Na Muhidin Amri,
Songea.
MANISPAA ya Songea mkoani Ruvuma imenunua mtambo wa kisasa wa
kuzolea taka (Kijiko) ambacho kitaalamu kinafahamika kwa jina la Back hoe
loader kilichogharimu zaidi ya shilingi milioni 170 kutoka kampuni ya Hansom
Tanzania Limited ambapo Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoani humo amekagua
mtambo huo na kuthibitisha kuwa upo salama.
Afisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alimweleza
mwandishi wetu kuwa tayari mtambo huo umeanza kufanya kazi ya ukusanyaji wa
taka ngumu katika viunga vya Songea, hivyo kuweza kupunguza muda wa kuzoa taka
kwa kutumia nguvu kazi hali ambayo imesaidia kuufanya mji wa Songea kuonekana kuwa
wa kuvutia kutokana na kasi ya kuondoa taka hizo zilizokuwa kero kubwa katika
maeneo mbalimbali ya mji huo.
Midelo alisema kuwa kwa wastani Manispaa ya Songea imekuwa
ikizalisha taka kiasi cha tani 71.5 kwa siku ambapo uwezo wa Manispaa hiyo
kuzoa taka hizo kwa siku ni kati ya tani 35 hadi 40 na kwamba hivi sasa inatarajia
kuongeza uwezo wake wa kuzoa taka hizo kwa siku kutokana na kununua mtambo huo.
Alisema Manispaa hiyo ambayo ina kata 21 na mitaa 95 ina
jumla ya wakazi 218,942 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Katika hatua nyingine Midelo alieleza kuwa imekuwa ikifanyika
kazi ya ujenzi wa bustani ya kisasa ya halmashauri ya Manispaa ya Songea ambayo
itaweza kubadilisha muonekano wa Manispaa hiyo kwamba kazi hiyo imeanza
kufanyika katika eneo ambalo lipo katikati ya viunga vya mji huo.
Afisa habari huyo alibainisha kuwa mradi huo ambao ujenzi
wake utakamilika katika kipindi cha miezi sita ni miongoni mwa miradi ambayo
inafadhiliwa na Benki ya dunia ambao unatarajia kugharimu shilingi milioni 399.
Midelo alisema kuwa ramani ya mradi huo ambao ni wa aina yake
katika mji wa Songea inaonesha kuwa utazungukwa na eneo la kulipia kwa ajili ya
kuegesha magari, vyoo vya kulipia na vibanda vya kupumzikia.
Pia mradi huo utakuwa na maeneo kwa ajili ya kuchezea watoto,
hoteli kwa ajili ya kupata chakula na vinywaji, huku likijengwa na eneo maalumu
la kupata taarifa za uwekezaji na utalii katika Manispaa na mkoa wa Ruvuma kwa
ujumla.
“Jambo la kufurahisha hapa ni kwamba bustani hii itapandwa pia
miti na nyasi ambazo zitaongeza kuwa na mandhari nzuri na muonekano wa kuvutia kwa
Manispaa yetu ya Songea kwa kuwa bustani ipo katikati ya mji wa Songea”,
alisema Midelo.
No comments:
Post a Comment