Monday, February 26, 2018

TAKUKURU RUVUMA YAOKOA MABILIONI YA FEDHA MISHAHARA HEWA

Yustina Chagaka, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma.


Na Muhidin Amri,     
Songea.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ruvuma, katika kipindi cha  kuanzia mwezi Julai hadi Desemba mwaka 2017 iliweza kuokoa kiasi cha shilingi Bilioni 25,174,375.00 ambapo katika sekta ya elimu fedha zilizookolewa ni shilingi 3,000,000.00 na sekta ya afya ziliokolewa shilingi 22,1743375.00 ikiwa ni mishahara hewa.

Pia taasisi hiyo katika kipindi hicho ilipokea taarifa 221 kutoka kwa wananchi kupitia vyanzo mbalimbali na kwamba idara zilizobainika kuongoza kulalamikiwa ni TAMISEMI malalamiko (57) Ardhi (41) Mahakama (25) Kilimo (15) Polisi (13) Vyama vya siasa (11) na Elimu malalamiko (12).

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani hapa, Yustina Chagaka aliwaeleza Waandishi wa habari hivi karibuni kuwa idadi ya kesi zilizoenda Mahakamani ni 11 zilizopo katika Mahakama ya Hakimu mkazi Songea, katika kesi nne zilihusu TAMISEMI, Idara ya afya, TASAF na Sekta binafsi.


Kwa mujibu Kamanda huyo alieleza kuwa katika Wilaya ya Mbinga kuna kesi nne ambazo zote zinahusu TAMISEMI, Wilaya ya Tunduru kesi mbili zilizohusu Idara ya ardhi na Mahakama huku Wilaya ya Namtumbo kulikuwa na kesi moja inayohusu nayo Idara ya ardhi.

Chagaka alisema katika mwaka 2017 kesi zilizofunguliwa Mahakamani zilikuwa tano na kuzitaja ni pamoja na Uhujumu uchumi yenye namba 16/2017 ambayo ipo katika Mahakama ya Hakimu mkazi Songea, kesi ya jinai namba 110/2017 iliyoko Mahakama ya Wilaya Tunduru na kesi ya jinai namba 11/2017 Wilayani Namtumbo.

Hata hivyo alitaja kesi nyingine za jinai namba 86/2017 na namba 87/2017 katika Mahakama ya Wilaya ya Mbinga ambapo kesi zilizokamilika na kutolewa hukumu katika kipindi hicho ni tano ambapo kati ya hizo mbili walipatikana na hatia.

No comments: