Na Kassian Nyandindi,
Songea.
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu
la Songea, Damian Dallu amesema kwamba suala la kuombea amani hapa nchini halitaweza
kufanikiwa, endapo kama vyombo vya dola havitazingatia utoaji wa haki kwa wananchi
wake.
Dallu alisema hayo jana wakati
alipokuwa akihubiri kwenye ibada ya misa takatifu ya Jumatano ya majivu,
iliyofanyika katika Kanisa kuu la kiaskofu la mtakatifu Mathias Kalemba mjini
Songea.
Alisema kuwa amani haiwezi kupatikana
katika taifa lolote lile kama vyombo vya dola havitatenda haki kwa wananchi
wake, huku akidai kuwa ili amani iweze kudumishwa na kuwa endelevu ni lazima
vyote viwili viende kwa pamoja.
Vilevile Askofu huyo amewataka
waumini hao kuanzia ngazi ya familia, ofisi, taasisi mbalimbali pamoja na
vyombo hivyo vya dola kuhakikisha vinatoa haki sawa kwa wananchi, watumishi na
wafanyakazi wao mbalimbali kwa lengo la kudumisha amani iliyopo na mshikamano huu
tulio nao.
Alisisitiza kuwa suala la kudumisha amani
linatakiwa lianzie ndani ya mioyo ya watu na sio kuzungumzia mdomoni peke yake,
badala yake ijidhihirishe kwa vitendo ikiwa pamoja na kutenda haki kwa wananchi
wake.
Kadhalika kufuatia hali hiyo aliwaomba
waumini hao kutumia kipindi hiki cha mfungo wa Pasaka kwa ajili ya kuwasaidia
watu wenye mahitaji muhimu wakiwemo watoto yatima, wafungwa, wagonjwa pamoja na
wazee wasiojiweza.
Pia Askofu Dallu aliendelea kuwaasa
waumini hao kutumia kipindi cha kwaresma kwa ajili ya kuachana na mambo ya
anasa na kujinyima mahitaji yao muhimu ambapo amedai kuwa lengo la kufanya
hivyo ni kuwasaidia watu hao wenye mahitaji muhimu ambao hawajiwezi.
No comments:
Post a Comment