Na Muhidin Amri,
Songea.
BAADHI ya shule za Msingi na Sekondari
zilizopo katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, zimekabidhiwa aina mbalimbali
ya miche ya miti kutoka kwa Rotaly Club tawi la Songea iliyopo mjini hapa ili
waweze kuipanda kwenye maeneo yao, ikiwa ni lengo pia la kurudisha uoto wa
asili na utunzaji wa mazingira katika shule hizo.
Miche hiyo ambayo imekabidhiwa ni ile
ambayo imeoteshwa katika vitalu kwa shule hizo ambayo ni miti 4,000 kati ya 15,000
wanayotarajia kuiotesha katika msimu wa mwaka huu.
Rais wa Club hiyo tawi la Songea,
Albert Kessy alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ambapo
alidai kuwa miti ambayo wanaizalisha kwenye vitalu hivyo ni ile aina ya matunda,
mbao, kivuli na mapambo.
Alifafanua kuwa mpango walionao ni
kuendelea kugawa miche mingi zaidi kwa shule hizo ili waweze kuipanda hasa
katika maeneo ambayo yanauharibifu mkubwa wa mazingira.
Kessy alibainisha kuwa katika kipindi
cha mwezi Novemba mwaka jana walifanya matembezi ya hiari, ambayo yalilenga
kukusanya fedha kwa ajili ya kununua mbegu za miti hiyo ambazo zimesaidia kuendelea
na zoezi la kuzalisha miche na kuigawa katika shule hizo.
Pia alieleza kuwa mbali na hilo Rotaly
Club licha ya kuwa na Wadau hao wa mazingira katika Manispaa hiyo, imefanikiwa
pia kukarabati miundombinu ya shule mbalimbali za msingi na sekondari mjini
humo ikiwemo ujenzi wa choo kipya kwa matumizi ya wanafunzi katika shule ya
sekondari Bombambili.
“Tumefanikiwa kukarabati miundombinu
ya shule ikiwemo ukarabati wa matundu ya vyoo 16 na kujenga choo kipya katika
shule ya sekondari Bombambali, ambapo kabla ya hapo wanafunzi wa kike na
wavulana walikuwa wakijisaidia katika choo kimoja na kwamba mradi huu wa miti tunakusudia
kufika maeneo ya shule zote katika Manispaa hii”, alisema Kessy.
Changmoto kubwa wanayokabiliana nayo
hivi sasa ni uhaba wa fedha kwani kiasi cha fedha walichoanzishia mradi huo
hivi sasa ni fedha ambazo wamechangishana kutoka kwa wanachama wa Club.
Mbali na mradi wa miti, Kessy aliongeza
kuwa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani na chuo
cha VETA Songea walifanikiwa kukusanya waendesha bodaboda na kuwapa mafunzo ya
udereva na uendeshaji wa matumizi sahihi ya barabara, ambapo vijana 150 waliweza
kupata leseni na vyeti baada ya kupata mafunzo hayo.
Kwa upande wake naye Mratibu wa shirika
lisilokuwa la Serikali, Roots and shoots ambalo linajihusisha na masuala ya uelimishaji katika utunzaji
wa mazingira kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya
Songea, Mwalimu Oddo Ngatunga alisema kuwa msaada huo wa miti utawasaidia
kuweza kurudisha uhifadhi wa mazingira kwa shule hizo kwa faida ya kizazi cha
sasa na kijacho.
No comments:
Post a Comment