Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbinga, wakiwa katika picha ya pamoja Wanafunzi na Walimu wa shule hiyo. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANAFUNZI wanaosoma katika shule ya Sekondari
Mkinga Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuongeza juhudi kwenye masomo
yao ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao na kutimiza malengo waliyonayo
katika maisha yao.
Aidha imeelezwa kuwa wametakiwa kuacha
kujiingiza kwenye matendo maovu ambayo yanaweza kuwaharibia ndoto ya maendeleo ya
masomo yao na maisha kwa ujumla.
Ushauri huo ulitolewa kwa nyakati
tofauti na Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilayani
humo, Sostenes Nchimbi na Katibu wa umoja huo Wilayani hapa, Daima Nyoni wakati
walipokuwa wakizungumza juzi na wanafunzi wa shule hiyo.
Mazungumzo hayo yalienda sambamba
mara baada ya watoto hao kushirikiana na viongozi hao wa CCM ambao walikuwa
wameambatana na Wajumbe wengine wa Wilaya wa jumuiya hiyo kwenda kupanda miti
katika eneo la shule hiyo kwa lengo la kutunza mazingira.
Zoezi hilo lilienda sambamba na
maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama hicho na kutimiza miaka 41 sherehe ambazo
ziliambatana na shughuli za kijamii ikiwemo upandaji miti uliofanywa na Jumuiya
hiyo.
Nchimbi alisema kuwa Wilaya ya Mbinga
ni moja kati ya Wilaya chache hapa nchini zenye fursa nyingi ambazo zinatoa
nafasi kwa vijana kujiendeleza zaidi kielimu, kwani hata historia inaonesha
kuna idadi kubwa ya viongozi waliosoma na kushika nafasi za juu hapa nchini
lakini tatizo baadhi ya vijana wenyewe hawataki kujituma na kuzingatia masomo
yao.
“Nawasihi sana vijana ongezeni juhudi
katika masomo yenu tumieni muda huu mlionao kujiandaa na masomo ya juu zaidi
badala ya kuridhika na hapa mlipofikia kwani kumbukeni elimu haina mwisho”,
alisema Nchimbi.
Naye Katibu wa Jumuiya hiyo ya Wazazi
Wilaya ya Mbinga, Daima Nyoni aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau
wengine wa maendeleo imeanza kufungua milango ya uwekezaji, hivyo inahitaji
wasomi wengi watakaofanya kazi katika sekta mbalimbali na wale ambao wenye elimu
ya juu.
Pamoja na mambo mengine, aliwataka wajitambue
na kuelewa kuwa vijana ndiyo nguzo kuu ya uchumi katika nchi hivyo ni vyema wanapaswa
kusoma kwa bidii ili taifa katika vizazi vijavyo liweze kupata wasomi wengi
zaidi na wazalendo, jambo ambalo litasaidia kuwa na wataalam wengi na kuokoa
kiasi kikubwa cha fedha wanacholipwa wataalam hao ambao ni wa fani mbalimbali kutoka
nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment