Na Kassian
Nyandindi,
UMUHIMU wa
maji katika maisha ya binadamu au kiumbe chochote kile kilichokuwa hai hapa
duniani ni jambo ambalo halina mjadala, kutokana na hilo ndio maana serikali
mara zote imekuwa ikihimiza umuhimu wa kutunza mazingira ili kunusuru vyanzo
vya maji vilivyopo viweze kuwa endelevu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Tatizo la
kukosekana kwa maji linaweza kusababisha matatizo mengi katika jamii
ikiwemo kutokea kwa magonjwa ya mlipuko na maji hayo endapo yanapatikana
kwa shida, hugeuka na kuwa karaha hasa kwa akinamama ambao ndio watu
wanaohusika kwa kiasi kikubwa kuyatafuta.
Baada ya
kuona umuhimu huo, serikali imeamua kuanzisha Mamlaka za maji ambazo zimekuwa
zikisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza au kuondoa tatizo la upatikanaji wa maji
katika maeneo ya miji.
Halmashauri
ya mji wa Mbinga iliyopo mkoani Ruvuma, kuna Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa
Mazingira (MBIUWASA) ambayo hivi sasa imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa
mji huo, katika kuendeleza huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Mwandishi wa
makala haya kwa kushirikiana na vyanzo mbalimbali vya habari amebaini kuwa
katika mji huo kumekuwa na vyanzo sita vya maji, ambavyo vimeainishwa kwa ajili
ya kuhudumia wananchi ili waweze kuondokana na tatizo la upatikanaji wa huduma
hiyo muhimu.
Kwa mujibu wa
taarifa ya maendeleo ya utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa mji wa Mbinga
inafafanuliwa kuwa, mkakati uliopo sasa ni kuongeza na kuboresha vyanzo vya
uzalishaji maji vilivyopo kutokana na hitaji la maji katika mji huo kuwa kubwa.
Chanzo
kilichopo sasa ambacho kinatumika katika kuzalisha nishati hiyo muhimu ni
kimoja tu ambacho ni cha Ndengu, hakitoshelezi hitaji hilo la maji hivyo
mikakati imewekwa ili kuondoa tatizo hilo sugu na kwamba tayari ujenzi wa
miundo mbinu mipya ya maji yaani vyanzo vingine vinne vya Lupembe umeanza
kufanyika ikiwemo tenki moja kubwa la kupunguza msongo wa maji na matenki
madogo manne ya kukusanyia maji, ambapo katika kipindi cha miezi mitatu kazi
hiyo imeelezwa kwamba itakuwa ujenzi wake umekamilika.
Pamoja na
ujenzi huo kuendelea kufanyika pia uchimbaji wa mitaro nayo inajengwa kwa ajili
ya kuweza kufukia mabomba makubwa yatakayoleta maji kwa wingi zaidi katika mji
huo.
Meneja wa
MBIUWASA, Patrick Ndunguru akizungumzia hilo anaeleza kuwa changamoto kubwa
waliyonayo sasa ni uchakavu wa miundombinu ya kuleta maji hayo kutoka kwenye
chanzo cha Ndengu hadi Mbinga mjini, ambapo miundombinu yake ni ya zamani
imejengwa mwaka 1970 hivyo imekuwa ikisababisha upotevu mkubwa wa maji ambayo
yanapaswa kuwafikia walaji.
Ndunguru
anafafanua kuwa hayo yote yanatokana na uwezo mdogo wa uzalishaji maji
unaosababishwa na kupanuka kwa mji, unahitaji kupanuliwa kwa miundombinu hiyo
haraka, kwani uzalishaji uliopo sasa ni mita za ujazo 2,100 kwa siku
ikilinganishwa na mahitaji halisi yanayohitajika ni mita za ujazo 5,248.
Aidha
anabainisha kuwa katika kuendeleza na kuboresha huduma hiyo muhimu anaishukuru
Serikali, kupitia Wizara ya maji na umwagiliaji imetenga shilingi Bilioni 1
katika bajeti yake ya mwaka 2017/2018 ambazo zitawezesha kupanua bomba kuu la
uzalishaji maji hivyo kumudu ongezeko kubwa la mahitaji ya maji kufika katika
eneo la mji.
“Vilevile
Wizara imekuwa ikitoa fedha kwa awamu kwa lengo la kuweza kukamilisha mradi huu
mkubwa ambao tumeanza kuujenga hapa lengo kuu ni kuongeza uwingi wa maji,
katika mwaka 2017 hadi 2018 malengo yetu pia ni kujenga machujio ambayo kazi
yake kubwa ni kutibu maji kabla hayajasafirishwa kwenda kwa watumiaji”, alisema
Ndunguru.
Anaongeza
kuwa mradi huo unalenga kupanua huduma kwa kuyafikisha maji katika maeneo mengine ya mji huo
ambayo hayajafikiwa na huduma ambapo ujenzi wake utakuwa unatekelezwa kwa
awamu, kulingana na kiasi cha fedha watakachokuwa wanapata hivyo anaiomba
serikali kupitia wizara husika iendelee kutoa fedha za ujenzi wa miundombinu
hiyo ili mradi uweze kukamilika ujenzi wake.
Mamlaka ya
Maji safi na usafi wa mazingira katika mji huo wa Mbinga kwa ujumla ilianza
kazi yake rasmi Septemba Mosi mwaka 2003 ambapo tokea kuanzishwa kwake mpaka
sasa ina jumla ya wateja 2,426 ambao wameunganishiwa maji na kufungiwa mita.
Hivyo basi, eneo
hilo la mji lina jumla ya wakazi 59,655 kati ya hao 27,501 wanaishi kwenye eneo
la mtandao wa bomba la maji hayo safi na salama ambapo ni sawa na asilimia 46.1
huku uzalishaji wa maji ukiwa ni mita za ujazo 58,967 kwa mwezi, ambapo maji
yanayopotea kutokana na uchakavu wa miundombinu hiyo yanakadiriwa kuwa ni mita
za ujazo 17,191 sawa na asilimia 29.2.
Katika
kupambana na tatizo hilo ndio maana Wizara ya maji na umwagiliaji kwa
kushirikiana na Mamlaka hiyo, imeanza sasa kuboresha miundombinu ambayo ni
chakavu ili kuweza kuondokana na changamoto hii ambayo imedumu kwa miaka mingi
sasa.
Ndunguru
anaeleza kuwa changamoto nyingine iliyopo mbele yao ni pamoja na baadhi ya
wateja kutolipia ankra zao za maji kwa wakati, hivyo kuifanya mamlaka ishindwe
kutekeleza majukumu yake ipasavyo ambapo anatoa wito kwa wateja wote waliopo
ndani ya mji wa Mbinga ambao wameunganishiwa huduma hiyo ya maji walipe ankra
hizo ili mamlaka iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
Anasema
tahadhari iliyopo sasa kwa wananchi ni kwamba wajiepushe na vitendo vya wizi wa
maji kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha maendeleo ya mradi hivyo anaonya pia
kwa watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa maoni
yangu, sote tunatambua kuwa maji ni muhimu kwa maisha yetu ya kila siku hivyo
kinachotakiwa kwa jamii ni kushiriki kikamilifu kuhakikisha vyanzo vinavyozalisha
maji hayo vinatunzwa vizuri ili visikauke na kwamba njia mojawapo ya kuvitunza
ni kuacha tabia ya kuchoma moto misitu, kulima karibu na vyanzo hivyo au
kulisha mifugo na kila mwananchi anapaswa kuwa mlinzi wa chanzo cha maji
kilichopo jirani naye.
Imekuwa ikisisitizwa mara tunapoona kuna tatizo katika eneo jirani la uharibifu
wa mazingira tusisite kutoa taarifa katika mamlaka husika na viongozi waliopewa
dhamana ya kuongoza eneo ambalo uharibifu huo umetokea, wanalojukumu pia la
kuhakikisha kwamba kila wanapofanya mikutano nao wasisite kuwaelimisha wananchi
juu ya umuhimu wa kutunza mazingira hayo na vyanzo vya maji ambapo tukifanya
hivi tutaweza kuondokana na tatizo la ukosefu wa maji safi na salama.
No comments:
Post a Comment