Tuesday, September 3, 2013

HABARI ZA MAHAKAMANI WILAYANI MBINGA

Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.

WATU watatu wakazi wa kijiji cha Litumbandyosi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wamefikishwa katika mahakama ya wilaya kwa tuhuma za mauaji.

Imedaiwa na mwendesha mashitaka wa polisi ispekta Nassib Swed mbele ya hakimu mkazi katika mahakama ya wilaya hiyo Joakim Mwakyolo kuwa washitakiwa Triphon Ngatunga(47),Saimon Haule(35) na Pasko Mgimba(37) wote wakazi wa kijiji cha Litumbandyosi wanatuhumiwa kumuua Lucas Soko(66) wa kijiji hicho.

Aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa washitakiwa hao wanatuhumiwa kutenda kosa la kumuua Soko februari 25 mwaka huu majira ya saa 4.00 usiku nyumbani kwake huku wakimtuhumu ni mshirikina ambapo walitumia silaha aina ya panga na shoka kufanya uhalifu huo.

Aidha watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji na kwamba wamerudishwa mahabusu hadi septemba 2 mwaka huu.
                          
  
Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.

MAHAKAMA ya  wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imemhukumu mkazi mmoja wa kijiji cha Muhukuru wilaya ya Songea adhabu ya kifungo cha miaka 3 kwenda jela kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali.

Akisoma hukumu hiyo hakimu mfawidhi katika mahakama hiyo Geofrey Mhini alisema kuwa mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kuwa mshitakiwa Makarius Ndunguru(42) mkazi wa kijiji cha Muhukuru, bila halali alikutwa akiwa na manyoya ya ndege wa aina mbalimbali pamoja na nyama ya Ngorombwe vyote vikiwa na thamani ya shilingi 400,000 ambavyo alitoka navyo katika hifadhi ya Liparamba.

Mhini alisema kuwa mahakama imemtia hatia Ndunguru na kumhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 3 kwenda gerezani ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Awali mwendesha mashitaka wa polisi Inspekta Nassibu Swed alidai mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa alikutwa na nyara hizo za serikali na askari wanyama pori Januari 18 mwaka huu majira ya saa 5.15 asubuhi katika kijiji cha Muhukuru wilayani Songea.

Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.

MFANYABIASHARA mmoja wa Mbinga mjini mkoani Ruvuma amehukumiwa na mahakama ya wilaya hiyo adhabu ya kifungo cha miaka 3 kwenda jela kwa kosa la kukutwa na mali za wizi yenye thamani ya shilingi 144,000.

Akisoma hukumu hiyo hakimu mkazi katika mahakama ya wilaya hiyo Joackim Mwakyolo alisema kuwa mahakama imezingatia ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kuwa, mshitakiwa Maneno Mgaya(27) mfanyabiashara wa Mbinga mjini alikutwa na ndoo 4 za rangi zinazodaiwa kuwa ni za wizi dukani kwake.

Mwakyolo alisema kuwa mahakama imemtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 3 kwenda jela, ili liwe fundisho kwa wafanyabiashara wengine wenye tabia kama hiyo.

Awali mwendesha mashitaka wa polisi Inspekta Nassib Swed alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Mgaya alikutwa na ndoo hizo za wizi dukani mwake, majira ya saa 6.30 mchana Aprili 15 mwaka huu.

No comments: