Na Mwandishi wetu,
ULINZI na Usalama umeimarishwa katika eneo alilozikwa mwanafunzi
wa chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline katika kijiji cha
Olele Wilayani Rombo.
Mwandishi wetu ambaye aliwasili katika eneo la tukio leo Ijumaa wakati mazishi ya mwanafunzi huyo yanafanyika, alibaini uwapo wa askari
wengi wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na askari kanzu.
Mbali na askari kanzu, walionekana maofisa usalama wa Taifa
na Polisi waliovalia kiraia, wakiwa wameegesha magari kimkakati, mita kati ya
100 hadi 150 kutoka nyumbani kwa wazazi wa marehemu.
Vilevile Ofisa mnadhimu wa Polisi namba moja wa Mkoa
Kilimanjaro, Koka Moita, ambaye alizoeleka kuwa katika sare, alionekana
akitembea kwa miguu mitaani akiwa amevalia kiraia.
Moita alipoulizwa kuhusu usalama, alikiri kuna ulinzi wa
kutosha lakini alisema anayeweza kuzungumzia hilo ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Hamis Issah.
Pia walikuwa mgambo ambao wameshika doria maeneo ya maegesho
ya magari ya wageni mbalimbali na eneo la Kanisa ilipofanyika ibada.
Askari wa usalama barabarani nao walionekana barabara kuu ya
Olele-Useri, wakisimamia usalama wa watembea kwa miguu na watumiaji wengine wa
barabara, jirani na shughuli za mazishi zilipofanyika.
Waziri wa Elimu
Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako aliahidi kumsomesha
mdogo wake Akwilina Akwilini, ambaye ni Angela Akwilini na hivi sasa anasoma
kidato cha tatu.
Akizungumza baada ya mazishi ya
Akwilina aliyeuawa kwa kupigwa risasi Februari 16, mwaka huu eneo la Mkwajuni
jijini Dar es Salaam, Profesa Ndalichako alisema atamsomesha Angela hadi Chuo
Kikuu.
Pamoja na mambo mengine, Akwilina Akwiline katika safari yake
ya mwisho hapa duniani, amezikwa katika makaburi ya kijijini kwao Olele Wilayani
Rombo.
No comments:
Post a Comment