Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma, Yustina Chagaka. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma, imeokoa zaidi ya shilingi milioni 25 ambazo
zilitaka kutumika kama mishahara hewa na idara mbalimbali za Serikali Mkoani
humo.
Yustina Chagaka ambaye ni Mkuu wa taasisi
hiyo Mkoani hapa alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa
habari mjini hapa.
Chagaka alikuwa akitoa taarifa ya Mkoa
wa Ruvuma katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, ambapo alisema kuwa kati ya fedha
zilizookolewa zaidi ya shilingi milioni 22 ni za sekta ya afya na milioni 3 ni kutoka
sekta ya elimu.
Alifafanua kuwa katika kipindi hicho
TAKUKURU ilipokea taarifa 221 kutoka kwa wananchi.
Alizitaja idara ambazo zinaongoza
kulalamikiwa kuwa ni Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambapo kuna
taarifa za malalamiko 57, ardhi 41, mahakama 25, polisi 13, vyama vya siasa 11
na elimu 12.
Kadhalika aliongeza kuwa katika
kipindi hicho wameweza kukagua pia miradi nane ya maendeleo inayohusu ujenzi wa
miundombinu ya afya, elimu na maji yenye thamani zaidi ya shilingi bilioni 8.5.
Alisema kuwa katika baadhi ya miradi
hiyo ilikuwa na viashiria vya ubadhirifu na mapungufu mengi, hivyo uchunguzi wa
matumizi ya fedha za miradi hiyo umeanzishwa ili kuweza kubaini ni kiasi gani
cha fedha hakikutumika ipasavyo katika miradi husika.
No comments:
Post a Comment