Monday, September 30, 2013

MAPENDEKEZO YA WILAYA TATU YASABABISHA MVUTANO KATI YA MADIWANI NA WATAALAMU


Na Steven Augustino,
Tunduru.

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, limepitisha mapendekezo ya uundwaji wa mji mdogo, mgawanyo wa eneo la utawala na kuridhia kuundwa kwa mkoa mpya utakaoziunganisha wilaya ya hiyo na Namtumbo.

Mapendekezo hayo yalipitishwa katika kikao maalum kilichoketi kwenye ukumbi wa Klasta mjini humo, na kwamba Madiwani hao walifikia makubaliano hayo  baada ya majadiliano ya muda mrefu ambapo awali, baadhi yao walipendekeza uwepo wa mgawanyiko wa Wilaya mbili wakilenga kusogeza huduma na kuharakisha maendeleo kwa wananchi.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo ambayo yalionekana kutoendana na mapendekezo ya wataalamu ambao walienda na mapendekezo ya mgawanyo wa wilaya mbili, Wilaya ya kwanza walitaka iundwe na tarafa za Matemanga na Nampungu wilaya ya pili iundwe na tarafa za Nakapanya, Mlingoti na Namasakata na wilaya ya tatu  nayo ikitajwa kuundwa na tarafa za Nalasi na Lukumbule.

Akifafanua maelezo ya mgawanyo huo Diwani wa kata ya Ligunga Kazembe Said alisema kuwa, kutakuwa na faida mbalimbali kwani katika kupatikana kwa wilaya hizo tatu kutapanua huduma na kuiwezesha serikali kufikisha huduma kwa wananchi wake kwa haraka, na kuyafikia malengo husika iliyojipangia kuwafikia wananchi wake ifikapo 2020 na kwamba  endapo watapendekeza mgawanyo wa  wilaya mbili watakuwa wameshiriki kulitenga eneo kubwa ambalo bado litakuwa  halifikiwi wa uirahisi kiutawala.

Uchache wa vigezo vilivyodaiwa kutakiwa kuangaliwa upya wakati wa mgawanyo huo, Diwani wa kata ya Masonya Fadhili Msahamu alisema kuwa wilaya ya Namtumbo wakati inatangazwa kuwa Boma, wilaya yao ilikuwa na tarafa 3, kata 13 na  sasa inaomba kupewa wilaya ya pili ikiwa na wanazo kata na kwamba wilaya ya Tunduru kwa sasa  inazo kata 35, Tarafa 7 na Vijiji 148 na  eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 18,778 ambalo pia linaweza kugawanywa na kuongeza maeneo ya utawala.

Upande wa uundaji wa mkoa mpya wa SELOU unaotarajiwa kuunganisha wilaya za Tunduru na Namtumbo, Madiwani hao walipitisha bila mabadiliko yoyote huku mgawanyo wa mapendekezo ya kuundwa kwa mamlaka ya mji mdogo wa Tunduru, madiwani wa kata za Kidodoma Seif Miwani, Said Mkandu na Mbunge wa jimbo la Tunduru Kusini Alhaji Mtutura walitoa mapendekezo ya kuongeza maeneo mapya ili kuwa na eneo la kutosha.

Awali akitoa taarifa za mapendekezo hayo afisa mipango wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Kenneth Haulle aliwaeleza madiwani hao kuwa vigezo walivyopewa kutoka ofisi ya Waziri mkuu ni pamoja na kuzingatia maeneo mbali mbali  ikiwemo kigezo cha kwanza ni matumizi ya takwimu mbali mbali ikiwemo zinazozungumzia idadi ya watu, vijiji, kata na tarafa zilizopo wilayani humo.

Haulle aliendelea kufafanua kuwa wilaya ya Tunduru sasa inayo majimbo mawili ya uchaguzi ya Tunduru Kusini na Tunduru Kaskazini yenye wakazi 298,274 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, inazo tarafa 7, kata 35, vijiji 148 na vitongoji 1,015 hali ambayo iliwasukuma wataalamu hao kupeleka mapendekezo hayo ya mgawanyo wa wilaya mbili za  kiutawala, wakiwa wanafuata vigezo na maelekezo ya kitaifa yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa mgawanyo huo.

No comments: