Thursday, September 19, 2013

BARAZA LA TAIFA LAISIMAMISHA KAMPUNI KUENDELEA NA KAZI YA UCHIMBAJI WA MAKAA YA MAWE

Rais Jakaya Kikwete.





















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BARAZA la taifa la hifadhi na usimamizi  wa mazingira limeisimamisha kampuni ya Tancoal Energy, inayochimba makaa ya mawe katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma  kufanya kazi ya kupakia na kusafirisha makaa ya  mawe katika kituo cha Amani Makolo na Bandari ya Ndumbi,  kwa muda wa siku saba kutokana na kukiuka maagizo ya baraza hilo.

Kampuni hiyo imesimamishwa baada ya timu ya baraza hilo la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira, kukagua na kutoa maelekezo mara kadhaa ya namna ya kupunguza athari za vumbi kwa wananchi,  uchafuzi wa vyanzo vya maji, kujenga vyoo na mifereji ya kupitisha taka vimiminika na kampuni hiyo kutotekeleza maagizo hayo.

Dokta Madoshi Makene alisema maeneo yaliyofungiwa kufanya kazi ni eneo la Amani Makolo Mbinga  na bandari ya  Ndumbi, katika wilaya ya Nyasa mkoani humo, ambako kunazalishwa kiasi kikubwa cha vumbi kutokana na shughuli ya upakiaji na usafirishaji wa makaa hayo ya mawe na kushindwa kuzuia vumbi lisisambae katika makazi ya watu.

Katika eneo la Ndumbi timu hiyo haijakuta vyoo vilivyojengwa kwa ajili ya wafanyakazi, na hakuna mifereji kwa ajili ya kupitisha maji machafu yanayotoka kwenye eneo hilo ili yasiende kuchafua maji ya mito na ya ziwa Nyasa ambayo hutumika na wananchi katika shughuli za maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wao wakazi wa kijiji cha Amani makolo wilaya ya Mbinga wanaomba serikali iwasaidie ili waweze kulipwa na  kuhama, sasa wanashindwa kuishi katika makazi yao kutokana na mazingira ya nyumba zao kuzungukwa na vumbi na kusababisha watoto kuugua mafua na kikohozi.

Meneja wa mazingira na usalama wa kampuni ya Tancoal Felix Fida, amekiri kuwa ni kweli wanafahamu matatizo ya vumbi katika vituo hivyo, lakini kuna juhudi zinazofanyika ili kupunguza ama kuondoa kabisa kero hiyo.

No comments: