Hii ni moja kati ya nyumba ambayo imeezuliwa na upepo mkali ulioambatana na mvua katika kijiji cha Njalamatata kata ya Mkongo Nakalawe Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma. |
Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
UPEPO mkali uliokuwa umeambatana na mvua katika kijiji cha
Njalamatata kata ya Mkongo Nakalawe Wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma, umeleta
maafa kwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho kuezuliwa nyumba zao na kukosa
mahali pa kuishi.
Tukio hilo limetokea juzi majira ya mchana baada ya nyumba
tano kuezuliwa kwenye kijiji hicho na kufanya wakazi hao, wakibaki wanahangaika
kutafuta mahali pa kujihifadhi kwa majirani zao.
Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo ikiwa imeongozana
na Katibu tawala wa Wilaya ya Namtumbo, Adelin Nchimbi walikwenda katika eneo
hilo la tukio na kuzungumza na waathirika ambao nyumba zao zimebomolewa na upepo
huo uliokuwa umeambatana na mvua hiyo.
Walipofika katika eneo la tukio Kamati hiyo ilishuhudia
nyumba tano zikiwa zimeezuliwa katika kijiji hicho cha Njalamatata, lakini hapa
kujitokeza mwananchi yeyote aliyejeruhiwa.
Kamati hiyo iliweza kubaini kwamba hasara hiyo
iliyojitokeza ilitokana na nyumba hizo kujengwa chini ya kiwango.
Akizungumza na waathirika hao katika eneo la tukio Katibu
tawala wa Wilaya ya Namtumbo, Nchimbi alitoa msisitizo na kuwaelekeza wakazi
hao kuzingatia ubora na taratibu husika wakati wanapojenga nyumba zao ili
wasiweze kupata hasara kama hiyo.
Pamoja na mambo mengine, wananchi walioathirika ni Clavery
Ponera, Donatus Kapinga, James Mdagi, Sadick Kapinga, Rusti Kimbili na Lotary Hongo
ambao wote ni wakazi wa kijiji hicho Wilayani hapa.
No comments:
Post a Comment