Monday, September 30, 2013

KAMPUNI YA BAM YAPONGEZWA KWA KAZI YA USAMBAZAJI WA PEMBEJEO ZA KILIMO MKOANI RUVUMA

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Juma Simai, akifungua jengo(Ghala) la kampuni ya BAM ambalo hutumika kuhifadhia pembejeo za kilimo.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Juma Simai akiwa ndani ya ghala la kuhifadhia pembejeo, akisisitiza jambo mara baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya kampuni ya BAM juu ya usambazaji wa pembejeo za kilimo mkoani Ruvuma.

Uongozi wa kampuni ya BAM ukiwa katika picha ya pamoja na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Juma Simai.(aliyeshika Mwenge)

Hizi ni moja kati ya pembejeo za kilimo ambazo husambazwa na kampuni ya BAM kwa wakulima mkoani Ruvuma.

Mkurugenzi mkuu wa BAM, Bernad Malila. (Picha zote na Kassian Nyandindi)



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KIONGOZI wa mbio Mwenge  wa Uhuru Juma Simai ameipongeza kampuni ya BAM (LTD) inayojishughulisha na usambazaji wa pembejeo za kilimo katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma, kutokana na kuwa na mipango thabiti inayolenga kupanua shughuli za kilimo na kuongeza uzalishaji wa chakula hapa nchini hatua ambayo inaweza kuinua uchumi wa wakulima na nchi kwa jumla.

Simai alitoa pongezi hizo hivi karibuni mjini  Mbinga, wakati akifungua jengo la ghala la kuhifadhi pembejeo za kilimo lenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 600 za mbolea aina mbalimbali na kuiagiza serikali ya wilaya ya Mbinga, kuunga mkono juhudi kubwa iliyoonyeshwa na kampuni hiyo kwani inalenga kuwakomboa na kuwasaidia wakulima.

Alisema iwapo viongozi watashirikiana na BAM katika mkakati wa kitaifa wa kukifanya kilimo kiwe ni kati ya maeneo makubwa ya kiuchumi, kuna uwezekano mkubwa wa wilaya hiyo kupiga hatua za haraka za maendeleo kufuatia kuwepo kwa eneo kubwa la ardhi inayofaa kwa ajili ya shughuli za kilimo ikilinganishwa na maeneo mengine hapa nchini.

Alieleza kuwa kitendo cha kampuni hiyo kupunguza bei za pembejeo ni faraja kubwa siyo kwa wakulima pekee, bali hata kwa serikali kwani nayo imepania kukifanya kilimo kiwe ni eneo lingine la kibiashara zaidi kwa kuajiri maafisa ugani wengi na kupunguza ruzuku na kodi katika vifaa vya kilimo, hivyo ni vyema kila mmoja wakiwemo viongozi kushiriki na kuiunga mkono kampuni hiyo ambayo  imeleta unafuu mkubwa kwa wakulima wa wilaya ya Mbinga, mkoa na taifa kwa ujumla.

“Viongozi wa Mbinga, wapeni ushirikiano hawa watu  wanaokuja  kuleta maendeleo hapa wilayani kwenu, narudia kulisema hili kwa sababu viongozi katika maeneo mengi tumekuwa watu wa kujisahau sana, hakuna maendeleo ya kweli yanayokuja bila ya kushirikiana na wadau”, alisema Simai.

Awali akitoa taarifa ya kampuni hiyo Meneja mkuu wa kampuni ya BAM Suzo Komba alieleza kuwa lengo  kubwa la mradi huo ni kuleta huduma za usambazaji wa pembejeo kwa wakulima wakubwa na wadogo katika maeneo ya karibu zaidi mkoani Ruvuma,  ili kuwarahisishia upatikanaji wa pembejeo na mahitaji mengine ya wakulima badala ya kutembea umbali mrefu kufuata pembejeo za kilimo.

Komba alitaja walengwa wakuu katika mpango huo ni wakulima wa mazao ya mahindi, kahawa, mpunga na mazao mengine ya chakula na biashara ambayo kwa kiasi kikubwa yanazalishwa katika wilaya ya Mbinga na kuwa na kituo kikubwa  cha usambazaji na kitakacholinda ubora wa mbolea zitakazouzwa kupitia kampuni  hiyo.


Alisema hadi sasa kampuni hiyo imeweza kujenga ghala kubwa la kuhifadhia mbolea ambalo limegharimu zaidi ya shilingi milioni 235.7 fedha ambazo zimetokana na mfuko wa kampuni hiyo kutokana na faida kidogo wanazopata baada ya kuuza pembejeo za kilimo, wanazozisambaza na kwamba aliishukuru serikali chini ya wizara ya kilimo na chakula kwa ushirikiano mkubwa wanaouonyesha kwa wasambazaji wa pembejeo za kilimo.



No comments: