Friday, August 11, 2017

WAKULIMA WAILILIA SERIKALI WAIOMBA IWARUHUSU KUUZA MAHINDI YAO NJE YA NCHI

Na Mwandishi wetu,     
Songea.

LICHA ya serikali kuwataka wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya chakula kama vile mahindi kutopeleka nje ya nchi kwa ajili ya kuyauza, baadhi ya wakulima mkoani Ruvuma wameiomba serikali kuwaruhusu kupeleka huko kwa ajili ya kutafuta soko ili kunusuru hasara itakayoweza kuwapata kutokana na wengi wao kuwa na mahindi mengi.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa baadhi yao Cosmas Ndunguru na Iman Mapunda walisema kuwa serikali haina budi kuwaonea huruma na kulegeza masharti iliyoweka ili kuweza kutoa fursa kwao kwa lengo la kuweza kupata soko la uhakika.

Walisema kuwa lengo la serikali kuzuia mahindi yasiuzwe nje ya nchi ni jambo zuri kwani linalenga kuchukua tahadhari ya kutokea kwa tatizo la njaa hasa katika mikoa yenye upungufu mkubwa wa chakula lakini waliongeza kuwa kutokana na uzalishaji kuwa mkubwa hata wakiruhusu kuuza mahindi nje bado taifa litakuwa na akiba ya kutosha ya chakula.


Said Kondo ambaye ni mkulima wa kijiji cha Matepwende wilayani Namtumbo mkoani humo alieleza kuwa ni vyema serikali ikawaonea huruma wakulima hao kwa kusikiliza kilio chao ili waweze kupata fedha za kuendeshea maisha yao na shughuli mbalimbali za kimaendeleo kutokana na wengi wao hutegemea kupata fedha kupitia sekta ya kilimo.

Kondo alisema baadhi ya wakulima wamekwisha anza kuuza mahindi yao kwa walanguzi ambao hupita vijijini na kuwalaghai wakulima ili wayauze kwa bei ndogo, kwa sababu hata Wakala wa  Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) hajaanza kununua mahindi na haijulikani soko lake litafunguliwa lini.

Vilevile Cosmas Ndunguru aliongeza kuwa mbali na kuipongeza serikali kwa hatua nzuri inayochukua dhidi ya watumishi  wabadhirifu wa mali za umma na wale wanaowanyonya wakulima, ameiomba pia kuangalia uwezekano wa kupeleka fedha za kutosha NFRA ili iweze kununua kiasi kikubwa cha mazao hasa mahindi kwa bei nzuri ili wakulima waweze kuondokana na adha wanayoendelea kuipata hivi sasa.


Pia alifafanua kuwa serikali isipofanya hivyo kuwasaidia wakulima kuwatengenezea soko zuri la kuuza mazao yao wanayolima kuna hatari ya wakulima wengi Tanzania kuendelea kuwa maskini kwa kunyonywa na wajanja wachache wanaotumia nafasi ya ukosefu wa soko la uhakika kununua mazao yao kwa bei ndogo isiyolingana na gharama ya uzalishaji shambani.

No comments: