Saturday, March 26, 2016

WAKULIMA WA KAHAWA WAIOMBA SERIKALI KUONGEZA KASI YA USAMBAZAJI WA MADAWA

Ofisa ugani wa Taasisi ya kituo cha utafiti zao la kahawa TaCRI, Daniel Mwakalinga ambaye yupo kati kati amevaa shati lenye rangi nyeupe akitoa elimu ya kilimo bora cha zao la kahawa kwa wakulima wa kijiji cha Mkinga kata ya Mapera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma ambapo wakulima hao aliwataka kutumia miche ya kahawa aina ya vikonyo ambayo haishambuliwi na wadudu waharibifu.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKULIMA wanaolima zao la kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali ya awamu ya tano hapa nchini, kuongeza kasi ya usambazaji wa madawa yanayodhibiti zao hilo lisishambuliwe na wadudu waharibifu, ili waweze kuzalisha kahawa kwa wingi na yenye ubora.

Aidha walieleza kuwa ugonjwa wa Chulebuni (CBD) ni ugonjwa ambao huenea kwa kasi, ambapo mti wa kahawa ulioshambuliwa na ugonjwa huo hupoteza asilimia 90 ya mavuno endapo mkulima hatazingatia namna ya kuzuia ugonjwa huo.

Rai hiyo ilitolewa na wakulima hao kwenye maadhimisho ya siku ya mkulima wa kahawa yaliyofanyika kijiji cha Mkinga kata ya Mapera wilayani hapa, ambapo Taasisi ya utafiti wa zao la kahawa TaCRI wilayani humo imejiwekea utaratibu wake kila mwaka wa maadhimisho hayo, ikilenga kuelimisha wakulima juu ya kilimo bora cha zao la kahawa.

SOUWASA YALIA NA WAHARIBIFU WA MAZINGIRA YASEMA ATAKAYEKAMATWA KUFIKISHWA MAHAKAMANI



Na Julius Konala,
Songea.

MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (SOUWASA) katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imepiga marufuku kuendesha shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji, ikiwa ni lengo la kukabiliana na tatizo la ukame linaloweza kujitokeza kipindi cha kiangazi.

Aidha imeelezwa kuwa kwa mwananchi atakayebainika kukiuka agizo hilo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

Mhandisi uzalishaji wa mamlaka hiyo, Jones Salema alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa hiyo, Mhandisi Francis Kapongo.

Friday, March 25, 2016

UWT RUVUMA YAMPONGEZA MAGUFULI UTENDAJI WAKE WA KAZI




Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani Ruvuma, imempongeza Rais John Magufuli kwa kazi anazozifanya za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitendo ambacho kimeelezwa kuwa kufanya hivyo ni kujenga imani kwa wananchi na serikali yao.

Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa UWT mkoani humo, Kuruthumu Mhagama alipokuwa kwenye kikao cha baraza maalumu la jumuiya hiyo kilichofanyika mjini hapa, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kuruthumu alisema serikali ya awamu ya tano, chini ya kauli mbiu ya Hapa kazi tu imedhamiria kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi wake na kwamba kinachotakiwa sasa, kila mwananchi ahakikishe anatekeleza majukumu yake ipasavyo kwenye eneo lake ili dhamira ya serikali kuwaletea maendeleo iweze kutimia.

Thursday, March 24, 2016

KILOSA JUU BADO WAMLALAMIKIA MKUU WA WILAYA YA NYASA

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.


MKUTANO  ulioitishwa na Mkuu wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Margaret Malenga kwa lengo la kuzungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kilosa juu wilayani humo, umeingia dosari baada ya wananchi hao kukataa kutoa maeneo yao ili waweze kumpisha mwekezaji anayetaka kutumia sehemu ya eneo la kijiji hicho kujenga kituo cha kuuzia mafuta.

Aidha katika mkutano huo wananchi hao walifikia hatua ya kugomea kutoa maeneo yao, kutokana na Mkuu huyo wa wilaya kukataa kuwaeleza wazi pale walipotaka kujua ni mwekezaji gani atakayejenga kisima hicho cha mafuta.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Vilevile kufuatia kuwepo kwa usiri huo uliogubikwa juu ya nani atajenga kituo hicho, wananchi hao walipotakiwa kuandika majina yao ya mahudhurio na kuweka sahihi zao walikataa kutekeleza hilo, wakidai kuwa hawaoni uhalali wa wao kuhudhuria mkutano huo kutokana na mambo mengi kufichwa na kutowekwa wazi juu ya uwekezaji huo unaotakiwa kufanyika. 

Tukio hilo la aina yake lilitokea Marchi 22 mwaka huu majira ya mchana, kwenye ukumbi mdogo wa ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo ambako mkutano huo ulifanyika kwa muda wa masaa matano, na kushindwa kufikia muafaka wa jambo hilo.

BMT YAWATAKA WAANDISHI WA HABARI KUFICHUA MATATIZO YALIYOPO KWENYE KLABU ZA MICHEZO


Na  Kassian Nyandindi,

Songea.

MJUMBE wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) hapa nchini, Zainabu Mbiro (Pichani) amewaomba waandishi wa habari wasaidie kufichua migogoro iliyopo katika klabu za michezo ili mamlaka husika, ziweze kuchukua hatua na kuweza kuondokana na matatizo yaliyopo ambayo yanarudisha nyuma maendeleo katika sekta ya michezo.

Mbiro alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa mkoani Ruvuma, ambapo pia aliipongeza timu ya Majimaji mkoani humo kwa kuendelea vizuri katika michezo mbalimbali ya soka.

Tuesday, March 22, 2016

AKUTWA BARABARANI AMEFARIKI DUNIA AKIWA AMEPONDEKA KICHWA NA MBAVU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Mabatini, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma Omary Rashid (64) amekutwa akiwa amefariki dunia, katika tukio la kugongwa na gari au pikipiki.

Zubery Mwombeji.
Mashuhuda wa tukio hilo, walisema waliuona mwili wa marehemu huyo ukiwa umelala barabarani eneo la mabatini jambo ambalo liliwafanya wahisi kwamba, huenda marehemu aligongwa na vyombo hivyo vya moto.

Mtoto wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Abdala Issa, alisema kuwa huenda chanzo cha kifo chake kilisababishwa na tabia yake ya ulevi wa kupindukia na kwamba, baada ya kuzidiwa na pombe alilala barabarani na hivyo kugongwa bila kujitambua.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na wanaendelea kufanya uchunguzi, ili kuweza kujua chanzo cha kifo chake.

MWANAFUNZI ALAZWA HOSPITALI BAADA YA KUUMWA NA NYOKA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MWANAFUNZI anayesoma darasa la saba shule ya msingi Msamaria, iliyopo kijiji cha Mtangashari wilayanai Tunduru mkoa wa Ruvuma, Ramadhan Swedi (14) amelazwa katika Hospitali ya wilaya hiyo, baada ya kuumwa na nyoka.

Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa, mwanafunzi huyo alikumbwa na mkasa huo wakati akiwa anacheza mpira na wenzake katika maeneo ya shule hiyo.

 Mzazi wa mwanafunzi huyo, Usale Swedi alisema baada ya tukio hilo kutokea walimu walimpatia huduma ya kwanza ya kumfunga kamba na kumnywesha mafuta ya taa, na baadaye kumpeleka nyumbani kwake.

AKAMATWA NA POLISI KWA TUHUMA ZA KUKUTWA NA BUNDUKI KINYUME NA TARATIBU



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI wa kijiji  cha Namiungo  wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Abdul Pushapusha (56) anashikiliwa na Polisi, kwa tuhuma za kukutwa na bunduki kinyume na taratibu za umiliki wa silaha za moto.

Aidha katika tukio hilo, mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa na risasi moja ya bunduki aina ya Rifle na maganda matano ya risasi za bunduki aina ya Shortgun kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa mtuhumiwa alikamatwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Monday, March 21, 2016

WAFUNGWA TUNDURU WAFARIKI DUNIA BAADA YA KUPIGWA RADI GEREZANI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAFUNGWA wawili ambao walikuwa wakitumikia kifungo katika gereza la kilimo na mifugo Majimaji, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma wamefariki dunia papo hapo baada ya kupigwa na radi.

Sambamba na vifo hivyo, pia watatu walijeruhiwa baada ya kupigwa na radi hiyo na kukimbizwa hospitali ya wilaya hiyo, kwa ajili ya matibabu zaidi ambako wamelazwa na hali zao bado ni mbaya.

Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea majira ya jioni Marchi 18 mwaka huu, wakati wafungwa hao wakiwa wamekwisha fungiwa gerezani.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa ni mipango ya Mungu, hivyo hakuna wa kumlaumu.

WANANCHI KILOSA JUU WAMLALAMIKIA MKUU WA WILAYA YA NYASA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.


BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Kilosa juu, wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma wamemlalamikia Mkuu wa wilaya hiyo, Margaret Malenga kwa kutumia amri ya kuwataka wahame katika maeneo yao wanayoishi kabla ya kulipwa fidia zao, ili waweze kumpisha mwekezaji anayetaka kutumia sehemu ya eneo la kijiji hicho kujenga kituo cha kuuza mafuta.

Aidha walisema kuwa wameshangazwa na kitendo hicho, wakidai kuwa anatumia nguvu kutaka wananchi hao waondoke jambo ambalo ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi, hivyo wanaiomba serikali kuingilia kati ili waweze kupata haki yao ya msingi.

Walisema kuwa wasipopewa malipo ya fidia zao ipasavyo, kamwe hawataweza kuhama mpaka utakapofanyika upembuzi yakinifu, juu ya malipo hayo katika maeneo yao wanayoishi.

Kadhalika walieleza kuwa, kumekuwa na usiri mkubwa uliogubikwa juu ya mwekezaji huyo ambapo mnamo Marchi 9 mwaka huu ulifanyika mkutano kijijini hapo na Mkuu huyo wa wilaya, na pale walipomtaka aeleze bayana juu ya nani anayetaka kuwekeza katika eneo hilo hakutaka kumtaja.

CCM RUVUMA KUANZA KUTUMBUA MAJIPU YAWATAKA WATENDAJI WAKE KUFANYA KAZI KWA UADILIFU

Upande wa kushoto, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho akimpatia mmoja wa wanachama wa UWT cheti cha pongezi na shukrani, baada ya kuongoza na kufanya kazi vizuri ndani ya jumuiya hiyo.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho amesema kwamba katika baadhi ya maeneo mkoani humo watendaji wake ndani ya chama, wamekuwa sio waaminifu kwenye matumizi ya fedha hivyo kufuatia kuwepo kwa hali hiyo wamejipanga kuwachukulia hatua ili kuweza kunusuru hali hiyo isiweze kuendelea na kuwaondoa hofu wanachama wa chama hicho.

Aidha alisema kuwa fedha hizo ni zile ambazo zinatolewa na jumuiya za chama na michango kutoka wadau mbalimbali, kwa ajili ya kukiendeleza chama. 

“Nawataka watendaji wafanye kazi kwa uadilifu mkubwa, ondoeni usumbufu ndani ya chama tumikieni chama kwa moyo wote na sio kuwa watu wa kubadilika, watu kama hawa hatuwahitaji ndani ya chama”, alisema Mwisho.

Mwenyekiti huyo alisema hayo jana kwenye kikao cha wajumbe wa baraza la wanawake wa CCM mkoani Ruvuma, ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa chama hicho mkoani humo.

Alisema kuwa uongozi wa mkoa huo ndani ya chama umekaa na kubaini kwamba, katika maeneo yake kuna watendaji ambao sio waaminifu na ni majipu ambayo inabidi yatumbuliwe ili kuweza kuleta heshima, kwa kuwapa adhabu ya kuwafukuza kazi na nafasi zao kuzibwa na wengine wenye kuzingatia maadili ya kazi ndani ya chama.

Wednesday, March 16, 2016

RAIS MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA KINYEREZI



MWALIMU AVULIWA MADARAKA KWA UTOVU WA NIDHAMU



Na  Kassian Nyandindi,
Songea.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amemvua madaraka na kumhamisha Makamu mkuu wa shule ya sekondari Namabengo, wilayani Namtumbo  mkoani humo, Shaibu Champunga ambaye alikuwa akituhumiwa na wanafunzi wa shule hiyo kwamba anawatolea lugha chafu, kuwadhalilisha, kuwashika matiti na makalio watoto wa kike pamoja na kuwachapa viboko visivyokuwa na idadi kinyume na sheria za shule.

Aidha Mwambungu alisema kuwa amechukua hatua hiyo, baada ya kwenda kusikiliza kero za wanafunzi hao ambao hivi karibuni  walikuwa wameandamana kwa kutembea kwa miguu, kutoka Namabengo kwenda Songea ofisini kwake kwa lengo la kutaka kuonana naye, licha ya kuwa maandamano hayo yalizuiwa na askari Polisi wa wilaya hiyo.

Hayo yalisemwa juzi na Mkuu huyo wa mkoa wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, juu ya sakata hilo la wanafunzi hao ambao kilio chao kimedumu kwa muda mrefu wakimlalamikia mwalimu wao, Champunga kutokana na kuwafanyia vitendo viovu ambavyo vinadhalilisha utu wao.

WAKUU WA MIKOA WAAGIZWA KUKUSANYA MAPATO KIKAMILIFU

Suleiman Jaffo.


Dar es Salaam.

NAIBU waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jaffo amewataka Wakuu wa mikoa hapa nchini, kuhakikisha kwamba wanasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ndani ya mikoa yao, ili fedha hizo ziweze kutatua matatizo ya wananchi yaliyopo katika mikoa yao.

Waziri huyo alisema hayo leo alipokutana na wakuu wapya wa mikoa, kabla ya kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi huku akiongeza kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na uzembe katika ukusanyaji mapato, hali ambayo inachangia mikoa mingi kushindwa kutatua matatizo yao binafsi na kutegemea msaada toka serikali kuu.

Pamoja na mambo mengine, amewataka wakuu hao wa mikoa, kushirikiana kikamilifu na watendaji wa mikoa yao, ili waweze kufanya kazi pamoja na endapo kutakuwa na ubadhirifu wowote wakuu hao wa mikoa wasifumbie macho, vitendo hivyo.

Tuesday, March 15, 2016

WANAFUNZI NALWALE TUNDURU WASHTAKI WAZAZI WAO



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANAFUNZI shule ya msingi Nalwale, iliyopo katika kata ya Nandembo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamewashtaki wazazi wao kwa uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) kwamba, wamekuwa wakipuuzia utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na mfuko huo.

Wanafunzi hao walibainisha hayo, wakati walipotembelewa na viongozi kutoka TASAF ngazi ya mkoa na wilaya na kuwashuhudia watoto hao, wakisoma wakiwa hawana sare na viatu miguuni mwao.

Aidha walifafanua kwamba mbali na wao kutambua umuhimu wa kuwapatia huduma hizo, bado wamekuwa wakipuuza na badala yake hutumia fedha zinazotolewa na mfuko  kwa shughuli nyingine.

Mwanafunzi Abibi Said anayesoma darasa la tatu katika shule hiyo, alisema kuwa kila anapomweleza baba yake amnunulie sare na viatu ili na yeye apendeze kama wenzake, amekuwa akijibiwa kuwa fedha alizopokea kupitia utaratibu wa uhaulishaji fedha kwa kaya maskini amezitumia kununulia mbolea.

MAJAMBAZI TUNDURU YAUA MWENYEKITI KWA RISASI NA KUPORA FEDHA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WATU wanaodaiwa kuwa ni majambazi, wamemuua kwa kumpiga risasi Mwenyekiti wa kitongoji cha Chilundundu, Zubery Mohamed (53) na kufanikiwa kumpora kiasi cha shilingi 80,000.

Sambamba na mauaji hayo, pia majambazi hao walipiga risasi nne hewani na kufanikiwa kupora kiasi cha shilingi 470,000 mali ya Mkalela Muhidin (28) tukio ambalo lilifanyika, majira ya usiku.

Zubery Mwombeji.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Marchi 11mwaka huu, katika kitongoji hicho kijiji  cha Misechela wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.

Baadhi ya mashuhuda walisema kwamba, katika matukio yote majambazi hao walitumia bunduki aina ya SMG na kwamba katika tukio la kwanza lililotokea kwenye kitongoji cha Mkalela kijiji cha Misechela, maharamia hao walifyatua hewani risasi na kufanya uporaji huo wa shilingi 470,000. 

Walisema katika tukio la pili maharamia hao, walimpiga risasi nne na kumuua Mohamed wakati akiwa anatumia upanga ili kuweza kupambana na majambazi hao, majira hayo ya usiku.

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUSHAMBULIWA NA FISI WAKATI AMELALA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKAZI mmoja wa kijiji cha Jiungeni kata ya Mchesi, tarafa ya Lukumbule  wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Mohamed Kilapile (75) amefariki dunia baada  ya kushambuliwa na fisi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo zinaeleza kuwa, fisi huyo alimvamia Kipalile na kumkata kichwa huku akiachanisha kiwiliwili chake na kutoweka nacho, kwa ajili ya kwenda kula nyama yake.

Tukio hilo lilitokea Marchi 9 mwaka huu, majira ya usiku wakati marehemu huyo akiwa amelala katika nyumba yake, ambayo haikuwa na mlango.

Godfrey Manyahi ambaye ni Afisa tarafa ya Lukumbule, alithibitisha kuwepo kwa mauaji hayo na kwamba hilo ni tukio la pili kutokea katika tarafa hiyo, mwaka huu.

Monday, March 14, 2016

SERIKALI KUJENGA MAHAKAMA NYASA MAPEMA MWAKA HUU


Na Kassian Nyandindi,

Nyasa.

SERIKALI hapa nchini imesema kwamba, ujenzi wa Mahakama katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma utaanza na kukamilika mapema iwezekanavyo mwaka huu, ikiwa ni lengo la kusaidia na kuwaondolea usumbufu wananchi wa wilaya hiyo katika kutafuta, kudai na kupata haki zao.

Wilaya ya Nyasa haina jengo la Mahakama tangu serikali ilipoianzisha miaka saba iliyopita, licha ya kuwepo kwa Hakimu mkazi mfawidhi ambaye hana hata ofisi ambapo wakati mwingine hulazimika kusafiri umbali mrefu kilometa 60 kwenda wilaya ya Mbinga, kuwahudumia wananchi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande alisema hayo hivi karibuni mara baada ya kuwasili katika mji mdogo wa Mbamba bay wilayani humo, akiwa katika ziara yake ya siku nne mkoani Ruvuma kukagua na kuangalia uendeshaji wa shughuli za mahakama mkoani humo.

Aidha Jaji Mkuu amewataka wananchi na wadau wengine wa mahakama kutoa ushirikiano kwa watendaji husika, ili kufanikisha  malengo yaliyojiwekea ya kumaliza usikilizaji wa kesi mbalimbali kwa wakati na kuwezesha wananchi kupata haki zao za msingi.

Pia alifafanua kuwa kuchelewa kwa ujenzi wa mahakama  wilayani Nyasa, kunatokana na ukosefu wa fedha hivyo serikali imeahidi kutoa fedha kwa ajili ya kujenga na kuzifanyia ukarabati baadhi ya  mahakama zake hapa nchini, ambazo majengo yake yapo katika hali mbaya.

MBINGA YABAINI KAYA ZISIZOSTAHILI MPANGO WA TASAF

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga hivi karibuni akisisitiza jambo katika moja ya vikao vyake wilayani humo ikiwemo akiwataka wananchi kujiunga na vikundi vya ujasiariamali.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

OFISI ya Mkurugenzi mtendaji, Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imefanya ufuatiliaji na kubaini kwamba, baadhi ya wanufaika waliopo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini katika wilaya hiyo hawana vigezo vya kuendelea kupata ruzuku katika mpango huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani humo, Ahasante Luambano alisema kuwa ofisi yake itaendelea kufanya ufuatiliaji mara kwa mara ili kuweza kuzibaini kaya hizo kwa utekelezaji zaidi.

MAJINA YA UTEUZI WAKUU WA MIKOA HAYA HAPA

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ATEUA WAKUU WA MIKOA



                                                                      
                                   TAARIFA HIZI NI KWA HISANI YA TOVUTI YA IKULU

OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM,
TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa wakuu wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara, ambapo kati yao 13 ni wapya, 7 wamebakizwa katika vituo vyao vya kazi, 5 wamehamishwa vituo vya kazi na 1 amepangiwa Mkoa Mpya wa Songwe.
Uteuzi huo umetangazwa na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe leo tarehe 13 Machi, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam.
Wakuu wa Mikoa walioteuliwa ni kama ifuatavyo;
  1. Mh. Paul Makonda - Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.
  2. Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Elias Kyunga - Mkuu wa Mkoa wa Geita.
  3. Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu - Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
  4. Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga - Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
  5. Brigedia Jeneral Mstaafu Emmanuel Maganga - Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
  6. Mh. Godfrey Zambi - Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
  7. Dkt. Steven Kebwe - Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
  8. Kamishna Mstaafu wa Polisi Zerote Steven - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
  9. Mh. Anna Malecela Kilango - Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
  10. 10.  Mhandisi Methew Mtigumwe - Mkuu wa Mkoa wa Singida.
  11. 11.  Mh. Antony Mataka - Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
  12. 12.  Mh. Aggrey Mwanri - Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
  13. 13.  Mh. Martine Shigela - Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
14. Mh. Jordan Mungire Rugimbana - Mkuu wa Mkoa Dodoma.
15. Mh. Said Meck Sadick - Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro.
16. Mh. Magesa Mulongo - Mkuu wa Mkoa Mara.
17. Mh. Amos Gabriel Makalla - Mkuu wa Mkoa Mbeya.
18. Mh. John Vianey Mongella - Mkuu wa Mkoa Mwanza.
19. Mh. Daudi Felix Ntibenda - Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
20. Mh. Amina Juma Masenza - Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
21. Mh. Joel Nkaya Bendera - Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
22. Mh. Halima Omary Dendegu - Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
23. Dkt. Rehema Nchimbi - Mkuu wa Mkoa wa Njombe.
24. Mhandisi Evarist Ndikilo - Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
25. Mh. Said Thabit Mwambungu - Mkuu wa Mkoa Ruvuma.
26. Luteni Mstaafu Chiku Galawa - Mkuu wa Mkoa wa Songwe (Mkoa mpya).

Wakuu wote wa Mikoa walioteuliwa, wataapishwa Jumanne tarehe 15 Machi, 2016 saa 3:30 Asubuhi Ikulu, Jijini Dar es salaam.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
13 Machi, 2016

Saturday, March 12, 2016

WALALAMIKIA KITENGO CHA TAALUMA ELIMU MSINGI SONGEA



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

KITENGO cha taaluma idara ya elimu msingi, Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kimetupiwa lawama kwa kile kinachodaiwa uwepo wa baadhi ya maofisa elimu wa idara hiyo kuigawa ofisi na kutengeneza makundi, hali ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango cha elimu katika manispaa hiyo na kuifanya kuwa ya mwisho, katika halmashauri nane zilizopo mkoani humo.

Baadhi  ya walimu, wakuu wa shule za msingi na waratibu elimu kata ambao wameomba majina yao yasitajwe gazetini wameulalamikia uongozi husika kwa kuendekeza chuki na majungu ambayo sasa yanasababisha kuvunjika moyo utendaji kazi kwa baadhi ya watumishi na halmashauri hiyo kuwa ya mwisho kimkoa matokeo ya mtihani wa taifa darasa la saba mwaka jana.

Walisema kuwa ni jambo la aibu kutokea, kwani Manispaa ya Songea ina shule chache ambazo wanaweza kuwafanya wanafunzi wafaulu mitihani yao vizuri kutokana na miundombinu ya shule hizo, kuwa mizuri tofauti na maeneo mengine ndani ya mkoa huo.

Walisema kitendo kinachofanywa na baadhi ya viongozi wa idara hiyo kinakwamisha maendeleo ya elimu, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuingilia kati na kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo ili lisiweze kuleta madhara baadaye katika jamii.

Thursday, March 10, 2016

RAIS MAGUFULI AFANYA ZIARA YA KUSHITUKIZA BENKI KUU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, akiwa ameongozana na Naibu Gavana wa Benki Kuu (BOT) Dkt. Natu Mwamba alipowasili makao makuu ya benki hiyo kwa kufanya ziara ya kushitukiza leo.


Wednesday, March 9, 2016

MKAGUZI WA NDANI OFISI YA MKUU WA MKOA RUVUMA ASHIKILIWA NA TAKUKURU

Yustina Chagaka, Mkuu wa TAKUKURU mkoani Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

PHILIMON Lenard ambaye ni Mkaguzi wa mahesabu ya ndani, Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, anashikiliwa na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani humo, akidaiwa kuhusika na vitendo vya rushwa katika utendaji wa kazi zake za utumishi wa umma.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa TAKUKURU  mkoani Ruvuma, Yustina Chagaka alisema kuwa Lenard alikamatwa Machi 4 mwaka huu majira ya mchana, baada ya ofisi yake kupata taarifa kutoka  kwenye vyanzo mbalimbali kuhusiana na vitendo vya rushwa alivyokuwa akivifanya.

WALIMU MBINGA WALALAMIKIA MAOFISA KUWATOLEA LUGHA MBAYA

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WALIMU wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamewalalamikia baadhi ya maofisa wa halmashauri ya wilaya hiyo kuwatolea lugha mbaya pale walimu hao, wanapokwenda katika ofisi za maofisa hao kupeleka shida zao za kikazi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Aidha wamesikitishwa na utunzaji mbaya wa kumbukumbu zao, jambo ambalo linasababisha walimu hulazimika kurudia kuzipeleka zaidi ya mara moja hasa pale wanapodai malimbikizo ya mishahara yao, na kwamba katika ofisi zinazohusika na kushughulikia tatizo hilo kuna baadhi ya walimu hawajafanyiwa hesabu za malimbikizo yao kwa muda mrefu.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya ya Mbinga, Wernery Mhagama alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya chama hicho wilayani humo, katika uzinduzi wa mafunzo ya siku moja ya walimu Wawakilishi mahali pa kazi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

Taarifa hiyo, ilikuwa ikitolewa kwa Ofisa utumishi wa wilaya ya Mbinga, Mwajuma Kihiyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo akimwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo.

DIWANI HALMASHAURI WILAYA YA MBINGA AFARIKI DUNIA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

DIWANI wa kata ya Maguu wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Nathaniel Hyera kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amefariki dunia, kutokana na kupata tatizo la ugonjwa wa shinikizo la damu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Ambrose Nchimbi alisema kuwa Hyera alifikwa na mauti Marchi 8 mwaka huu, majira ya asubuhi wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo.

Nchimbi alisema kuwa halmashauri yake, inasikitika kumpoteza diwani huyo kwani alikuwa ni mtu ambaye anatoa ushauri mzuri na kupigania maendeleo ya wananchi wake na wilaya hiyo kwa ujumla.

MADIWANI TUNDURU WASUSIA KIKAO CHA BAJETI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MADIWANI wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamesusia kuendelea na kikao cha kupitisha rasimu ya bajeti ya halmashauri ya wilaya hiyo, wakidai kuwa kumekuwa na tatizo la uchakachuaji mkubwa wa miradi ya wananchi wilayani humo.

Aidha walisema kuwa wameamua kufanya hivyo kutokana na kikao hicho kucheleweshwa kufanyika, huku sababu za msingi za kuchelewa huko hazijulikani.

Hayo yalisemwa na madiwani hao, katika mahojiano maalumu yaliyofanyika baada ya kutoka nje ya kikao hicho huku wakiongeza kuwa viongozi wa halmshauri hiyo baadhi yao wamekuwa hawatekelezi majukumu yao ya kazi ipasavyo, ikiwemo suala la ujenzi wa miradi ya wananchi.

Madiwani hao ambao wapo 16 kutoka katika vyama vinavyounda UKAWA wilayani Tunduru, walisema kilichowakera hasa ni kitendo cha kuchelewa kuanza kwa kikao hicho wakiwa wanamshinikiza Mwenyekiti wao, Mkwanda Sudi ili awaeleze ni sababu gani iliyowafanya wachelewe kuanza kwake sababu ambazo hazikutolewa.

Tuesday, March 8, 2016

AUAWA KWENYE CHUMBA CHA MAHABUSU NA WANANCHI WENYE HASIRA KALI



Na Mwandishi wetu,
Songea.

ERASTO Nditi (31) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kindimba juu wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa na kitu kizito kichwani.

Nditi aliuawa akiwa kwenye chumba cha mahabusu, katika Ofisi ya mtendaji wa kijiji hicho baada ya kuvamiwa na wananchi hao.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zuberi Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Marchi 3 mwaka huu majira ya saa 2:30 usiku.

Mwombeji alifafanua kuwa, wananchi hao walichukua maamuzi hayo magumu wakidai kwamba marehemu huyo enzi ya uhai wake alikuwa mkorofi, mwizi na amewahi kumkata mwananchi mwenzake, upanga mkononi wakati alipokamatwa akiiba.

WATIWA MBARONI KWA KOSA LA KULIMA BANGI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma, linawashikilia wakazi wawili wa kijiji cha Mseto na Liparamba wilayani Nyasa mkoani humo kwa tuhuma ya kukutwa wakiwa wamelima  mashamba mawili ya bangi,  yenye ukubwa wa ekari tano  ambayo inadaiwa kwamba yamekuwa yakitegemewa na watu wanaojihusisha na  biashara haramu ya kuuza bangi wilayani humo.

Zuberi Mwombeji.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zuberi Mwombeji akizungumza na gazeti hili jana ofisini kwake aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Thadei Ngonyani (26) mkazi wa kijiji cha Mseto na Philimoni Kumburu (58) wa Liparamba ambapo wote walikamatwa juzi majira ya saa za mchana.

Alifafanua kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na oparesheni yake kabambe katika maeneo mbalimbali mkoani humo, dhidi ya watu hao wanaojihusisha na kilimo cha zao la bangi na  kwamba msako huo ulianza  katika wilaya ya Nyasa.

Kamanda Mwombeji alieleza kuwa katika tukio la kwanza huko katika kijiji cha Mseto kilichopo kata ya Liparamba, tarafa ya Mpepo askari Polisi wakiwa kwenye msako huo walifanikiwa kumkamata Ngonyani, akiwa amelima zao hilo katika shamba lenye ukubwa wa ekari tatu.

WANAFUNZI NAMABENGO WASIMAMISHWA MASOMO KUTOKANA NA KUKOSA NIDHAMU



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WANAFUNZI 10 kati ya 106 wanaosoma kidato cha sita, shule ya sekondari Namabengo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wamesimamishwa kuendelea na masomo katika shule hiyo kwa muda wa wiki tatu, kutokana na kukosa nidhamu na kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Maandamano hayo walifanya wakielekea kwa Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu kwa lengo la kupeleka malalamiko yao dhidi ya Makamu mkuu wa shule hiyo, Shaibu Champunga wakimtuhumu kuwa na lugha na tabia chafu na vitisho kwa wanafunzi hao.

Katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo, Alkwin Ndimbo alipozungumza na mwandishi wetu alisema kwamba baada ya wanafunzi hao kufanya maandamano hayo, zilifanyika jitihada za kuwarudisha shuleni kwa lengo la kubaini chanzo cha maandamano hayo huku akimwagiza Ofisa elimu wa sekondari wilayani humo, Patrick Atanas ahakikishe anachukua hatua za haraka kwa kukutana na viongozi wa shule na wanafunzi hao, ili kuona tuhuma zinazomkabili Makamu mkuu wa shule hiyo.

Sunday, March 6, 2016

OMBENI SEFUE ATENGULIWA KATIKA NAFASI YA KATIBU MKUU KIONGOZI


MM INTERTAINMENT KUSAIDIA WATOTO YATIMA SONGEA

Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Ruvuma, Sikudhani Chikambo upande wa kulia, akikabidhi fedha taslimu shilingi laki moja jana kwa Mratibu na Mkurugenzi wa MM Intertainment, Marietha Msembele kama mchango wake kwa ajili ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Na Muhidin Amri,
Songea. 

BAADHI ya wanawake katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wametumia siku ya mwisho wa wiki kufanya zoezi la kuosha magari katika mitaa mbalimbali ya Manispaa hiyo mjini hapa, ili waweze kupata fedha kwa ajili ya kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu na wale wanaoishi katika mazingira magumu.
 
Mkurugenzi wa kampuni ya MM Intertainment iliyopo mjini hapa, Marietha Msembele ambaye ndiye Mratibu wa zoezi hilo  alisema kuwa wameamua kufanya hivyo, kwa kuuweka mpango huo kuwa endelevu na utalenga  kukusanya shilingi milioni  10 ambazo zitapelekwa kusaidia kununulia vifaa vya shule kama vile sare, viatu, vitabu, daftari na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya watoto hao ambao wapo katika Manispaa hiyo.

Alisema kuwa licha ya serikali, kutangaza na kuanza kutekeleza suala la elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari kidato cha nne nchini kote, hata hivyo bado kuna watoto ambao hadi sasa hawajaripoti katika shule hizo kutokana na kukosa mahitaji  muhimu na wapo bado majumbani, hivyo yeye na kampuni yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameamua kufanya hivyo ili kuweza kusaidia watoto hao.

WANAWAKE RUVUMA WAIOMBA SERIKALI KUONGEZA NAFASI ZA UPENDELEO

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, Farida Mdaula wa tatu kushoto akifurahia jambo na baadhi ya wanawake wenzake Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, baada ya kufungua zoezi la uoshaji magari kwa ajili ya kupata fedha za kusaidia watoto wenye mahitaji muhimu na wale wanaoishi katika mazingira magumu, wa tatu kulia ni Mkurugenzi wa kamapuni ya MM Intertaiment iliyoratibu zoezi hilo, Maretha Msembele.


Na Muhidin Amri,
Songea.

KUELEKEA siku ya wananawake duniani ambayo kila mwaka inafanyika Marchi 8, serikali imeombwa kuongeza nafasi za upendeleo kwa wanawake ili  kuwaongezea uwezo  wa kiutendaji, hasa pale wanapoteuliwa kushika  nafasi mbalimbali za uongozi na kuwaongezea nguvu katika kukabiliana na  changamoto zinazowakabili mbele yao katika maisha yao ya kila siku.

Rai hiyo ilitolewa jana mjini Songea na Mwanaharakati wa masuala ya wanawake na mfanyabiashara maarufu, anayeuza mafuta ya kuendeshea mitambo mbalimbali mkoani Ruvuma,  Farida Mdaula wakati  alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanawake wa Manispaa ya Songea, ambao waliamua kushiriki katika zoezi la usafi wa kuosha magari kwa ajili ya kutafuta fedha za kusaidia  watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wale waliokacha kwenda shule kwa kukosa mahitaji muhimu.

Alisema wanawake wengi wanakabiliwa na umaskini, hasa wa kipato na kukosa fursa ya kushirikishwa kwenye vyombo vya maamuzi na hata katika umilikaji wa rasilimali, licha ya ukweli kwamba ndiyo kundi  kubwa linalochangia maendeleo na kukua kwa uchumi wa nchi yetu.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI ATOA AMRI YA KUBOMOLEWA KWA KITUO CHA MAFUTA TUNDURU


Na Steven Augustino,
Tunduru.

NAIBU Waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani, ameamuru kuvunjwa mara moja kituo cha kuuza mafuta cha kampuni ya Cross roads, ambacho kinamilikiwa na Saleh Ahamad mjini Tunduru mkoani Ruvuma, ili kupisha ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Aidha Waziri huyo pia amemwagiza Katibu tawala wa wilaya hiyo, Ghaib Lingo kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Tunduru, kufanya uchunguzi juu ya uhalali uliotumika kumpatia kibali cha kujenga kituo hicho katika eneo ambalo sio rasmi.

Kwa mujibu wa maagizo hayo, Ngonyani ameagiza hatua kali zichukuliwe kwa wahusika wote ikiwa ni pamoja na kuwataka kumlipa fidia ya hasara atakayoipata, kutokana na zoezi hilo la uvunjaji litakapofanyika. 

Saturday, March 5, 2016

JENERALI MILANZI AWATAKA WANARUVUMA KUTUNZA VIVUTIO VYA UTALII

Mnara wa Mashujaa wa watu waliokufa, wakati wa vita vya Majimaji hapa mkoani Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MKOA wa Ruvuma, umetakiwa kuona umuhimu wa kuendelea kutunza vivutio vya utalii na kutumia fursa ya uwepo wa vivutio hivyo, kama njia mojawapo ya kujipatia kipato badala ya kuwaachia watu wengine kutoka nje ya mkoa huo wanufaike na rasilimali zilizopo ndani ya mkoa.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alitoa rai hiyo juzi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Songea mkoani humo, kwenye maadhimisho ya kumbukizi ya Mashujaa wa vita vya Majimaji na utalii wa utamaduni, yaliyofanyika katika viwanja vya Mashujaa vilivyopo Mahenge mjini hapa.

Jenerali Milanzi alisema kuwa serikali kupitia shirika la makumbusho ya Taifa, ipo tayari kutoa utaalamu na miongozo kwa wadau wote ambao wapo tayari kuanzisha makumbusho katika maeneo ya ndani na nje ya mkoa huo, ili kuweza kutoa fursa mbalimbali za uwepo wa vivutio vingi hapa nchini.

MKOA WA RUVUMA UNA ZIADA YA TANI MILIONI 1 ZA MAHINDI

Wakuu wa wilaya za mkoa wa Ruvuma, wakipokea maagizo ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na namna wanavyopaswa kusimamia utekelezaji huo.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MKOA wa Ruvuma una  ziada ya chakula tani milioni 1 za mahindi, ambazo zimetokana na ongezeko la uzalishaji katika msimu wa kilimo wa mwaka 2014/2015  uliofikia tani milioni 1.564,283 huku mahitaji halisi ya wananchi wake waishio katika mkoa huo, ni tani 469,172.

Uzalishaji wa zao hilo katika msimu huo, mkoa ulifanikiwa kuzalisha tani 689,123 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 17.3.

Kwa  mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika kipindi cha mwaka jana, zinaonesha kuwa wastani wa pato la mtu mmoja (Per capital income ) mkoani humo, limezidi kukua kutoka shilingi milioni 1,913,526 kwa mwaka 2013/2014 hadi kufikia shilingi milioni 2,082,167 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 8 kwa mwaka 2014/2015.