Na Mwandishi wetu,
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Charles Kichere amemsimamisha kazi Meneja wa Mamlaka hiyo Mkoa
wa Mara, Nicodemus Mwakilembe kutokana na uzembe wa kutosimamia ipasavyo matumizi
ya Mashine za Kielektroniki (EFDs) ambazo hutumika kutolea risiti kwa wafanyabiashara
wa Mkoani humo.
Hatua hiyo ya kusimamishwa kazi imetokana
na ziara ya kushtukiza iliyofanywa ya kukagua matumizi ya Mashine hizo aliyoifanya
Kamshina huyo kwenye baadhi ya maduka ya biashara Wilayani Bunda Mkoa wa Mara.
Akizungumza mara baada ya ziara yake,
Kichere alisema kuwa Meneja huyo ameonyesha uzembe wa hali ya juu kwani kuna
wafanyabishara wengi Mkoani kwake, ambao walikwisha lipa fedha kwa ajili ya
kupata mashine za EFDs lakini mpaka sasa hawajapatiwa mashine hizo.
“Katika ziara yangu nimegundua kwamba
wapo wafanyabiashara ambao walikwisha lipia mashine hizi miaka kadhaa iliyopita
lakini mpaka sasa, bado hawajapatiwa mashine zao na wamekuwa wakitumia mwanya
huo kama kinga ya kutochukuliwa adhabu na TRA wakati Meneja wa Mkoa yupo na
hachukui hatua yoyote, huu ni uzembe uliopitiliza na kamwe siwezi kuuvumilia”, alisisitiza
Kichere.
Kutokana na uzembe huo, Kamishna huyo
amewaagiza Mameneja wote wa TRA hapa nchini pamoja na majukumu mengine kuhakikisha
wanasimamia kikamilifu matumizi ya mashine za EFDs katika mikoa yao na kuongeza
kuwa hatasita kumwajibisha Meneja yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu
yake ipasavyo.
No comments:
Post a Comment