Akwilina Akwiline. |
HATIMAYE Mazishi ya mwili wa
aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina
Akwiline yatafanyika siku ya Ijumaa Februari 23 mwaka huu Mkoani Kilimanjaro.
Moi Kiyeyeu akizungumza na mwandishi
wetu alisema kwamba baada ya kikao cha familia, wamekubaliana kuwa Akwilina
atazikwa Mkoani humo baada ya kuagwa Februari 22 mwaka huu katika viwanja vya chuo
hicho Mabibo jijini Dar es Salaam.
Akwilina alifariki dunia Februari 16
mwaka huu baada ya kupigwa risasi akiwa kwenye daladala, wakati Polisi
wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na
Maendelea (CHADEMA).
“Tutamuaga ndugu yetu siku ya
Alhamisi katika viwanja vya chuo cha NIT pale Mabibo na siku hiyo hiyo tutaanza
safari kuelekea Rombo-Mashati Olele Mkoani Kilimanjaro na mazishi tutafanya
Ijumaa”, alisema Kiyeyeu.
Ndugu wakusanyika Muhimbili
Kadhalika mwili wa mwanafunzi huyo umepelekwa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo Jumatatu Februari 19 mwaka huu asubuhi.
Mwili wa Akwilina umehamishiwa katika
Hospitali hiyo ukitokea Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kufanyiwa
uchunguzi.
Ndugu wa marehemu wamekusanyika hapo Muhimbili
katika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti, wakisubiri uchunguzi ukamilike ili
kujua hatima ya kuusafirisha kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Wilayani
Rombo Mkoani Kilimanjaro.
Moses Kiyeyeu aliyejitambulisha kuwa
ni kaka wa marehemu alisema madaktari na wahusika wengine wanaendelea na
utaratibu wa uchunguzi wa mwili.
"Mwili umefikishwa hapa tangu
asubuhi na kule ndani kuna kaka yetu ndiye anashuhudia uchunguzi huo, wametuambia
tutoke kwanza ndani watatuita baadaye ili kupewa taarifa nini kinafuata kuhusu
mwili wa ndugu yetu”, alisema.
Hata hivyo Kiyeyeu aliongeza kuwa familia
inasubiri uchunguzi ukamilike ili waruhusiwe kuuchukua mwili kwa kuwa wazazi wa
Akwilina wanausubiri.
No comments:
Post a Comment