Baadhi ya Wanafunzi wa shule ya msingi Subira katika Manispaa ya Songea wakiwa katika hofu kutokana na ugonjwa wa ajabu ulioikumba shule hiyo. |
Na Mwandishi wetu,
Songea.
UGONJWA wa ajabu ambao haujafahamika jina lake, umezuka shule
ya msingi Subira iliyopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma na kusababisha
wanafunzi 335 kutohudhuria masomo yao darasani tangu mwezi Machi mwaka huu.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Majidu Ngonyani alisema kuwa
shule ina jumla ya wanafunzi 578 lakini wanafunzi wanaohudhuria masomo mpaka
sasa ni 243 tu ambao ni sawa na asilimia 42 kutokana na tatizo hilo.
Kwa mujibu wa maelezo ya Ngonyani alisema kuwa wanafunzi wanaopata
ugonjwa huo hasa ni wa kike na kwamba hadi sasa licha ya madaktari kuchukua
vipimo kwa wanafunzi wanaougua bado haijafahamika ni ugonjwa wa aina gani.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Abdul Mshaweji na Afisa
elimu msingi wa Manispaa hiyo, Edith Kagomba mara kadhaa wamefanya ziara katika
shule hiyo ili kuweza kutafuta ufumbuzi wa kudumu kwa kufanya mikutano na
wananchi waliokaribu na shule hiyo lakini imeshindikana.
Katika kikao cha Julai 21 mwaka huu ambacho kamati ya shule,
walimu na wananchi licha ya kuketi pamoja huku wakishirikisha viongozi
mbalimbali wa madhehebu ya dini kwa ajili ya kufanya maombi maalumu wakiwa
wanaamini yanaweza kumaliza tatizo hilo linaloathiri taaluma na maendeleo ya
watoto wa shule hiyo lakini pia ilishindikana.
Tatizo lililoikumba shule ya msingi Subira limewahi kutokea
katika shule ya sekondari Beroya, shule ya msingi Mwengemshindo na Chandarua
katika Manispaa ya Songea ambapo ufumbuzi wake ulifanywa kwa maombi maalumu ya
madhehebu ya dini na watoto waliweza kuendelea vizuri na masomo yao mpaka sasa.
No comments:
Post a Comment