Monday, September 23, 2013

WATANZANIA WATAKIWA KUWABEZA NA KUEPUKA VIONGOZI WANAOTUMIA MAJUKWAA KUVURUGA AMANI YA NCHI YETU

Kikundi cha Ngoma aina ya Mganda kikitumbuiza mara baada ya Mwenge wa Uhuru, kuwasili katika kijiji cha Mpapa wilayani Mbinga.

Mwenge wa uhuru mara baada ya kuwasili ukitokea wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, ukipelekwa katika eneo maalum tayari kwa maandalizi ya makabidhiano kwa wilaya ya Mbinga mkoani humo.

Mkuu wa wilaya ya Nyasa(Aliyeshika maiki) Ernest Kahindi, akizungumza, kutambulisha/kukabidhi wageni waliokuwa wakikimbiza Mwenge kwa ngazi ya kitaifa, mkoa na wilaya hiyo.

Senyi Ngaga Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, akisalimiana na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Juma Ally Simai wakati wa utambulisho na makabidhiano ya viongozi wa mbio za mwenge kitaifa mara baada ya mwenge huo ukitokea wilayani Nyasa.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Juma Ally Simai akisalimiana na Mwenyekirti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga, Christantus Mbunda.

Mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi, akijiandaa kuukabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga akiupokea Mwenge wa uhuru kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi. (Picha zote na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WATANZANIA wametakiwa kuwabeza, kuepukana na Viongozi wa dini au siasa  ambao hutumia majukwaa kuhutubia wananchi, kwa nia ya kuchochea maneno yenye kujenga kuvuruga amani iliyopo hapa nchini, badala yake wawe na mshikamano, upendo na utulivu ili kuimarisha amani hiyo isiweze kuvurugika.

Rai hiyo iliotolewa na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Juma Ally Simai, alipokuwa akitoa ujumbe wa Mwenge huo wakati akizungumza na baadhi ya wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, katika kijiji cha Mpapa kata ya Mpapa wilayani humo.

Simai alitoa kauli hiyo mara baada ya kumaliza kufanya makabidhiano ya Mwenge huo kijijini hapo, ambapo awali msafara wa mwenge ulikuwa ukitokea katika wilaya mpya ya Nyasa mkoani humo.

 “Ndugu zangu amani ndio msingi mkuu wa maendeleo, kwa umoja wetu tulionao tuendelee kuudumisha tuachane na mambo ya itikadi za kisiasa au dini, sisi sote ni wa moja”

“Tuepukane na viongozi wa dini au siasa wenye nia mbaya ya kuvuruga umoja huu, taifa letu halikujengwa kwa misingi ya kiubaguzi”, alisisitiza Simai.

Alieleza kuwa Tanzania ilipata Uhuru mapema, kutokana na kuondoa ubaguzi miongozi mwa jamii.

“Amani ikitoweka ndani ya nchi madhara yake ni makubwa, hebu angalia nchi za wenzetu ambao tunapakana nao, amani imevurugika hivyo kuirudisha tena ni kazi kubwa sana”, alisema.

Pamoja na mambo mengine Mwenge wa Uhuru wilayani Mbinga umeweza kufanya kazi kwenye miradi 11 yenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 1,061,881,200.

Katika miradi hiyo kazi iliyofanyika ni kuwekewa mawe ya msingi, kufunguliwa, kuzinduliwa na kukaguliwa ambapo kati ya miradi hiyo nguvu za Wananchi ni shilingi milioni 592,950,000 mchango wa Halmashauri 209,938,800 Serikali kuu 126,912,000 Wahisani 107,830,400 na nguvu za watu binafsi 24,250,000.

Hilo ni ongezeko la shilingi milioni 439,412,126 sawa na asilimia 70.6 kwa miradi iliyotekelezwa wilayani Mbinga kwa mwaka jana (2012).

Hata hivyo Mwenge huo wa Uhuru leo Wananchi wa wilaya hiyo wanakesha nao katika uwanja wa Taifa uliopo mjini hapa, na kuendelea na mbio zake kesho, kuelekea wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

No comments: