Na Mwandishi wetu,
Songea.
MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (SOUWASA) katika
Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, inazidai baadhi ya taasisi na idara za serikali fedha
zaidi ya shilingi milioni 794,118,058.38 ikiwa ni malimbikizo ya ankra ya maji
hadi kufikia Julai 30 mwaka huu baada ya kusambaza huduma ya maji kwa taasisi
hizo.
Aidha licha ya mamlaka hiyo kutoa notisi kwa idara na taasisi
hizo ikizitaka kulipa deni hilo kuanzia Juni 28 mwaka huu hali imekuwa kinyume na
kwamba ni taasisi mbili tu ambazo ni shule ya sekondari ya wasichana Songea
iliyopo mjini hapa iliyokuwa inadaiwa shilingi 6,295,128.00 ambayo imelipa deni
lake kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Chuo cha waganga wasaidizi
Songea ambacho kimepunguza shilingi milioni 10 kati ya shilingi milioni
30,209,469.22 ambazo kilikuwa kinadaiwa.
Kaimu Mkurugenzi wa SOUWASA Mhandisi John Kapinga alisema
kuwa Hospitali ya rufaa Songea ndiyo inayoongoza kwa kudaiwa shilingi milioni
276,233,440.73, ikifuatiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) shilingi 126,690,090.10,
Magereza ya mkoa shilingi 153,594,369.55 na Polisi inayodaiwa shilingi 101,229,537.40.
Alizitaja taasisi nyingine kuwa ni shule ya Wavulana Songea
shilingi 4,916,661.60 Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya
Songea shilingi 4,340,451.92, Manispaa ya Songea shilingi 6,574,868.79 Ofisi ya
Katibu tawala mkoa wa Ruvuma (RAS) shilingi 51,306,330.27, Chuo cha Ualimu
Songea (TTC) shilingi 12,852,690.00, shule ya sekondari London shilingi
12,920,563.50 na idara ya Maliasili inadaiwa shilingi 1,452,279.60.
Idara ya uhamiaji inayodaiwa jumla ya shilingi milioni 5,502,177.70
ambayo hivi sasa imekwisha katiwa huduma ya maji tangu mwezi Februari mwaka huu
ambapo Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge ameiomba Mamlaka hiyo
kurejesha huduma ya maji kwa kuwa juhudi za kulipa deni hilo zinaendelea na Ofisi
ya uhamiaji makao makuu Jijini Dar es Salaam.
Dokta Mahenge amewaagiza Wakuu wa idara hizo kwenda kusimamia
ipasavyo matumizi ya maji na ikiwezekana kufunga mita za maji ili kuepusha
matumizi makubwa ya upotevu wa maji usiokuwa wa lazima katika taasisi zao.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa aliongeza kuwa ni lazima idara
na taasisi hizo zilipe madeni hayo kwa wakati ili kuweza kuifanya Mamlaka hiyo
ya maji kuzalisha maji kwa wingi ambayo asilimia kubwa uzalishaji wake umekuwa
ukifanywa kwa kusukumwa na mashine zinazotumia nishati ya umeme katika kutoa
huduma husika kwa wananchi.
Alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona licha ya SOUWASA
ikijitahidi kuboresha huduma zake, lakini taasisi hizo za umma hazilipi ankra
za maji kwa wakati badala yake zimekuwa zikilimbikiza madeni yao kwa muda mrefu
na kufikia hatua ya kuwa makubwa.
Hata hivyo kwa upande wake Mhasibu wa Mamlaka hiyo ya maji, Leonard
Luhagila alifafanua kuwa gharama ya kuendesha mitambo ya kusukuma na kuzalisha maji
kwa nguvu ya umeme, kwa mwezi ni kati ya shilingi milioni 20 hadi 25 na kwamba hivi
sasa mamlaka imekuwa ikidaiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani
Ruvuma zaidi ya shilingi milioni 30.
No comments:
Post a Comment