Na Mwandishi wetu,
SERIKALI imesema kuwa Mwalimu wa shule ya Sekondari
kufundisha shule ya Msingi, maana yake sio kwamba kushushwa cheo na kwamba
jambo hilo sio la ajabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa kitengo cha mawasiliano
Ofisi ya Rais (Utumishi), Florence Lawrence imesema kuwa Serikali kuwapangia
baadhi ya walimu wa Sekondari kufundisha shule za Msingi ni moja ya hatua za
kuongeza ufanisi na kuleta mgawanyo sawa wa walimu katika shule hizo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Dokta Laurean Ndumbaro amenukuliwa katika taarifa hiyo ambayo ilitolewa leo
Februari 20 mwaka huu.
Alisema hatua hiyo haimaanishi kuwa walimu wanaotoka kwenye
shule ya Sekondari kwenda kufundisha Msingi wameshushwa cheo.
Dokta Ndumbaro alitoa ufafanuzi huo katika kikao kazi na Watumishi
wa Halmashauri ya Mji wa Makambako.
Alisema lengo la Serikali ni kuondoa upungufu wa walimu
katika shule za Msingi na kuimarisha utoaji wa elimu.
Katibu Mkuu huyo ameainisha kuwa sifa za kufundisha na
kiwango cha elimu zinaendana na mabadiliko yanayotokea duniani, hivyo mwalimu
mwenye elimu ya kiwango cha Shahada ya kwanza kufundisha shule ya Msingi
isionekane ni jambo la ajabu.
Pamoja na mambo mengine, Dokta Ndumbaro amewaambia Watumishi
wa umma kuwa, maendeleo katika sekta yoyote, ikiwamo ya elimu yanakuja na
mabadiliko hivyo wayapokee na kufanya kazi ili kuweza kufikia lengo.
No comments:
Post a Comment