Na Muhidin Amri,
Tunduru.
WANANCHI wa kijiji cha Kalulu kata ya Kalulu Halmashauri ya
Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, wameipongeza Serikali kwa jitihada zake
inayofanya katika kupunguza kero za muda mrefu zinazokwamisha kasi ya ukuaji wa
maendeleo kwa wananchi vijijini Wilayani humo.
Aidha wananchi hao wamepongeza kazi kubwa zinazofanywa na
Meneja wa Wakala wa Barabara (TARURA) Mhandisi, Cyprian Kimwaga kwa kutengeneza
barabara inayoanzia kijiji cha Milonde hadi Kalulu Wilayani hapa, kwa kiwango
cha changarawe jambo ambalo limewezesha magari kuanza kupita kwenda katika
vijiji hivyo ambapo ni muda mrefu yalikuwa yanashindwa kwenda huko kutokana na
barabara hiyo kuwa na hali mbaya.
Wakizungumza na kwa nyakati tofauti, jana baadhi ya wananchi walisema
kuwa usimamizi na mipango ya TARURA Wilayani Tunduru imefanikisha kutengenezwa
kwa barabara hiyo ambayo kwa muda mrefu ilikuwa kero kubwa katika jamii.
“Kwa kweli lazima tukubali tangu Serikali yetu ilipoanzisha Wakala
wa Barabara TARURA kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kuimarika kwa miundombinu
ya barabara katika kijiji chetu, tunafurahi kuona magari yanafika kwa wingi
katika kijiji hiki kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri, tunaipongeza sana
Serikali yetu”, alisema Said Kalolo mkazi wa kijiji cha Kalulu.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala huyo wa barabara Wilayani
Tunduru, Cyprian Kimwaga aliongeza kuwa ukarabati wa barabara hiyo umefanyika
kwa juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais
Dokta John Pombe Magufuli, kwa uamuzi wake wa kutoa fedha kwa ajili ya
ukarabati wa barabara hiyo na nyingine katika Wilaya hiyo.
Kimwaga alisema kijiji cha Kalulu kina umuhimu mkubwa kwani
ni moja kati ya maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao mbalimbali ya chakula
na biashara ambayo ndiyo yanaingiza mapato makubwa kwa Halmashauri ya Wilaya
hiyo na Serikali kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment