Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SERIKALI Wilayani Mbinga Mkoa wa
Ruvuma, imetoa onyo kali kwa Wafanyabiashara wanaojishughulisha na uuzaji wa Mbolea
ya kukuzia mazao shambani Wilayani humo, kuzingatia bei elekezi iliyotolewa na
Serikali na sio vinginevyo.
Mhandisi Gilbert Simya. |
Aidha imeelezwa kuwa msako mkali
unaendelea kufanyika ili kuweza kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za
kisheria, watu wanaodaiwa kuficha mbolea ya ruzuku ambayo ni ya kukuzia mazao aina
ya UREA na baadaye huuza bei ya juu kwa wakulima tofauti na maelekezo
yaliyotolewa na Serikali.
Katibu tawala wa Wilaya hiyo,
Mhandisi Gilbert Simya alisema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi
wa habari Ofisini kwake juu ya tatizo la uhaba wa mbolea za kukuzia mazao
shambani lililopo Wilayani hapa.
Simya alifafanua kuwa mahitaji ya
mbolea aina hiyo katika Wilaya ya Mbinga hivi sasa yamekuwa makubwa ambapo
maafisa kilimo wanafanya tathimini, ili kujua ni kiasi gani halisi kinatakiwa
kutokana na uzalishaji uliopo hivyo kila mfanyabiashara anapaswa kuuza kwa
kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali.
Alisema kuwa kuanzia Februari Mosi
mwaka huu bei mpya ya mbolea aina ya UREA ambayo imetolewa na Mamlaka ya
Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ni kwamba mfuko wenye kilo 50 kwa Halmashauri
ya Mji wa Mbinga unapaswa kuuzwa kwa shilingi 56,585, kilo 25 unauzwa kwa
shilingi 30,293, kilo 10 unauzwa shilingi 12,117 na kilo 5 inabidi uuzwe kwa
shilingi 6,459.
Vilevile akifafanua kwa upande wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mfuko wa kilo 50 nao unauzwa kwa shilingi
57,149, kilo 25 shilingi 30,575, kilo 10 shilingi 12,230 na kwamba kilo 5
unauzwa kwa shilingi 6,515.
“Bei ya jumla ambayo Wakala wa Mkoa
mzima kwa mfuko wa UREA wa kilo 50 popote pale anapaswa kuuza kwa shilingi
52,824 na kila mkulima nasisitiza anapouziwa mbolea apewe risiti ya Serikali (EFD)”,
alisema Simya.
Hata hivyo kwa upande wao baadhi ya
wakulima wa Wilaya hiyo kwa nyakati tofauti wamelalamikia kuuziwa mbolea aina
ya UREA kwa bei ya juu na baadhi ya wafanyabiashara Wilayani humo, jambo ambalo
Serikali ya Wilaya imethibitisha kupokea malalamiko hayo na kueleza kuwa
yanafanyiwa kazi na wahusika watakapobainika watachukuliwa hatua kali za
kisheria.
No comments:
Post a Comment