Na Mwandishi wetu,
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dokta Hamis Kigwangalla
amewataka wamiliki na waendeshaji wa hoteli za daraja la kati kumwandikia
mapendekezo yatakayomwezesha kutoa uamuzi sahihi, juu ya namna wanavyoweza
kuchangia mapato ya nchi.
Dokta Hamis Kigwangalla. |
Akizungumza jijini hapa leo Dokta Kigwangalla alisema kuwa
uchunguzi umebaini kuwa hoteli zenye hadhi ya kati na nyumba za kulala wageni
maarufu 'Guest House' zimekuwa zikipokea watalii wengi kutokana na ubora wake
unaochangiwa na unafuu wa bei.
Waziri huyo alieleza kuwa tafsiri ya watalii haimaanishi
Wazungu pekee bali ni wageni wowote wanaotumia nyumba za kulala wageni, kutoka
nje ya eneo hilo wakiwemo wanaofika kwa ajili ya mikutano na shughuli za
biashara.
“Mnaweza kuniambia hoteli zetu zina hadhi ya chini kwa sababu
bei ya chumba ni kati ya Shilingi 40,000 hadi 70,000 lakini tunafahamu hizi
hoteli Wazungu wameshazijua na wanalala kwenye hoteli zenu na mnaweza kuanza
kuwatoza kwa dola”, alisema Kigwangalla.
Alisema kuwa lengo la Serikali ni kuwawezesha kukusanya
mapato yatakayosaidia kuipatia uwezo wa kuhudumia wananchi kwenye sekta
mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, usambazaji wa huduma
ya maji, elimu na afya.
Mmoja wa wamiliki wa hoteli hizo, Amani Charles kwa upande
wake alisema wanakusudia mapendekezo watakayowasilisha kwa Dokta Kigwangalla
baada ya kukubaliana yatawawezesha kufanyabiashara kwa njia nzuri badala ya
kunyonywa kimapato kutokana na kutokuwepo usawa wa malipo.
Aliongeza kuwa mkanganyiko wa malipo unatokana na wao
kutakiwa kulipa kwa dola ya Marekani 1.5 kwa kitanda, ambayo ni karibu ni sawa
na Shilingi 2,000 wakati wateja wao wanalipa kwa fedha za Kitanzania huku
uamuzi wa kulipa kwa kiwango maalumu kwa mwaka au kwa asilimia kulingana na
wateja wanaolala.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema utaratibu
ambao umewekwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Arusha utaendelea,
kwa sababu Serikali imeweka malengo ya makusanyo na wale ambao ukadiriaji wa
mapato yao umefanyika hivi karibuni utapatiwa majibu na Waziri wa Maliasili na
Utalii.
No comments:
Post a Comment