Na Mwandishi wetu,
Songea.
WANANCHI zaidi ya 600 wa kutoka katika vijiji mbalimbali
Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, wanatarajia kupata ajira katika mgodi wa makaa ya
mawe uliopo kwenye kijiji cha Maniamba kata Muhukuru Wilayani humo, ambao
unatarajiwa kuanza shughuli zake za uchimbaji wakati wowote kuanzia sasa.
Kampuni ya Kambas Group of Companies ambayo imeanza shughuli
ya utafiti wa madini hayo tokea mwaka 2017 na kubaini uwepo wa makaa kiasi cha
takribani tani milioni 20 ambapo baada ya kukamilisha utafiti huo yataweza kuchimbwa
kwa muda wa miaka 40 kwa uzalishaji wastani wa tani 500,000 kwa mwaka.
Yahaya Yusufu ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni hiyo alisema
hayo juzi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge Ajira na Walemavu
Jenista Mhagama wakati Waziri huyo alipokuwa ametembelea kujionea shughuli
zinazoendelea kufanyika katika mgodi huo ambapo Mhagama alikuwa katika ziara
yake ya kuhimiza, kuangalia na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za
kimaendeleo katika jimbo lake la Peramiho Wilayani hapa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mwenyekiti huyo alieleza kuwa Kampuni
ya Kambas mara baada ya kukamilisha utafiti na kuanza rasmi uchimbaji wa madini
hayo, inatarajia kuongeza wigo wa ajira hasa kwa Wakazi wanaozunguka katika
eneo ulipokuwa mradi na kwamba shughuli zitakazokuwa zinafanywa hapo
zitahusisha makundi ya watu wenye elimu inayohitaji sifa mbalimbali na wale wasiokuwa
na elimu.
Alisema kuwa Kampuni wakati wote itajitahidi kufanya kazi kwa
kushirikiana karibu na Serikali katika kuboresha maendeleo na kuimarisha
mahusiano katika jamii ikiwemo kusaidia kutoa huduma mbalimbali ikiwemo ujenzi
wa Ofisi ya kata, zahanati ya kijiji na baadhi ya madarasa ya shule ya msingi.
Pamoja na mambo mengine alizungumzia pia changamoto wanazokabiliana
nazo ikiwemo ubovu wa barabara kutoka Muhukuru barabarani hadi eneo ulipokuwa mradi
sawa na urefu wa Kilometa 6 kwani barabara hiyo sio nzuri inahitaji matengenezo
ili kuwezesha magari makubwa kupita.
Yusufu ameiomba Serikali isaidie kuimarisha barabara hiyo ili iweze
kupitika wakati wote na kuweza kurahisisha katika kusafirisha makaa ya mawe
yatakayokuwa yanachimbwa huko.
Mara watakapokuwa wanaanza shughuli za uchimbaji Halmashauri
ya Wilaya ya Songea itaweza kupata asilimia 3 ya mapato yatokanayo na shughuli
za uchimbaji huo kwa kila mwezi na ukusanyaji wa ushuru shilingi 1,000 kwa kila
tani ya makaa yatakayopatikana na kusafirishwa.
No comments:
Post a Comment