Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge amepiga
marufuku kwa kuwataka Wakurugenzi na Wakuu wa idara katika halmashauri za
wilaya mkoani humo, kuacha mara moja tabia ya kuhamisha na kubadili matumizi ya
fedha ambazo zilitengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya wananchi ikiwemo
kilimo na miradi mingine.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu huyo wa mkoa jana wakati
akizungumza na wakulima, watendaji wa serikali pamoja na wananchi waliohudhuria
ufunguzi wa maonesho ya wakulima nanenane ambayo kimkoa yanafanyika katika
viwanja vya nanenane vilivyopo katika kata ya Msamala Manispaa ya Songea mjini
hapa.
Dokta Mahenge alisema kuwa tabia hiyo imekuwa ikikwamisha mkakati
wa kuinua maendeleo ya wananchi hasa kwa upande wa shughuli za kilimo katika
maeneo mbalimbali, kwa sababu baadhi ya wakuu hao wa idara hushirikiana na
wakurugenzi wao kuiba fedha hizo kwa mtindo huo jambo ambalo linarudisha nyuma mpango
wa kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani.
Alisisitiza kuwa suala la kuongeza tija katika uzalishaji kwa
eneo ni muhimu na kama tunataka kujitosheleza kwa chakula na kupata ziada ya
kuuza nje ya nchi ni muhimu kuongeza kiwango cha uzalishaji na sio vinginevyo.
Vilevile alibainisha kuwa takwimu za uzalishaji wa zao la mahindi
katika mkoa wa Ruvuma zinaonesha kwamba hekta moja inazalisha kati ya tani 2
hadi 3 lakini utafiti unathibitisha kuwa hekta hiyo moja inaweza kuzalisha hadi
kufikia tani 7 hivyo mkulima anapaswa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili
aweze kufikia malengo hayo.
Kutokana na hali hiyo Dokta Mahenge amewataka wakulima wa
mkoa huo waachane na tabia ya kilimo cha mazoea ambacho katika kipindi cha
msimu wa uzalishaji wa mazao ya chakula mkoani humo kimekuwa kikiwarudisha
nyuma licha ya kazi kubwa wanayoifanya mwaka hadi mwaka.
Alisema mkoa una eneo la ukubwa wa hekta 59,943 linalofaa kwa
kilimo cha umwagiliaji lakini hadi sasa eneo linalotumika ni hekta 10,266.1 tu
sawa na asilimia 17 ya eneo hilo licha ya kilimo hicho kuwa ndiyo mhimili
mkubwa wa kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali.
Pia amezitaka halmashauri za wilaya kwa kushirikana na
wananchi ziendelee kuomba fedha za ujenzi wa skimu za umwagiliaji kupitia mfuko
wa umwagiliaji wa wilaya (DIDF) chini ya programu ya kuendeleza sekta ya kilimo
ili kuweza kujenga na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji iliyopo mkoani
hapa.
Kadhalika takwimu za uzalishaji wa mazao ya chakula na
biashara katika mkoa huo zinaonesha kuwa katika msimu wa mwaka 2016/2017 jumla
ya hekta 837,208 za mazao ya chakula na biashara ambazo zilitoa mavuno tani
1,858,908 wakati mahitaji ya chakula kwa wakazi wa mkoa huo wapatao
1,376,891 kulingana na sensa ya mwaka 2012 ni tani 469,172 kwa mwaka na huku
ziada ya chakula ikiwa ni tani 1,689,699 za mazao ya chakula.
Pamoja na mambo mengine aliwapongeza wananchi kwa mafanikio
hayo yaliyofikiwa kwani chakula cha ziada kilichozalishwa kitasaidia kulisha
wananchi katika maeneo yenye upungufu mkubwa wa chakula hapa nchini na ziada
kuuzwa licha ya hivi sasa kukabiliwa na changamoto nyingi katika uzalishaji,
uhifadhi, usindikaji na masoko.
Aliwataka wakulima wa mazao ya kahawa, tumbaku na
korosho kuwa tayari kutumia mikutano ya wadau katika kupanga mikakati ya
kujadili hali ya masoko ipoje, sambamba na wataalamu wa kilimo na mifugo kuwa
na tabia ya kuwafikia wakulima na kutoa huduma za ugani kwa wakati ili kuongeza
tija ya uzalishaji kwa mazao ya kilimo na mifugo.
Awali Katibu tawala msaidizi wa mkoa huo Bwai Biseko alisema kuwa
maonesho hayo ya nanenane mwaka huu yameandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa kwa
kushirikiana na halmashauri za wilaya, ambapo lengo lake wananchi watumie fursa
ya maonesho hayo kwa ajili ya kuona na kujifunza kwa lengo la kuchochea maendeleo
katika sekta hiyo muhimu.
Hata hivyo mkakati wa serikali ya awamu ya tano ni kukifanya
kilimo kuwa ndiyo njia kuu ya kukuza uchumi ambapo wananchi wenyewe ni
washiriki wakuu katika maonesho hayo.
No comments:
Post a Comment