Friday, August 18, 2017

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUHAMASISHA UWEKEZAJI MKOANI RUVUMA

Na Muhidin Amri,        
Songea.

IKIWA uchumi wa mkoa wa Ruvuma unatajwa kukua kwa kasi kwa wastani wa pato la mwananchi wa kawaida linalofikia shilingi milioni 2.6 mwaka 2016 hadi 2017 kutoka shilingi milioni 2.2 mwaka 2013, wito umetolewa kwa waandishi wa habari wa mkoa huo kutumia kalamu zao kuandika habari zinazohamasisha watu wenye uwezo na makampuni mbalimbali kwenda kuwekeza katika sekta ya kilimo kutokana na maeneo mengi mkoani humo hufaa kwa kilimo.

Aidha serikali imeombwa kutenga fedha za kutosha kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NRFA) Kanda ya Songea ili aweze kununua kiasi kikubwa cha mahindi ambacho kimezalishwa kwa wingi katika maeneo ya mkoa huo ili kuepusha uwezekano wa wananchi kupata hasara.

Hayo yalisemwa jana na baadhi ya wakulima wanaoendelea na maonesho yao ya bidhaa za kilimo katika viwanja vya nane nane kata ya Msamala Manispaa ya Songea mjini hapa huku wakisisitiza kuwa ni vyema sasa waandishi wa habari wakawa wazalendo kwa kuandika habari hizo zenye kuchochea uwekezaji na shughuli zote za maendeleo ya wananchi.


Walisema kuwa waandishi na vyombo vyao vina wajibu mkubwa wa kufikisha kilio hiki cha wananchi hasa wakulima na changamoto zao, ikiwemo serikali kuongeza fedha kwa NFRA ili wakulima waweze kuuza mahindi na mazao mengine waliyozalisha katika msimu huu wa mwaka 2016 na 2017.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa mkoa huo walisema kuwa bado kuna fursa nyingi za kiuchumi hata hivyo hazijafanyiwa kazi kwa sababu waandishi waliopo na vyombo vyao vya habari havijaweza kutimiza majukumu yao, badala yake vimejikita hasa kuandika habari za watu maarufu ambazo hazina manufaa kwa wananchi wanyonge wanaoendelea kuteseka na hali ngumu ya maisha.

Ally Abdallah alisema kuwa mkoa wa Ruvuma ni kati ya mikoa ambayo inazalisha kwa wingi zao la mahindi tatizo kubwa ni ukosefu wa soko la uhakika la kuuza zao hilo, lakini baada ya serikali kuzuia mahindi kuuzwa nje bado wakulima wangenufaika kama kungekuwa na viwanda vingi vya kuongeza thamani ya zao hilo na hatimaye wakulima wangeuza unga badala ya mahindi.


Naye Anna Komba aliwataka waandishi wa habari kujikita zaidi kuandika habari zenye manufaa kwa wananchi hasa wale waishio vijijini ambao wanakabiliwa na kero mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maafisa ugani, hasa wakati wa maandalizi ya msimu wa kilimo pale unapoanza ili waweze kuzalisha kwa wingi na kwamba kalamu zao zikitumika vyema zitasaidia pia kuinua uchumi wa mkoa ambao zaidi ya asilimia 80 hutegemea shughuli za kilimo ikiwa ndio chanzo kikuu cha mapato.

No comments: