Baadhi ya Wanufaika wa TASAF mtaa wa Mtendewawa Manispaa ya Songea wakipokea fedha za Ruzuku zinazotolewa na mfuko huo kwa kaya maskini. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea Mkoani
Ruvuma, imeanza kutoa malipo kwa njia ya Mtandao kwa kaya maskini zipatazo 4,880
zilizopo katika mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF).
Mratibu wa Mfuko huo katika Manispaa
hiyo, Christopher Ngonyani alisema kuwa kati ya kaya hizo kaya 2,638 sawa na
asilimia 54 zinapokea fedha kwa njia ya mitandao ya simu na kaya 2,242 sawa na
asilimia 46 bado zinapokea fedha kwa njia ya fedha taslimu.
Alisema kuwa katika kipindi cha mwezi
Januari hadi Februari mwaka huu kaya 2,242 zimelipwa fedha taslimu zaidi ya
shilingi milioni 88 na kaya 2,638 zimelipwa kwa mtandao zaidi ya shilingi milioni
88 na kufanya jumla ya zaidi ya shilingi milioni 176 zimetolewa kwa wanufaika
wote katika kipindi hicho.
“Lengo ni kwamba ifikapo mwezi Juni mwaka
huu tunatarajia kufikia asilimia 90 ya wanufaika wote wa TASAF kulipwa fedha
kwa njia ya mtandao”, alisema Ngonyani.
Vilevile alisema kuwa lengo la Serikali
kuanzisha malipo kwa njia ya mtandao ni kuweza kurahisisha usafirishaji wa
fedha kwa usalama wa hali ya juu, kufikisha fedha kwa wakati kwa walengwa na
kupunguza gharama za uendeshaji wa mradi.
Ngonyani alifafanua kuwa lengo la
kufanya hivyo ni kuhakikisha wanufaika wote wanajisajili kulipwa kwa njia ya
mitandao ili kuepukana na changamoto nyingi ambazo zinaweza kujitokeza katika
malipo ya fedha taslimu ikiwemo kutolewa kwa malipo hewa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Songea, Palolet Mgema akizungumza na wanufaika hao katika mtaa wa Mitendewawa
Kata ya Mshangano Manispaa ya Songea Mkoani hapa, alisema Serikali iliamua
kuanzisha mfumo huo wa ruzuku kwa kaya maskini ili kuweza kumkomboa mwananchi mwenye
maisha duni.
Mgema alisema hivi sasa asilimia
kubwa ya wanufaika wameweza kujiingiza katika shughuli za uzalishaji mali
ikiwemo ufugaji na biashara ndogo ndogo.
Kadhalika Mkuu huyo wa Wilaya anazitaja
changamoto ambazo zimejitokeza kwa baadhi ya wanufaika wachache Wilayani humo, kuwa
ni pamoja na kutumia fedha wanazozipata kwa masuala ya mambo ya anasa ikiwemo
kunywa pombe, hali ambayo inarudisha nyuma azma ya Serikali ya kuzikomboa kaya hizo.
Utafiti uliofanywa katika mitaa
mbalimbali ya Manispaa ya Songea ambayo wanufaika wamelipwa kwa njia ya
mtandao, tumebaini kuwa mfumo huo umepata mafanikio makubwa baada ya wanufaika
wengi kupata fedha zao mapema na kwa haraka, hali ambayo imesababisha wanufaika
ambao bado hawajajisajili kwenye mfumo huo kuhamasika kwenda kujisajili.
Manispaa hiyo ni moja kati ya
Halmashauri 16 nchini zilizochaguliwa kufanya majaribio ya malipo kwa njia ya mtandao
wa simu, kwa wanufaika wa Mfuko huo wa maendeleo ya jamii ili kuepukana na
changamoto zilizokuwa zimejitokeza kwa kutumia mfumo wa kulipwa fedha za taslimu.
Kwa ujumla mpango huu wa kunusuru
kaya maskini unaendeshwa katika Halmashauri 163 nchini na kwamba umeweza
kunufaisha kaya maskini zikiwemo zile ambazo awali zilikuwa zinapata mlo mmoja
kwa siku ambapo hivi sasa zinaweza kupata milo mitatu kwa siku.
No comments:
Post a Comment