Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge amewataka
Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za mkoa huo kukamilisha ujenzi wa skimu
zote za umwagiliaji zilizopo mkoani hapa, ili ziweze kuanza kutumika kwa kilimo
cha umwagilliaji.
Lengo la kukamilisha ujenzi huo Mkuu huyo wa mkoa alisema utaweza kuleta tija kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa mazao badala ya
kutegemea kilimo cha msimu wa mvua.
Dokta Mahenge alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki alipokuwa
akizungumza na wakurugenzi watendaji, wenyeviti wa halmashauri na wakuu wa
wilaya wa mkoa huo katika kikao cha kazi kilichofanyika Ikulu ndogo mjini
Songea.
Alisema kuwa mbali na miradi hiyo kuongeza tija katika
uzalishaji itasaidia pia kuongeza thamani ya mazao kwa kuyasindika kabla ya kuuza
sokoni.
“Tengeni maeneo maalum pia kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ili
kuweza kuongeza thamani ya mazao watakayokuwa wanazalisha wakulima, hakikisheni mnaweka
mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa viwanda vya usindikaji vyakula, utengenezaji
wa vyakula vya mifugo na mazao mengine”, alisema Dokta Mahenge.
Alisisitiza kuwa serikali inaendelea kuhimiza kuwa kila
halmashauri inapaswa kutenga maeneo kwa ajli ya shughuli za viwanda ambavyo
baadaye vinapojengwa vinaweza kuleta ajira kwa vijana, wanawake na makundi
mengine.
No comments:
Post a Comment