Tuesday, September 24, 2013

MAKABIDHIANO YA MWENGE WA UHURU LIGANGA: KIONGOZI WA MBIO HIZO KITAIFA, AWATAKA WANAFUNZI KUZINGATIA MASOMO

Msafara wa Mwenge wa Uhuru ukiwasili katika kijiji cha Liganga wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, tayari kwa makabidhiano ukitokea wilayani Mbinga.

 Mwenge wa Uhuru ukipelekwa katika eneo maalum, kwa ajili ya maandalizi ya kukabidhiwa wilaya ya Songea.

Wanafunzi wa shule ya Msingi Liganga, wakiwa wameshika mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali wa mbio za Mwenge wa Uhuru.


Burudani ngoma za asili, nazo hazikuwa nyuma katika kijiji cha Liganga.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Juma Alli Simai, akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Liganga ambapo aliwasisitiza watoto hao, kuzingatia masomo wanapokuwa shuleni.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga(aliyeshika Maiki) akizungumza jambo wakati akiwa katika hatua ya kumkabidhi kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Juma Alli Simai (aliyekuwa upande wa kushoto) kwenda wilaya ya Songea, kwa ajili ya kuendelea na mbio hizo mkoani Ruvuma. Upande wa kushoto ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilayani Mbinga Christantus Mbunda.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Juma Alli Simai, akiveshwa Skavu baada ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga kumkabidhi kwa wananchi wa wilaya ya Songea.


Mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti, akikumbatiana na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kuveshwa Skafu, ikiwa ni ishara ya kukaribishwa kwa kiongozi huyo wa kitaifa wilaya ya Songea.

Senyi Ngaga Mkuu wa wilaya ya Mbinga, akitoa heshima(maelezo) kabla ya kuukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa wilaya ya Songea.

Mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti, akiwa ameushika Mwenge wa Uhuru mara baada ya kukamilika kwa makabidhiano kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga ambaye ameonyesha mgongo(amevaa trakisuti nyeusi)

Tayari Mwenge wa Uhuru ukiwa katika eneo maalum, kwa ajili ya kuendelea na mbio zake wilayani Songea mkoa wa Ruvuma. (Picha zote na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

HATIMAYE Mwenge wa Uhuru uliokuwa ukiendelea kufanya kazi zake wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, sasa umemaliza kazi husika salama na kukabidhiwa leo kwa uongozi wa wilaya ya Songea.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika kijiji cha Liganga wilayani humo, ambapo Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga alifanya kazi ya kumkabidhi kiongozi mwenzake ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti.

Wakati makabidhiano hayo yakifanyika kijijini hapo shamra shamra na burudani za hapa na pale, zilikuwa zikiendelea kutolewa ambapo vikundi vya ngoma za asili navyo havikuwa nyuma, katika makabidhiano hayo.

Kiongozi wa mbio hizo za Mwenge wa Uhuru kitaifa,  Juma Alli Simai naye hakuwa mbali katika kutoa ujumbe wa mbio hizo, ikiwemo lile la kuwataka Watanzania kuendelea kuheshimu, kulinda amani na utulivu huu tulionao.

Pamoja na mambo mengine Simai pia alisisitiza kwa wazazi kuhakikisha watoto wao wanawapeleka shule, na sio kuwaacha majumbani.

Alisema jukumu la mzazi kumpeleka mtoto shule ni jambo la lazima na sio hiari, hivyo linapaswa kuzingatiwa wakati wote kwa kuhakikisha pia mtoto husika anapata mahitaji yake muhimu, awapo shuleni.

Mwenge wa Uhuru wilayani Mbinga, umeweza kufanya kazi kwenye miradi 11 yenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 1,061,881,200.

No comments: