Tuesday, September 3, 2013

WATU WENYE MAKUNDI MAALUM WATAKA KATIBA IJAYO IZINGATIE HAKI ZAO ZA MSINGI

Washiriki wa kuchangia maoni ya rasimu ya katiba mpya wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika picha ya pamoja nje ya ukumbi wa Mbiku uliopo mjini hapa.

Stevene Matteso akichangia hoja wakati wa kutoa maoni ya marekebisho ya rasimu ya katiba mpya katika ukumbi wa Mbiku uliopo mjini hapa.


Walemavu nao hawakuwa mbali katika kusikiliza na kutoa maoni yao.                             (Picha zote na Kassian Nyandindi)





Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

WASHIRIKI katika uchangiaji wa maoni ya rasimu ya katiba mpya wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametaka katiba ijayo ihakikishe kwamba inaweka misingi ya kutambua makundi maalum, ikiwemo upatikanaji wa haki zao bila kubaguliwa.

Pamoja na serikali kutoa matamko mengi juu ya haki za Walemavu  lakini utekelezaji wake umekuwa hautekelezwi ipasavyo, jambo ambalo linasababisha kundi hilo likose haki zake za msingi na kujikuta kutengwa na jamii.

Rai hiyo ilitolewa na washiriki hao ambao ni watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali wilayani Mbinga, wakati walipokuwa katika mafunzo ya siku tatu ya katiba, ambayo yalifadhiliwa na shirika la The foundation for civil society, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mbiku uliopo mjini hapa.

Walisema kuwa haki za binadamu hususani kwa walemavu zilizopo katika rasimu ya katiba mpya, haitambui ipasavyo watu hao kwa makundi na mahitaji yao hivyo ni vyema yakafanyika mabadiliko ya dhati ikiwemo suala la uhitaji wa vifaa vya kufundishia darasani hususani kwa watu wasioona na viziwi.


Mmoja kati ya washiriki hao aliyejitambulisha kwa jina la Efigenia Kinunda alisema, hata Rais anapopewa nafasi ya kuteua watu kuingia katika nafasi ya ubunge, katiba ijayo ihakikishe watu kutoka kwenye makundi maalum, ni lazima nao wapewe kipaumbele katika kuwateua kwenye nafasi hiyo na kwamba kila mkoa pawepo na mwakilishi wa nafasi ya ubunge ili kuweza kusaidia kutambua kwa urahisi matatizo ya walemavu katika mkoa husika.

“Kwa ujumla rasimu hii ukiingalia kwa ujumla wake juu haki za makundi maalum, inashindwa hata kuyatambua ipasavyo, tufike mahali tukubali inatukandamiza kwa sehemu fulani”, alisema Kinunda.

Naye Steven Matteso alieleza kwamba katiba ijayo ijenge mazingira ya kuwawezesha walemavu wawe wanapata matibabu bure, ruzuku zitolewe kwenye vyama vya walemavu, kusamehewa kodi katika biashara wanazozifanya na kuwepo miundombinu rafiki mashuleni na hata katika ofisi zinazohudumia jamii.

Hata hivyo aliongeza kuwa katika katiba ijayo, itamke kuwepo nafasi ya walemavu katika kuchangia uchumi wa nchi na haki sawa za binadamu ikiwemo ajira katika sekta binafsi na serikalini.


No comments: