Na Kassian Nyandindi,
Tunduru.
UJENZI wa daraja kubwa la kisasa
katika mto Nanyungu litakalounganisha kijiji cha Fundimbanga na vijiji vingine
Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma, limeanza kujengwa ili kuweza kuondoa kero mbalimbali
zilizodumu kwa muda mrefu ambazo walikuwa wakipata wananchi wa Wilaya hiyo.
Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini
(TARURA) Wilayani hapa, ndiye ambaye ameanza kazi ya usimamizi wa ujenzi huo na
kwamba kukamilika kwa daraja hilo, imeelezwa kwamba kutarahisisha mawasiliano
kati ya pande hizo mbili kwa maeneo ya vijiji hivyo.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Tunduru,
Mhandisi Cyprian Kimwaga alisema kuwa kujengwa na kukamilika kwa daraja hilo
kutamaliza pia kero ya wananchi kuvuka kwa kutumia daraja la miti lililopo katika
mto huo.
Kimwaga alifafanua kuwa kuvuka katika
daraja hilo la miti kumekuwa kukihatarisha usalama wa maisha ya wananchi hasa
kipindi cha masika wakihofia kusombwa na maji au kuliwa na mamba kutokana na
mto huo kuwa na mamba wengi.
Alisema kuwa Serikali imetoa zaidi ya
shilingi bilioni 115.804 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita
45 ambapo ni kati ya madaraja makubwa, Wilayani humo na linatajwa kuwa
ndiyo mradi mkubwa kutekelezwa na TARURA katika Mkoa wa Ruvuma tangu Serikali
ilipoanzisha Wakala huyo.
Daraja hilo linajengwa na Kampuni ya
kitanzania inayofahamika kwa jina la IBIHI chini ya usimamizi wa TARURA ambapo
kampuni hiyo imeonesha uwezo mkubwa ambao daraja hilo linatarajiwa
kukamilika ifikapo Mei 28 mwaka huu na sasa ujenzi wa nguzo umekamilika kabla
ya kuendelea na kazi nyingine.
Vilevile kukamilika ujenzi wake wananchi
wanaozalisha mazao ya biashara na chakula ikiwemo korosho, mahindi na zao la
mpunga litawezesha pia waweze kufanya shughuli zao za biashara na kuharakisha kukua
kwa uchumi wao na Wilaya kwa ujumla.
Kadhalika kwa upande wao wakizungumzia
ujenzi wake baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Tunduru, Vumilia Lipapapa na Bahati
Mtweve wameishukuru Serikali kwa uamuzi iliochukua wa kulijenga daraja katika
mto Nanyungu wakieleza kuwa litasaidia wafanye shughuli zao za maendeleo kwa
ufasaha ikiwemo kati yao na watu wengine wa maeneo mengine.
Vumilia Mtweve alisema kuwa litaweza
kumaliza tatizo kwa akina mama wajawazito na wagonjwa wengine hasa pale
wanapougua na kubebwa kwa kutumia matenga, pale wanapokwenda hospitali kwa
ajili ya kupata matibabu kwani hapana usafiri mwingine unaoweza kupita katika
daraja hilo la miti.
“Kwa kweli tunaishukuru Serikali yetu
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa uamuzi wake wa kujenga daraja hili, tunaamini
litakapokamilika tutaondokana na kero hii ya wagonjwa wetu kubebwa katika
matenga kwa kutumia baiskeli hasa kwa akina mama wajawazito wanapofikia hatua
ya kujifungua”, walisema.
No comments:
Post a Comment