Monday, February 26, 2018

TLA YATOA VITABU VYA MASOMO SONGEA


Na Muhidin Amri,           
Songea.

CHAMA cha Wakutubi Tanzania (TLA) kimetoa vitabu 91 vya masomo ya aina mbalimbali kwa shule mbili za Sekondari katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, ikiwa ni mkakati wa Chama hicho kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu hapa nchini.

Shule zilizopata msaada huo ni shule ya Sekondari ya wasichana Songea na ile ya wavulana Songea, pamoja na Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) Songea ambacho nacho kimepata vitabu.

Mwenyekiti wa TLA, Juliana Manyerere alisema kuwa chama hicho hapa Tanzania hakipo nyuma katika suala zima la elimu kwani mwaka jana 2017 kimeweza kutembelea vyuo vinavyoendesha mafunzo ya Ukutubi vya Tumaini, Slads Bagamaoyo na Dar es Salaam pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu Wakutubi 41 wa shule za Sekondari zilizopo katika Manispaa ya Dodoma.


Alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watoa huduma za maktaba kwenye shule za Sekondari ili waweze kuwajengea wanafunzi tabia ya kupenda kujisomea na hatimaye waweze kufanya vizuri kwenye mitihani yao.

Aidha Manyerere ameiomba Serikali kuweka msisitizo kwa shule za Msingi na Sekondari hapa nchini, kuwa na maktaba na kuajiri Wakutubi kwenye maktaba hizo ili kutoa huduma bora na taaluma ya ukutubi kwa wanafunzi.

Kwa upande wake katibu wa Chama hicho, Leontine Nkebukwa alisema wanaunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano katika kukuza viwanda na kuelekea uchumi wa kati na kutunza maarifa ambayo yamehifadhiwa kwenye vitabu, maktaba kwa lengo la kukuza na kusambaza maarifa katika jamii.

No comments: