Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WATU Watano wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa
vibaya katika matukio mawili tofauti, akiwemo diwani wa kata ya Peramiho Issack
Mwimba (37) amefariki papo hapo baada ya kugongwa na gari wakati akiwa anaendesha
Pikipiki, akitokea Peramiho kuja Songea mjini.
Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma, Gemini Mushy akizungumza jana
na mwandishi wa habari hizi aliwataja wengine waliofariki kuwa ni Ally Hamis Blanket
(34) ambaye ni mkazi wa Songea mjini, Maria Njelwa (35), Seba Chichango (28) na
abiria mwingine wa jinsia ya kiume ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara
moja ambao wote ni wakazi wa kijiji cha Ng’ombo Wilaya ya Nyasa Mkoani hapa.
Alifafanua kuwa katika tukio la kwanza ambalo lilitokea
Februari 24 mwaka huu majira ya asubuhi huko katika maeneo ya Ruhuwiko mabwawani
nje kidogo ya Manispaa ya Songea, kwenye barabara ya kutoka Songea kwenda Wilaya
ya Mbinga gari lenye namba za usajili T 604 CXV aina ya Toyota Cresta,
ambalo lilikuwa
linaendeshwa na John Samwel Mbwambo mkazi wa Bombambili katika Manispaa hiyo
likitokea Peramiho kwenda songea mjini, liligonga Pikipiki yenye namba za
usajili MC 232 ARJ aina ya SANLG iliyokuwa ikiendeshwa na Issack Mwimba ambaye
ni diwani wa kata ya Peramiho kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
kusababisha majeraha makubwa yaliyosababisha kifo chake.
Vilevile Kamanda Mushy alieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni
uzembe wa dereva wa gari hiyo na kwamba Polisi inamshikilia dereva aliyekuwa
akiendesha gari hilo na taratibu za kisheria zimekamilika hivyo anatarajiwa
kufikishwa Mahakamani mapema wiki hii.
Alibainisha kuwa Februari 24 mwaka huu majira ya saa 11
alfajiri katika kijiji cha Kigonsera Wilayani Mbinga Mkoani humo, pia gari
lenye namba za usajili T 405 DHT aina ya Mitsubishi Canter lililokuwa linatoka kijiji
cha Ng’ombo Mbamba bay Wilayani Nyasa likiwa limesheheni mzigo wa dagaa Nyasa ambalo
lilikuwa linaendeshwa na dereva aliyejulikana kwa jina la Blanket, liliacha
njia kisha kupinduka na kusababisha vifo kwa dereva wa gari huyo pamoja na
abiria watatu ambao aliwataja abiria hao kuwa nia Maria Njelwa, Seba
Chichango na mwingine wa jinsia ya kiume jina lake halikuweza kufahamika mara
moja.
Kamanda Mushy aliwataja majeruhi kuwa ni Angel Mwasi (26)
mkazi wa Bombambili Songea mjini, Kawaida Abdallah (23) ambaye ni fundi magari
mkazi wa Makambi Songea mjini, Hamis Halifa Rashid (27) mkazi wa Tunduru,
Cosmas Mahungo (29) mkazi wa Makalole Tunduru, Edina Islam Ngonyani mkazi wa
Mahenge Songea na Amri Mbawala (27) mkazi wa Majengo Songea na kwamba majeruhi
wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Serikali Wilayani Mbinga
na chanzo cha ajali hiyo ni dereva kushindwa kumudu usukani wa gari hiyo akiwa
kwenye mteremko mkali.
No comments:
Post a Comment