika, ambapo kituo hicho kimeanza kutoa
huduma ya upasuaji kwa akinamama wajawazito.
Mary Lupindu akiwa amewashika watoto wake mapacha. |
Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dokta Mameritha Basike alisema
kuwa wameanza kutoa huduma hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dokta Khamis Kigwangala
ambaye aliagiza huduma ya upasuaji ianze kutolewa mara moja katika kituo hicho
ili kuweza kunusuru afya za akinamama hao.
Dokta Basike alisema kuwa kitengo hicho cha upasuaji hivi sasa
kinao uwezo wa kufanya hadi Operesheni saba kwa siku na kwamba wakiongezeka
madaktari watakuwa na uwezo wa kufanya upasuaji kati ya watu 10 hadi 15 kwa
siku.
Alisema wana madaktari wa upasuaji watatu na kwamba
wanahitaji madaktari wengine nane, wauguzi 12 na kuongezewa vifaa vya upasuaji
ili kuhakikisha kwamba wanafanyakazi zao kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake Daktari Mfawidhi wa kitengo cha upasuaji
katika Kituo hicho Dokta James Mapunda alitoa wito kwa wananchi wa Manispaa ya
Songea kwenda katika kituo hicho ili waweze kupata huduma za upasuaji badala ya
kwenda mbali kwa kuwa serikali hivi sasa imewasogezea huduma hiyo karibu.
Vilevile Madaktari wamefanikiwa kutoa huduma ya upasuaji kwa
mgonjwa wa kwanza ambaye alijifungua watoto mapacha baada ya kufanyiwa upasuaji
katika kituo hicho cha afya Mjimwema.
Mama huyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Mary Lupindu (30)
mkazi wa Mkuzo katika Manispaa ya Songea alisema amejifungua salama watoto wake
mapacha katika kituo hicho na hali yake inaendelea vizuri.
Lupindu alieleza kuwa anawashukuru madaktari waliokuwa wakimpatia
huduma ya matibabu ikiwemo huduma bora ya upasuaji ndiyo iliyomwezesha yeye na
watoto wake mapacha wanaendelea vizuri ambapo alitoa rai kwa wananchi wengine
wasiogope kupata huduma za upasuaji katika kituo hicho.
Kituo cha Afya Mjimwema kilianzishwa Aprili 8 mwaka 2002
ambapo Kituo hicho kina majengo nane yakiwemo jengo la wagonjwa wa nje, wodi ya
watoto na wanawake, wodi ya wazazi na huduma ya kujifungua, jengo la kutolea
huduma za afya ya uzazi na mtoto na wodi ya wanaume, jengo la utawala, jengo la
kuhifadhia maiti, nyumba mbili za watumishi na jengo la upasuaji.
Huduma ambazo hazitolewi katika kituo hicho ni huduma za
macho, huduma za kuongeza damu, huduma za pua, masikio, koo na huduma ya mionzi
yaani ultrasound.
Pamoja na mambo mengine, halmashauri ya Manispaa ya Songea
ina vituo 30 vinavyotoa huduma za afya ikiwemo zahanati 26 na hospitali ya
Rufaa iliyopo mjini Songea.
No comments:
Post a Comment