Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, Beda Hyera amewajia juu baadhi ya viongozi
wa kijiji cha Kihungu katika kata ya Kihungu Halmashauri ya Mji wa Mbinga
Mkoani humo kutokana na kushindwa kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya kijiji hicho.
Kufuatia hali hiyo, Hyera ametoa siku
saba kwa viongozi hao kuhakikisha kwamba wanasimamia na kukamilisha ujenzi huo mapema
iwezekanavyo, kuanzia Februari 5 mwaka huu kwani wananchi walikwisha changia fedha
na uongozi wa Halmashauri hiyo ulitoa vifaa vya kiwandani kwa ajili ya kukamilisha
kazi hiyo.
Hyera aliwanyoshea kidole viongozi wa
kijiji hicho ambao ni Mwenyekiti wa kijiji Adam Ngongi na Mtendaji wa kijiji
Denice Ndunguru kuwa ndiyo wanaokwamisha ujenzi huo usiweze kuendelea ipasavyo kutokana
na kutunishiana misuli kwa sababu zisizokuwa na maana.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti huyo
katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika kata ya Kihungu, kwenye kilele
cha maadhimisho ya sherehe ya kuzaliwa kwa CCM na kutimiza miaka 41
zilizofanyika kiwilaya katika kata hiyo.
Katika kuadhimisha sherehe hizo
viongozi wa Chama cha mapinduzi wakiongozwa na Mwenyekiti huyo wa chama hicho
waliweza kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi hiyo ambayo yamefikia katika hatua
ya ujenzi wa ringbim ili iweze kuezekwa, ujenzi wa Ofisi ya CCM ya kata ambayo
imefikia hatua ya kuezeka bati pamoja na ujenzi wa kituo cha afya Kalembo
kilichopo katika kata hiyo.
“Watendaji wa Serikali waliokwamisha
ujenzi wa Ofisi hii ya kijiji nimemwagiza Mkurugenzi mtendaji achukue hatua,
ili mradi ule pale ulipofikia ndani ya siku saba uwe umekamilika ujenzi wake”,
alisema Hyera.
No comments:
Post a Comment