Na Mwandishi wetu,
Dodoma.
LICHA ya Mkutano wa 10 wa Bunge la 11 uliomalizika juzi kuwa
mahsusi kwa ajili ya kamati za kudumu kuwasilisha taarifa zake ambazo hufuatiwa
na mijadala mizito hasa ya ufisadi, safari hii haikuwa hiyo pekee kwani kuna
mambo matano makubwa yaliyoibuka na kutikisa chombo hicho, baadhi yakiwa
hayatokani na taarifa hizo.
Katika mkutano huo uliofanyika kwa siku 12 na kumalizika
juzi, kamati zilizowasilisha taarifa zake ni; Hesabu za Serikali (PAC); Hesabu
za Serikali za Mitaa (LAAC); Bajeti; Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC); Viwanda,
Biashara na Mazingira.
Nyingine ni Kamati ya Ardhi, maliasili na utalii; Kilimo,
Mifugo na Maji; Miundombinu; Katiba na Sheria; Utawala na Serikali za Mitaa;
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Mambo yaliyotikisa bungeni ni mradi wa hati ya kielektroniki
ya kusafiria, fao la kujitoa, wabunge kutaka ulinzi, uhaba wa maji na utendaji
wa baadhi ya mawaziri.
Hati za kusafiria
Januari 30, Rais Dokta John Magufuli alizindua hati za
kielektroniki za kusafiria jambo ambalo liliibuka bungeni baada ya baadhi ya
wabunge kueleza kuwa mradi huo umegubikwa na ufisadi.
Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde alisema taarifa
zinaonyesha kuwa ufisadi ndani ya nchi bado umeendelea kuwapo na kwamba mradi
huo umekuwa ukitekelezwa kwa gharama za Dola 40 milioni za Marekani.
“Kuna taarifa nimezipata kuwa mradi huo ulikuwa na thamani ya
dola 16 milioni za Marekani sawa na paundi 11 milioni. Kuna taarifa kwamba
kampuni ambayo ilishapewa hati ya makubaliano ambayo hayakusainiwa hadi dakika
ya mwisho, lakini mwisho wa siku ilipewa kampuni ya HID”, alisema.
Alisema kampuni ya HID ambayo imepewa tenda hiyo haijawahi
kufanya kazi ya mradi wa hati za kusafiria mahali popote na imekuwa ikitengeneza
kadi.
Alisema kampuni hiyo imeingia ubia na watu ambao walikuwa
Nida (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa) wakati uliopita.
“Kwa hiyo mheshimiwa mwenyekiti, ufisadi bado upo na uchumi
umeendelea kuyumba lakini watu wameendelea kufichaficha tu kwa namna fulani,
kama tunapinga ufisadi lazima hatua zichukuliwe,” alisema.
Alisema taarifa walizonazo za ndani katika mradi wa hati za
kusafiria kuna ufisadi wa kutisha.
Mbali na Silinde suala hilo lilizungumziwa pia na Mbunge wa
Tarime Vijijini (Chadema), John Heche na mwenzake wa Iringa Mjini, Mchungaji
Peter Msigwa ambaye alitakiwa na Naibu Spika, Dokta Tulia Ackson kuwasilisha
nyaraka za ushahidi kuhusu ufisadi wa mradi huo wa hati za kusafiria kwa kamati
ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge.
Fao la kujitoa
Uliibuka mjadala mkali wa Muswada wa Sheria ya Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa mwaka 2017, huku kambi ya upinzani
bungeni ikipendekeza Serikali kuweka fao la kujitoa kutokana na umuhimu wake.
Muswada huo unalenga kuunganisha mifuko mitano ya hifadhi ya
jamii na kuwa na miwili kwa ajili ya watumishi wa umma na sekta binafsi. Mifuko
iliyopo sasa ni LAPF, PPF, GEPF, PSPF na NSSF na itakayobaki ni NSSF na PSPF.
Mbunge wa Bunda (Chadema), Ester Bulaya alisema kambi hiyo
inaona umuhimu mkubwa wa kuwapo kwa fao la kujitoa kama lilivyokuwa linatolewa
na mifuko iliyokuwapo.
“Bado kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na fao la kujitoa kama
lilivyokuwa linatolewa na mifuko iliyokuwapo. Bado ni la msingi na lazima kwani
mwanachama anakuwa tayari na akiba yake hivyo inakuwa ni mtaji wa kumtoa kwenye
umaskini wa kipato”, alisema.
Mbunge wa Kigoma mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alisema
hakuna namna ya kuendelea kulikwepa fao hilo kama ilivyokuwa kwa miaka minne
iliyopita.
“Huko nje vijana wengi sana wanataka fao hili liwepo, dhamira
ya Serikali na dola yoyote ni kujenga mazingira ambayo mfumo madhubuti wa hifadhi
ya jamii ambao hautakufanya baadaye uwe na wazee ambao hawana pensheni”,
alisema.
Mbunge wa Geita mjini (CCM), Constatine Kanyasu alisema
anatoka katika mkoa ambao una wachimbaji wa madini wengi na mgogoro wake mkubwa
siku nyingi umekuwa ni fao la kujitoa.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri wa Mkuu (Sera,
Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alisema
hakuna nchi yoyote ambayo mifuko ya jamii ina fao la kujitoa lakini Serikali
kwa kutambua umuhimu huo, imeweka fao la upotevu wa ajira.
Wabunge kuomba ulinzi
Siku ya mwisho ya mkutano huo, Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi
na Usalama ilipendekeza kufanyiwa marekebisho Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka
ya Bunge ili kuweka sharti la wabunge kupatiwa ulinzi katika maeneo mbalimbali.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Balozi Adadi Rajabu alisema ulinzi
huo uwe katika makazi ya wabunge wakiwa wanatekeleza majukumu ya kibunge mjini
Dodoma na katika majimbo yao.
Mapendekezo ya kamati hiyo yalionekana kuwagusa wabunge wengi
baada ya mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa wakati akichangia taarifa
hiyo kutoa mfano wa tukio la kupigwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu na hivyo kupendekeza wabunge walindwe.
Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye alitaka Sheria ya Usalama
wa Taifa ifanyiwe marekebisho kwa kuwa inazungumzia ulinzi wa viongozi na si
wananchi wengine.
Wakati Dokta Tulia, akiagiza Serikali kulifanyia kazi suala
la ulinzi na uwekaji wa namba maalumu kwa magari ya wabunge kama
ilivyopendekezwa na kamati, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dokta Mwigulu Nchemba na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora), George Mkuchika walipangua hoja za mapendekezo ya kamati hiyo kuhusu
ulinzi wa wabunge na kuhusishwa na yale yaliyohusu idara ya Usalama wa Taifa.
Hoja ya kukosekana kwa
maji
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Issack Kamwelwe alijikuta
katika wakati mgumu baada ya wabunge wengi kumbana wakitaka majibu ya maji
kutokana na hoja ya dharura ya mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe.
Katika hoja yake, Bashe aliwashtaki mawaziri bungeni akisema
wamekuwa chanzo cha mateso na mahangaiko kwa wananchi wa Nzega lakini akasema
lolote litakalotokea walaumiwe wao.
Bashe aliwataja mawaziri hao kuwa ni Dokta Philip Mpango
(Fedha), Dokta Medrad Kalemani (Nishati), Kamwelwe na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais (Tamisemi), Seleman Jafo kwamba wamesababisha wananchi wa jimbo lake
kukosa maji kwa siku ya 13 mfululizo.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo alipoomba mwongozo akitumia
kanuni ya 47 kuhusu jambo la dharura bungeni na alipopewa nafasi alisema
amekuwa akiwasiliana na Serikali lakini hakuna kinachoendelea na wahusika
wamekaa kimya. Hoja yake ilimuinua Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliyesema
tatizo la maji ni la nchi nzima na kwamba halitakiwi kupuuzwa na kutaka wananchi
watendewe haki maeneo yote.
Licha ya Waziri Mhagama kuagiza mawaziri wa Maji, Nishati na
Fedha kukutana mara baada ya kikao cha Bunge kuahirishwa, jambo hilo
liliendelea kutikisa Bunge.
Mbunge wa Nchemba (CCM), Juma Nkamia naye alieleza ukubwa wa
tatizo hilo katika jimbo lake huku mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete
akieleza jinsi anavyojibiwa kisiasa na Waziri Kamwelwe kuhusu maji.
Hata hivyo, Chenge alizima moto wa wabunge hao baada ya
kusema Serikali imeyachukua maoni yao na itayafanyia kazi.
Mawaziri na mihemko
Mawaziri wawili, Luhaga Mpina na Dokta Hamisi Kigwangalla
walilazimika kutoa majibu ya kina bungeni baada ya kushambuliwa kuhusu utendaji
wao.
Dokta Kigwangalla anayesimamia Wizara ya Maliasili na Utalii
na Mpina ambaye ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, walisema wataendelea kufanya kazi
kwa weledi.
Mbunge wa Busega (CCM), Dokta Raphael Chegeni alimuweka Mpina
katika wakati mgumu baada ya kusema amekuwa na kiburi na kumtaka aache kwa kuwa
anawaumiza wafugaji, akitolea mfano kamatakamata ya mifugo.
Nape alisema hakuna lililofanyika kwa wafugaji tangu Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015 ulipomalizika na kwamba kila wakati Serikali inafanya kazi
ya zimamoto badala ya kujipanga na kushughulikia matatizo ya wananchi
kikamilifu.
Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuph Salum Hussein, alisema
Wizara ya Maliasili na Utalii ni kama yai viza ambalo lina matumizi mazuri kwa
wanaolitumia lakini likikosewa linanuka.
Mchungaji Msigwa naye aligusia wizara hiyo, kubainisha kuwa
Kamati ya Maliasili imepokea malalamiko kutokana na hatua ya Waziri Kigwangalla
kufuta vitalu vya uwindaji.
No comments:
Post a Comment