Na Kassian Nyandindi,
Tunduru.
KATIKA kuchochea kasi ya ukuaji wa maendeleo katika
Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Serikali imeombwa kuongeza
fedha kwa ajili ya ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya barabara hasa
vijijini Wilayani humo, ambazo hazifanyiwa matengenezo kwa muda mrefu.
Imeelezwa kuwa endapo litatekelezwa hilo hata shughuli za
kiuchumi ambazo zinazofanywa na wananchi wataweza kutekeleza kwa urahisi na
hatimaye Wilaya nayo kuweza kunufaika na kupiga hatua katika ukuaji wa mapato
yake.
Hivi sasa kiasi cha fedha kinachotolewa na Serikali kwa ajili
ya ujenzi wa barabara hizo imeelezwa kuwa ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji
halisi yanayotakiwa, kwa kuwa Wilaya hiyo ni kubwa na imekuwa na mtandao mkubwa
wa miundombinu ya barabara wenye urefu wa Kilometa 1,261.2 sawa na Mkoa jirani
wa Mtwara.
Ombi hilo limetolewa jana na Meneja wa Wakala wa Barabara Mjini
na Vijijini (TARURA) Wilayani Tunduru, Mhandisi Cyprian Kimwaga alipokuwa akizungumzia
kuhusiana na ubovu wa barabara hizo katika Wilaya hiyo.
Kimwaga alifafanua kuwa Wilaya ina jumla ya barabara ambazo
zipo kwenye mtandao wa Wakala huyo ni 216 na kwamba kati ya hizo barabara za
lami ni Kilometa 1.371, changarawe Kilometa 81.388, udongo Kilometa 1178.44
ambapo kati ya hizo zinazopitika kipindi chote cha mwaka ni barabara zenye Kilometa
400 tu.
Alisema kuwa katika msimu wa mwaka huu 2018/2019 TARURA Wilayani
humo wamejipanga kuhakikisha kwamba wanajenga madaraja, vivuko na makalvati ili
barabara hizo ziweze kupitika kabla ya kuendelea na ujenzi husika.
Pia alieleza kuwa mkakati mkubwa walionao sasa ni kutoka
katika ujenzi wa barabara za changarawe hadi kufikia kiwango cha lami na kwamba
hivi sasa wanakamilisha, ujenzi wa barabara ya Milonde hadi Kalulu yenye urefu
wa Kilometa 26 ambayo ilikuwa katika hali mbaya kipindi hiki cha masika ambapo
wananchi wamekuwa wakishindwa kutumia barabara hiyo na hakuna magari yaliyoweza
kufika kwenye maeneo hayo kutoa huduma ya usafiri.
“Kutokana na hali hii wananchi wanalazimika kutembea kwa
miguu au Pikipiki kwa gharama kubwa katoka sehemu moja kwenda nyingine barabara
hii ni muhimu sana kiuchumi kwa Wilaya ya Tunduru kwani ndiyo eneo lenye
uzalishaji mkubwa wa mazao mchanganyiko,
“Kazi iliyofanyika katika barabara ile ni kupunguza milima, kuweka
changarawe katika maeneo yaliyokuwa na utelezi vilevile tutaendelea kufanya
hivyo hata katika barabara za udongo ambazo zinakwenda katika maeneo yenye
uzalishaji mkubwa”, alisema Kimwaga.
Aliongeza kuwa barabara nyingine ambayo wanatarajia kuanza
ujenzi wake ni ile inayoanzia Kalulu hadi kwenye hifadhi ya Selou yenye urefu
wa Kilometa 40 ambayo nayo ni muhimu kwa kukuza uchumi wa Wilaya na kurahisisha
kuleta Watalii waweze kupita vizuri bila vikwazo au usumbufu wowote ule.
No comments:
Post a Comment