Na Mwandishi wetu,
Arusha.
SERIKALI hapa nchini, imeagiza Halmashauri zote ambazo
hazijakamilisha mpango wa taifa wa kutoa huduma za vipimo kwenye zahanati
na vituo vya afya kuhakikisha kwamba inakamilisha huduma hiyo, ndani ya miezi
mitatu kuanzia sasa.
Agizo hilo limetolewa juzi na Naibu Waziri wa afya, Dokta Khamis
Kigwangala katika ziara yake ya siku tano, wakati alipokuwa akitembelea vituo
vya Afya na zahanati za Jiji la Arusha kwa lengo la kuangalia utendaji kazi na
changamoto zilizopo katika kutekeleza agizo la uboreshaji wa huduma ya upimaji
wa magonjwa mbalimbali.
Dokta Kigwangala alisema kuwa Rais Dokta John Pombe Magufuli
alikwisha toa maelekezo ya kuimarisha na kuboresha kwa huduma za afya kuanzia
ngazi ya zahanati na vituo hivyo vya afya alipokuwa akifungua kikao cha Bunge
mjini Dodoma, kwa lengo la kuokoa maisha ya wananchi ili waweze kupata vipimo
vya magonjwa katika maeneo wanayoishi kwa urahisi.
Alisema kuwa Wizara ya afya katika kuhakikisha agizo hilo la Rais Dokta
Magufuli linatekelezwa ipasavyo imetoa msisitizo wa utekelezaji huo ikiwemo pia hata sera
ya Wizara hiyo inazitaka halmashauri zote kuhakikisha kwamba huduma hiyo ya
vipimo vya magonjwa ya kawaida inapatikana kuanzia kwenye ngazi ya zahanati
hadi vituo vya afya.
Alifafanua kuwa serikali iliagiza pia kuanzishwa kwa huduma
ya upasuaji mdogo na vipimo hivyo lakini inashangazwa kuona halmashauri ya Jiji la
Arusha haijatekeleza kikamilifu maagizo hayo.
Vilevile aliongeza kuwa Wizara ya afya ilikwisha toa agizo kwa
kusisitiza utekelezaji wake kwenye kikao kilichofanyika Mwandoya wilaya ya
Meatu mkoani Simiyu na kwamba haitaki kusikia kwamba kumekuwa na visingizio vinavyokwamisha
utekelezaji huo.
Pia alisisitiza kuwa Wizara ipo tayari kuzichukulia
hatua halmashauri zote ambazo zitapuuza maagizo yake kwa kutofanyia
utekelezaji kuanzia sasa na hakuna atakayebakia salama iwapo ameshindwa
kutekeleza majukumu yake.
Waziri Dokta Kigwangala, licha ya kutembelea maeneo hayo ya
vituo vya kutolea huduma ya afya pia amekutana na changamoto mbalimbali ikiwemo
vituo vya afya kutokuwa na vyumba vya upasuaji kwa ajili ya akina mama
wajawazito kujifungulia na baadhi ya mashine za kuchunguza magonjwa kutofanya
kazi.
Hata hivyo aliagiza kwa kuitaka halmashauri hiyo ambayo
inakusanya kodi zaidi ya shilingi bilioni 12 kwa mwaka kutatua kero hizo haraka
na kwamba kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Jiji la Arusha, Rebeca
Mongi alisema kuwa halmashauri yake itatekeleza na kutatua kero hizo mapema ikiwemo
kukamilisha maelekezo na maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri wa afya Dokta
Kigwangala.
No comments:
Post a Comment