Na Muhidin Amri,
Songea.
JENISTA Mhagama ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera Bunge, Ajira na Watu wenye ulemavu ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya
Songea Mkoani Ruvuma kuhakikisha wanatumia vizuri asilimia tatu ya mapato
yatokanayo na shughuli zitakazoanza za uchimbaji wa makaa ya mawe katika kijiji
cha Maniamba kata ya Muhukuru Wilayani humo.
Aidha amesema wanapaswa kuweka mazingira bora yatakayoweza
kuwavutia wawekezaji, ambapo hatua hiyo itaweza kutoa fursa kwa wawekezaji
wengi kuweza kuwekeza ili mradi huo wa makaa ya mawe uweze kusonga mbele.
Hivi sasa Kampuni ya Kambas Group of Companies imeweza kuanza
kuwekeza katika kijiji hicho ili kuweza kufanya kazi zake katika mazingira
rafiki ya uchimbaji wa makaa hayo, hivyo Halmashauri hiyo ameitaka pia kuweka
mazingira mazuri ambayo hawataweza kukimbiwa na wawekezaji hao.
Waziri Mhagama ametoa agizo hilo jana, huku akiwaonya pia
viongozi wa kijiji cha Maniamba akiwataka kuwa waaminifu wa fedha kwa
kujiepusha na tabia ya wizi na kuwataka kutumia mapato hayo, kwa ajili ya
kusomesha vijana wao wa kijiji hicho ili wapate ujuzi utakaowawezesha kuwa na sifa
nzuri ya kufanya kazi kwenye mgodi huo.
Hayo yalisemwa na Waziri huyo alipokuwa akizungumza na wakazi
wa kijiji hicho, Wakuu wa idara ya Halmashauri ya Wilaya hiyo wakati alipotembea
katika eneo hilo ili kuweza kujionea kazi ya utafiti wa makaa ya mawe inayoendelea
kufanyika katika kijiji cha Maniamba na Kampuni ya Kambas Group of Companies.
Alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha
kwamba nchi ya Tanzania inafikia uchumi wa kati kwa kuanzisha viwanda vingi
ambavyo vitasaidia kukua kwa uchumi wake na Watanzania wengi waweze kupata
ajira katika viwanda hivyo.
Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Peramiho alieleza
kuwa hivi sasa Watanzania wapatao milioni 25 ndiyo wenye uwezo wa kufanya kazi na
kwamba kati yao asilimia 56 ni vijana ambao wapo katika ajira isiyokuwa rasmi
na ile ajira rasmi.
Alifafanua kuwa kutokana na kuwepo kwa tatizo hilo Serikali
imehamasisha na itaendelea kuhamasisha shughuli za uwekezaji ili watu wake
waweze kupata ajira hasa kwa wale wazawa na hatimaye kukuza uchumi wa nchi yetu.
Vilevile ameipongeza Kampuni hiyo kwa hatua iliyochukua ya
uamuzi wake wa kuwekeza katika utafutaji na uchimbaji wa makaa ya mawe katika
jimbo la Peramiho.
Hata hivyo amewataka wamiliki wa Kampuni ya Kambas Group of
Companies kufuata sheria zilizowekwa ikiwemo utoaji wa mapato ya asilimia 0.3
kwa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, ushuru wa kijiji cha Maniamba na
kuzingatia maslahi kwa wafanyakazi wake ili kuepuka migogoro inayoweza
kusababisha kazi ya uchimbaji wa madini hayo kukwama.
No comments:
Post a Comment