Na Mwandishi wetu,
KASSIM Majaliwa ambaye ni Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema kuwa Serikali imebaini kwamba maeneo
ya bahari kuu, bandari, vituo vya mabasi pamoja na viwanja vya ndege hapa
nchini ndiyo yanatumika zaidi kupitisha dawa za kulevya.
Wafanyabiashara, wasambazaji na
watumiaji wa dawa hizo alisema kuwa wamekuwa wakikamatwa lengo ikiwa ni kuhakikisha
kwamba biashara hiyo inakomeshwa na kumalizika kabisa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo
na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema kuwa Waziri huyo ametoa kauli hiyo wakati
akikabidhi gari kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za
Kulevya (DCEA), Rogers Sianga katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Alieleza kuwa mbali na kukamata meli pia
Serikali imewakamata wasambazaji pamoja na kundi kubwa la wafanyabiashara
wanaojihusisha na biashara hiyo sambamba na watumiaji.
Majaliwa alifafanua kuwa lengo la
kufanya hivyo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na kizazi chenye uwezo wa
kuzalisha mali.
Aliongeza kuwa Serikali imepiga hatua
kubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya na kwamba hivi karibuni imeweza kukamata
meli nyingi, moja ikiwa inatokea pwani ya Msumbiji na ilikamatiwa maeneo ya
Mtwara ikiwa na dawa nyingi za kulevya.
“Ni wakati wa Serikali sasa kuendelea
kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na leo hii
tunawakabidhi gari hili jipya kabisa ili liweze kuendelea na utekelezaji wa majukumu
yake ipasavyo”, alisema.
Kadhalika amewataka Watanzania
waachane na biashara ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kazi ya kusambaza,
kuzalisha, kutumia na wale watakaokamatwa wakijihusisha nazo watachukuliwa
hatua kali za kisheria.
Alisema hivi sasa Serikali inajenga
maabara ambayo itatumiwa na Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya
kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa dawa wanazozikamata.
Wananchi wanatakiwa kushirikiana na
Serikali katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa mara
wanapowabaini wafanyabiashara, watumiaji na wasambazaji wa dawa hizo.
Pia wahakikishe wanawalinda vijana
ili wasijihusishe na dawa za kulevya.
Kwa upande wake, Sianga ameishukuru
Serikali kwa kuipatia mamlaka hiyo gari ambapo alitumia fursa hiyo kuwataka
wananchi waachane na biashara hiyo huku akiwasihi kupambana kuhakikisha dawa za
kulevya haziingizwi nchini.
Hata hivyo mbali na kudhibiti
biashara hiyo alisema pia wanatoa elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa za
kulevya, ikiwemo vitendo viovu vinavyofanywa na watumiaji ili wachukie na
waache kutumia dawa hizo.
No comments:
Post a Comment