Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
UJENZI wa Kituo cha afya Kalembo katika
kata ya Kihungu Halmashauri Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, imeelezwa kuwa
unaendelea vizuri na umefikia katika hatua ya mwisho kukamilisha baadhi ya
vipengele vya ujenzi wa majengo husika.
Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilayani humo, Beda Hyera mara baada ya kutembelea
Kituo hicho na kujionea uhalisia wa kazi zinazofanyika.
Hyera alisema kuwa ujenzi huo ambao
unafanyika na usimamizi wake ameridhishwa nao kwamba unaendelea vizuri.
Amewapongeza Mwenyekiti Kipwele
Ndunguru na Mkurugenzi wake wa Halmashauri ya Mji huo, Robert Kadaso Mageni
kwamba waendeleze jitihada hizo za kukamilisha kazi ya ujenzi huo ili wananchi
wa kata ya Kihungu waweze kupata huduma ya matibabu kwa urahisi.
Vilevile alieleza kuwa Serikali ya
CCM inayoongozwa na Dokta John Pombe Magufuli, haitaki kuona wananchi wake
wanapata shida ndiyo maana imetengeneza Ilani ya chama hicho ambayo inatetea
maslahi ya mwananchi hivyo hata viongozi waliowekwa madarakani, wanapaswa
kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa na Serikali hiyo ili kuweza kuondoa
kero zinazoikabili jamii.
“Ndugu zangu Serikali hii malengo
yake ni kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata haki sawa katika nyanja ya
elimu, afya miundombinu ya barabara na mambo mengine muhimu yote ambayo
Mtanzania anapaswa kuyapata”, alisema Hyera.
Hata hivyo Serikali kwa ujumla,
imetoa fedha zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hicho
cha afya Kalembo kilichopo katika kata ya Kihungu Halmashauri ya Mji wa Mbinga
kwa ajili ya kufanya kazi ya kukamilisha ujenzi wa jengo la upasuaji, maabara,
wodi ya akina mama na watoto, nyumba ya mganga pamoja na jengo la kuhifadhia
maiti.
No comments:
Post a Comment