Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MLIPUKO wa Ugonjwa wa Kipindupindu
umetokea katika kijiji cha Ulima, kata ya Ukata Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma
na kuathiri watu 28 Wakazi wa kijiji hicho, ambao wote wamenusurika kupoteza
maisha baada ya timu ya wataalamu kuwahi kutoa tiba katika eneo la tukio.
Taarifa zilizomfikia Mwandishi wetu
kutoka kwa Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya hiyo, Hussein Sepoko alisema
kuwa tukio la ugonjwa huo liliambatana na watu hao kuugua vimelea vilivyoambatana
na dalili za kuhara na kutapika, ambapo kati ya hao wagonjwa 19 walikuwa wanawake
na 9 wanaume.
Sepoko alisema kuwa chanzo kikubwa
cha ugonjwa huo kilitokana na kuchafuliwa kwa vyanzo vya maji na uhaba wa vyoo
katika kijiji hicho, ambapo wananchi wengi wamekuwa wakitumia mto uliopo
kijijini humo ambao ndiyo mpaka unaotenganisha Wilaya ya Mbinga na Nyasa.
Alisema kuwa maji ya mto huo wananchi
hao wamekuwa wakiyatumia kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kunywa, bila hata kuyachemsha
licha ya watu kupewa elimu juu ya umuhimu wa kuzingatia usalama wa afya zao.
Pia alifafanua kuwa kumekuwa na uhaba
wa vyoo katika kaya nyingi ambazo wamezitembelea na kujionea hali hiyo, ikiwemo
hata shule ya msingi Ulima iliyopo katika kata hiyo imekuwa na uhaba wa matundu
ya vyoo hali ambayo inawafanya wanafunzi wengi kujisaidia porini.
Vilevile tatizo la unawaji wa mikono baada
ya kujisaidia nalo imekuwa ni changamoto kubwa huku wengi wao walikiri kutonawa
wakitoka kujisaidia na wengine hutumia maji, yaliyopo kwenye chanzo cha mto kujisafisha
huku maji hayo yakitumika na wengine ndiyo maana imetokea kwa urahisi kusambaa
kwa ugonjwa.
Mganga huyo alieleza kuwa uongozi wa
Wilaya ya Mbinga ulipopata taarifa juu ya hilo timu ya wataalamu wa afya ipo
huko mpaka sasa ikiendelea kuhudumia wananchi kwa kuwapa maelekezo ya aina
mbalimbali namna ya kujikinga na kuepukana nao.
Kadhalika wagonjwa hao waliobainika
walipelekwa katika zahanati ya misheni Lundomato iliyopo Wilayani humo na
kupatiwa matibabu kwa haraka ambapo wataalamu hao wameenda huko na vifaa tiba
na kuweza kuendelea kuokoa maisha ya waathirika hao.
Hata hivyo mpaka sasa hakuna vifo
vilivyotokea na kwamba sampuli zilizochukuliwa kwa wagonjwa hao kwa njia ya
haja kubwa na kupelekwa katika maabara ya Mkoa wa Ruvuma kwa utambuzi zaidi
bado zinathibitisha kuwa wagonjwa hao wanaugua Kipindupindu.
No comments:
Post a Comment