Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WILAYA ya Songea mkoani Ruvuma inakabiliwa na tishio la
kugeuka kuwa jangwa kutokana na wananchi wanaoishi wilayani humo kukata miti
hovyo huku wengine wakichoma misitu moto na baadhi ya watumishi wa serikali
wasiokuwa waadilifu kuruhusu wafugaji kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini
kuingiza idadi kubwa ya mifugo bila kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.
Mkuu wa wilaya hiyo, Pololet Mgema alisema hayo jana wakati
akitoa salamu za serikali katika kikao cha baraza la Madiwani halmashauri
wilaya ya Songea kilichofanyika katika kijiji cha Lundusi kata ya Maposeni
wilayani humo.
“Kuna uharibifu mkubwa katika mlima Lihanje na nimekuwa
nikitoa maagizo kwa watendaji wetu mara kwa mara kusitisha shughuli za kilimo
katika mlima ule hata hivyo bado imeonekana baadhi ya wananchi wanaendelea
kukata miti hovyo na kuendesha shughuli zao za kibinadamu, kuna watumishi pia
ambao ni wagumu kutekeleza maagizo ya serikali sasa mimi mwenyewe nitaanza
operesheni ya kuwaondoa ndugu zenu lakini msije kunilaumu kwa hatua
nitakayochukua”, alisisitiza Mgema.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya alifafanua kuwa ataanza
kupita kila kijiji hadi kijiji kwa ajili ya kuwatangazia wananchi kuhusiana na
mpango wa serikali kuutunza mlima huo kutokana na umuhimu wake baada ya kuona
watumishi waliopewa dhamana ya kusimamia suala zima la uhifadhi wa mazingira
katika mlima Lihanje kushindwa kutimiza wajibu wao kwa sababu wanazozijua.
Mgema amewataka watumishi na madiwani kusimamia ipasavyo
agizo la serikali la kutoruhusu uingizaji mifugo kutoka mikoa mingine na kuzuia
biashara ya kuchoma mkaa ambayo ndiyo chanzo kikuu cha uharibifu wa misitu.
Hata hivyo alisema hatua isipochukuliwa mapema kuna hatari
kubwa siku za usoni katika wilaya hiyo kuwepo kwa idadi kubwa ya mifugo
isiyolingana na ukubwa wa ardhi iliyopo hivyo kuwa na uwezekano wa kutokea vurugu
kati ya wakulima na wafugaji wakigombania ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo
na ufugaji.
No comments:
Post a Comment