Thursday, September 19, 2013

BALOZI WA PAPA AWATAKA WAKRISTO KUTOJIINGIZA KATIKA MACHAFUKO

Kanisa la Mtakatifu Killian lililopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Senyi Ngaga, naye hakuwa mbali katika kushiriki maadhimisho ya misa takatifu ya kuwapaka watoto mafuta ya Kipaimara.

 Balozi wa Papa nchini Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla, akiendelea na maadhimisho ya misa katika Kanisa la Mtakatifu Killian lililopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma. (Picha zote na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAUMINI wa dhehebu la Kikristo, wameshauriwa kutojiingiza katika matukio yenye kuhatarisha na kuvuruga amani ya nchi yetu, na badala yake waungane kwa pamoja kupinga matukio maovu yanayoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Wito huo ulitolewa na Balozi wa Papa hapa nchini, Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla alipokuwa akizungumza na Waumini wa Kanisa la Mtakatifu Killian Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, katika maadhimisho ya sherehe za misa takatifu ya kuwapaka mafuta ya daraja la kipaimara, watoto  waliokuwa wakipatiwa daraja hilo.

Balozi huyo alisema itakuwa si busara kwa waumini wa dhehebu hilo kujihusisha na matendo yasiyompendeza Mungu, hivyo ni vyema wajiepushe ili taifa liendelee kuwa na amani.

“Ndugu zangu matukio ya ajabu yamekuwa yakiendelea kutokea, mapadri wamekuwa wakifanyiwa vibaya kule Zanzibar, makanisa yetu yanachomwa moto, kwa kweli matukio kama haya hayavumiliki na   haya mpendezi Mungu”, alisema Padilla.

Aidha wakati wa maadhimisho ya misa hiyo ulinzi mkali ulikuwa umetanda kuzunguka kanisa hilo ndani na nje, ambao ulijumuisha maofisa usalama wa taifa na askari polisi huku waumini wa kiislamu ambao walionekana kutaka kuingia katika eneo la kanisa hilo, walizuiwa kuingia.

Vyanzo mbalimbali vya habari ambavyo vilizungumza na mwandishi wa habari hizi vilisema kuwa kuzuiwa huko, kulitokana na kuhusishwa kwa matukio mabaya yanayoendelea kufanyika hapa nchini hususani kwa lile la mlipuko wa bomu huko Arusha, ambalo lilitokea hivi karibuni.  

Kadhalika wengine walikuwa wakisema wachungaji na mapadre kule Zanzibar nao wamekuwa wakiumizwa na kupata mateso na makundi ya waislamu ambayo hayana nia njema na wakristo, na kwamba wamechoshwa na vitendo hivyo na kuitaka serikali ichukue hatua madhubuti za kisheria kwa wale wanaohusika.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa jimbo la Mbinga John Ndimbo naye alisema hivi sasa katika kipindi hiki kigumu, amewataka wakristo nchini  kuwa na umoja na kutolipiza kisasi kwa matukio mabaya wanayofanyiwa kama vile kushambuliwa kwa mapadre na kuchomewa moto makanisa, badala yake wawe watulivu na kuendelea kumwomba Mungu na yeye ndiye mwenye kujua nani anastahili kupewa adhabu kwa yule mwenye makosa.

No comments: