Tuesday, August 29, 2017

RAIS DOKTA MAGUFULI AONGOZA KIKAO CHA BARAZA LA MAWAZIRI IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu kiongozi pamoja na mawaziri wakisimama kwa heshima kumkumbuka aliyekuwa karani wa Baraza la Mawaziri Marehemu Hassan Rashid Shebuge aliyefariki mwezi Julai mwaka huu, kabla ya kuanza kikao hicho leo kilichofanyika Ikulu Jijini    Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli akiongoza kikao cha Baraza la Mawziri Ikulu Jijini Dar es salaam leo.(Picha na Ikulu)

WAKURUGENZI WATENDAJI RUVUMA WATAKIWA KUKAMILISHA UJENZI MIRADI YA UMWAGILIAJI

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge amewataka Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri za mkoa huo kukamilisha ujenzi wa skimu zote za umwagiliaji zilizopo mkoani hapa, ili ziweze kuanza kutumika kwa kilimo cha umwagilliaji.

Lengo la kukamilisha ujenzi huo Mkuu huyo wa mkoa alisema utaweza kuleta tija kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa mazao badala ya kutegemea kilimo cha msimu wa mvua.

Dokta Mahenge alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumza na wakurugenzi watendaji, wenyeviti wa halmashauri na wakuu wa wilaya wa mkoa huo katika kikao cha kazi kilichofanyika Ikulu ndogo mjini Songea.

BILIONI 14 KUJENGA BARABARA ZA LAMI MANISPAA YA SONGEA

Wataalamu wa Manispaa ya Songea wakikagua moja kati ya barabara ambazo zimejengwa kwa kiwango cha lami kwa ufadhili wa Benki ya dunia.
Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

MANISPAA ya Songea mkoani Ruvuma inatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 14.320 katika ujenzi wa barabara zake za mji huo kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 8.6.

Afisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa fedha za mradi huo zimetolewa na Benki ya dunia chini ya Mpango wa kuzijengea uwezo serikali za mitaa (ULGSP) kwa lengo la kuendeleza miundombinu ya halmashauri za Miji na Manispaa 18 zilizopo Tanzania bara ikiwemo Manispaa hiyo ya Songea.

Mradi huo ambao ulianza Juni Mosi mwaka 2015 alieleza kuwa ulitarajiwa kukamilika Juni 30 mwaka huu ambapo awali fedha iliyopokelewa na Manispaa hiyo ilikuwa ni zaidi ya shilingi bilioni saba ambayo imeanza kutekeleza mradi huo ambapo hadi sasa mkandarasi husika amekwisha lipwa kwanza shilingi bilioni nne.

WAKULIMA WA SOYA WAKABILIWA NA CHANGAMOTO LUKUKI

Na Mwandishi wetu,      
Songea.

MKOA wa Ruvuma umetajwa kuwa ni miongoni mwa mikoa michache hapa nchini ambayo inazalisha zao la Soya kwa wingi, huku changamoto kubwa ikiwa ni ukosefu wa soko la uhakika licha ya uzalishaji wake kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Dokta Binilith Mahenge ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akifungua kikao cha Wadau wa zao hilo ambacho kilijumuisha mikoa mitatu ya Ruvuma, Iringa na Njombe kilichofanyika katika Manispaa ya Songea mkoani hapa.

Alisema uzalishaji wa Soya umekuwa ukiongezeka toka msimu wa 2014/2015 na msimu wa mwaka 2016/2017 ambapo ulizalisha hekta 33,267 zilizoweza kutoa tani 32,331 ukilinganisha na msimu wa mwaka 2015/2016 ambao kulikuwa na hekta 19,026 zilizotoa tani 16,754.

RUVUMA KUONGEZA IDADI YA VITUO UPIMAJI SARATANI SHINGO YA KIZAZI

Na Mwandishi wetu,   
Songea.

ONGEZEKO la magonjwa yasiyoambukizwa katika mkoa wa Ruvuma imeelezwa kuwa yanasababishwa kwa kiasi kikubwa na mfumo wa maisha wanayoishi wananchi wa mkoa huo pamoja na ongezeko la watu wenye umri mkubwa katika jamii.

Aidha kutoshiriki mazoezi ya kimwili, ulaji wa mbogamboga, matunda na utumiaji wa pombe kupita kiasi nao umekuwa ukichangia wananchi kupata magonjwa hayo.

Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dokta Gozibert Mutangabarwa alisema hayo juzi alipokuwa akitoa taarifa juu ya hali ya tatizo la maradhi ya Saratani ya mlango wa kizazi na matiti,

Monday, August 28, 2017

WAKURUGENZI RUVUMA WAPIGWA MARUFUKU KUBADILI MATUMIZI YA FEDHA

Kutoka upande wa kulia ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dokta Binilith Mahenge, katikati ni Katibu tawala wa mkoa huo Hassan Bendeyeko na upande wa kushoto ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mkoani humo Suleiman Mwaliwale.
Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

DOKTA Binilith Mahenge ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amepiga marufuku Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoani humo, kubadilisha matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi bila kuwa na kibali maalum.

“Lazima tufuate kanuni na sheria zilizowekwa, huwezi kubadilisha matumizi ya fedha kutoka sehemu fulani kwenda kwenye mradi fulani wa maendeleo bila kibali maalum, cha msingi hapa ni lazima tufuate taratibu na sheria zilizowekwa”, alisisitiza.

Alitoa onyo hilo juzi alipokuwa akifunga kikao cha utekelezaji wa hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mkoani humo kwa mwaka 2015/2016 kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa Ikulu ndogo uliopo Songea mjini.

Sunday, August 27, 2017

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKUTANA NA MAKAMU WA RAIS WA CUBA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NAYE

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifanya mazungumzo ya kikazi na Makamu wa Rais wa Cuba, Gladys Bejarano katika mji wa Havana nchini Cuba jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Na Mwandishi wetu,

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba, Gladys Bejarano na kumhakikishia ufunguzi wa Ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini humo.

Aidha Majaliwa alisema kuwa Tanzania inatambua na kuthamini mahusiano mazuri ya kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi, kielimu, kiafya na kiutamaduni kati yake na Cuba hivyo inatarajia kufungua ubalozi nchini humo ili kuweza kurahisisha utendaji wa kazi za kibalozi.

Waziri Mkuu huyo alikutana na Makamu huyo wa Rais jana wakati alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi nchini Cuba ambapo malengo ya ziara hiyo yalikuwa ni kuimarisha na kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

HALMASHAURI ZA WILAYA MKOANI RUVUMA ZATAKIWA KUBORESHA MFUMO WA MANUNUZI


Baadhi ya washiriki wakiwa katika kikao cha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

IMEELEZWA kuwa Halmashauri za wilaya na Manispaa mkoani Ruvuma zisipoweka udhibiti wa kutosha katika eneo la manunuzi zitaendelea kuisababishia hasara serikali, hivyo zimetakiwa kuboresha udhibiti huo hasa kwenye kipengele cha manunuzi ya umma na kuweza kuimarisha ipasavyo miradi ya maendeleo ya wananchi.

Aidha kila Mkurugenzi katika halmashauri hizo ameagizwa kuwawezesha na kuwatumia wakaguzi wa ndani kikamilifu katika kutathimini ufanisi wa mifumo ya udhibiti wa ndani na kuchukua hatua stahiki, sambamba na kuziwezesha kamati za ukaguzi katika kutekeleza majukumu yao.

Mkuu wa mkoa huo, Dokta Binilith Mahenge alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha utekelezaji wa hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2015/2016 kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa Ikulu ndogo mjini hapa.

Saturday, August 26, 2017

TUNDURU WAPATIWA MSAADA WA KISHERIA

Na Steven Augustino,      
Tunduru.

WATEJA 456 waliopo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameweza kupatiwa msaada wa kisheria katika nyanja ya usuluhishi wa migogoro mbalimbali na kuwezeshwa kupata haki zao za msingi baada ya kuhitilafiana kwa muda mrefu.

Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la serikali wilayani humo, Tunduru Paralegar Center (TUPACE) John Nginga alisema hayo alipokuwa akitoa taarifa yake ya utekelezaji kwa Mkuu wa wilaya hiyo, Juma Homera.

Taarifa hiyo ilikuwa ikitolewa juzi wakati wa uzinduzi wa mradi wa ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma na uwajibikaji wa viongozi wa serikali kwa wananchi uliofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya wilaya hiyo uliopo mjini hapa.

Tuesday, August 22, 2017

MAMLAKA MAJI SAFI NA USAFI WA MAZINGIRA KUPINGA MAHAKAMANI HOJA YA BARAZA LA MADIWANI MBINGA

Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wakiwa kwenye kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika Agosti 17 mwaka huu kwenye ukumbi wa Umati mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, imesema kwamba ipo tayari kwenda Mahakamani kupinga hoja iliyopitishwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo juu ya ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya halmashauri ya wilaya hiyo, ambazo zinatarajiwa kujengwa katika eneo la Ndengu lililopo katika kata ya Nyoni wilayani humo.

Vilevile MBIUWASA wameeleza kuwa wakiwa kama wadau wakubwa wa eneo hilo katika suala la uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji hawajashirikishwa katika mchakato huo ili waweze kutoa ushauri wao kama eneo hilo linafaa kwa shughuli hizo za ujenzi au la.

Kauli hiyo ilitolewa na Meneja wa Mamlaka hiyo, Patrick Ndunguru wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake akieleza kuwa ni lazima wazingatie sheria ya athari za mazingira ya mwaka 2004 na wao wakiwa kama wadau wakubwa walipaswa washirikishwe kwanza kabla ya hoja hiyo kupitishwa katika vikao vya Madiwani.

DC AKEMEA VITUO VYA AFYA WILAYA YA MBINGA KUKOSA DAWA

Upande wa kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye akiwataka watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo kutekeleza majukumu waliyopewa na serikali kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa, kushoto ni Mkurugenzi mtendaji Gombo Samandito na katikati ni Mwenyekiti wake wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Ambrose Nchimbi.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amesema kwamba ni aibu kuona au kuendelea kusikia katika zahanati na vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo wilayani humo, kwamba fedha zipo za kununulia dawa lakini wagonjwa wanalalamika hakuna dawa.

Nshenye alisema kuwa hivi karibuni alitembelea katika baadhi ya vituo hivyo wilayani hapa na kukuta malalamiko hayo ambapo kufuatia hali hiyo ameagiza kuwa endapo itaendelea sasa utafika wakati wa wahusika kuwajibishwa pale atakapoona kuna tatizo kama hilo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema hayo wakati alipokuwa akihutubia katika kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani humo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.

Monday, August 21, 2017

WADAU WAPINGA ENEO LA UJENZI OFISI ZA HALMASHAURI WILAYA YA MBINGA

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga

BAADHI ya Wadau wa maendeleo na mazingira katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wameanza kupinga hoja iliyopitishwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo, juu ya ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani humo ambazo zinatarajiwa kujengwa katika eneo maarufu linalofahamika kwa jina la Ndengu lililopo katika kata ya Nyoni wilayani hapa.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye.

Wadau hao walisema hayo kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wakidai kwamba hawakubaliani na maamuzi hayo kwani eneo hilo ambalo wanataka kujenga ofisi hizo, lilitengwa na kuhifadhiwa kwa miaka mingi kwa ajili ya kutunza mazingira na vyanzo vya maji vilivyopo huko ambavyo ndiyo tegemeo kubwa kwa ajili ya kulisha wakazi wa mji wa Mbinga.

Aidha walifafanua kuwa wakiwa kama wadau wakubwa wa mazingira wanatambua kuwa pale panapojitokeza kuwa na uwekezaji mkubwa kama huo ni lazima kwanza kufanyike tathimini ya athari za mazingira katika eneo kama hilo ambako ujenzi wa ofisi hizo wanataka kuufanya kwa kushirikisha maoni ya wataalamu wa sekta ya mazingira na sio kuchukua maamuzi kama hayo peke yao.

“Unajua leo panapokuwa na makazi katika eneo kama lile ni lazima uzalishaji wa taka utakuwa mkubwa hasa kipindi cha masika mvua zitakapokuwa zinanyesha maji yake yatakayokuwa yanatiririka ambayo yamebeba taka nyingi zitakazokuwa zinazalishwa pale, zitakuwa zinaangukia kwenye bonde lile ambalo lina vyanzo vya maji vinavyolisha wakazi wa mji huu ni lazima jambo hili tunapaswa kuwa waangalifu”, alisema Jordan Ndunguru.

MBIO ZA MARATHON SELOU NAMTUMBO KUFANYIKA SEPTEMBA MWAKA HUU

Na Mwandishi wetu,    
Namtumbo.

KAMPUNI tanzu ya Mantra inayochimba madini ya Uranium One na ROSATOM wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, imedhamini mbio za Marathon Selou Namtumbo ambazo zinatarajiwa kuanza kufanyika mapema mwezi Septemba mwaka huu.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Mkuu wa wilaya ya hiyo, Luckness Amlima alisema kuwa mbio hizo zitakuwa za urefu wa kilometa 2.5 kwa wanawake, kilometa tano kwa wanawake na wanaume na kilometa 21 kwa wanawake na wanaume ambapo zina lenga kuhamasisha michezo na kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wanawake na jengo la upasuaji wilayani hapa.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa lengo ni kukusanya shilingi bilioni 7 ambazo kama zitapatikana zitaweza pia kutosheleza kujenga hospitali ya wilaya ya Namtumbo.

NYASA WANUFAIKA NA WASAIDIZI WA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU

Ziwa Nyasa.
Na Julius Konala,   
Nyasa.

MKUU wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Isabella Chilumba amelipongeza shirika lisilo la kiserikali la Wasaidizi wa Sheria na Haki za Binadamu (WASHEHABINYA) wilayani humo kwa kuendesha mafunzo juu ya utawala bora kwa wananchi pamoja na viongozi wa vijiji na kata, ambayo yameweza kuwajengea uwezo namna ya kuishi na kufanya shughuli zao za kimaendeleo.

Aidha mafunzo hayo yamefanyika kwa siku tatu katika kata nne za wilaya hiyo ambayo yamefadhiliwa na shirika la The Foundation For Civil Society (FCS) kutoka Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa wilaya hiyo, Chilumba ndiye aliyefungua mafunzo hayo juzi mjini hapa yaliyoshirikisha baadhi ya wananchi, wenyeviti wa vitongoji, vijiji, pamoja na maofisa watendaji wa kata.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa mradi huo umefika wakati muafaka kwa kile alichoeleza kuwa wananchi wengi hawajui haki zao za msingi, kutokana na kutojua sheria pamoja na kushindwa kesi zao mbalimbali Mahakamani kwa sababu ya ukosefu wa msaada wa kisheria.

Sunday, August 20, 2017

HALMASHAURI ZAAGIZWA KUKAMILISHA MPANGO WA TAIFA WA VIPIMO KATIKA ZAHANATI NA VITUO VYA AFYA

Na Mwandishi wetu,
Arusha.

SERIKALI hapa nchini, imeagiza Halmashauri zote ambazo hazijakamilisha mpango wa taifa wa kutoa huduma za vipimo kwenye zahanati na vituo vya afya kuhakikisha kwamba inakamilisha huduma hiyo, ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.

Agizo hilo limetolewa juzi na Naibu Waziri wa afya, Dokta Khamis Kigwangala katika ziara yake ya siku tano, wakati alipokuwa akitembelea vituo vya Afya na zahanati za Jiji la Arusha kwa lengo la kuangalia utendaji kazi na changamoto zilizopo katika kutekeleza agizo la uboreshaji wa huduma ya upimaji wa magonjwa mbalimbali.

Dokta Kigwangala alisema kuwa Rais Dokta John Pombe Magufuli alikwisha toa maelekezo ya kuimarisha na kuboresha kwa huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati na vituo hivyo vya afya alipokuwa akifungua kikao cha Bunge mjini Dodoma, kwa lengo la kuokoa maisha ya wananchi ili waweze kupata vipimo vya magonjwa katika maeneo wanayoishi kwa urahisi.

Alisema kuwa Wizara ya afya katika kuhakikisha agizo hilo la Rais Dokta Magufuli linatekelezwa ipasavyo imetoa msisitizo wa utekelezaji huo ikiwemo pia hata sera ya Wizara hiyo inazitaka halmashauri zote kuhakikisha kwamba huduma hiyo ya vipimo vya magonjwa ya kawaida inapatikana kuanzia kwenye ngazi ya zahanati hadi vituo vya afya.

WANAFUNZI TUNDURU WAPOTEZA MAISHA BAADA YA KUFUKIWA NA KIFUSI CHA UDONGO

Wananchi wakiwa katika eneo la tukio wakati miili ya wanafunzi wa shule ya msingi Chikomo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ikitafutwa baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo wakati wakichimba mchanga.
Na Steven Augustino, 
Tunduru.

WANAFUNZI wawili wanaosoma katika shule ya msingi Chikomo iliyopo katika kata ya Mbesa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na kifusi cha udongo wakati wakichimba mchanga.

Tukio hilo lilitokea Agosti 15 mwaka huu na kwamba katika tukio hilo wanafunzi hao walikuwa wakichimba mchanga kwa ajili ya matumizi ya ujenzi wa darasa katika shule yao.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Kamishina Mwandamizi wa Polisi, Gemini Mushi aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Sophia Ngongi na Semen Selemani wote wanaosoma darasa la tatu katika shule hiyo.

Akizungumzia tukio hilo Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Omary Melle alisema kuwa tukio ajali hilo lilitokea majira ya saa 9:20 baada ya wanafunzi hao wakiwa wametoka darasani muda wa masomo kwisha.

SERIKALI YATOA SIKU SABA KWA MBUNGE TUNDU LISSU KUOMBA RADHI NA KUFUTA MANENO YAKE


Saturday, August 19, 2017

SERIKALI YAJIBU MADAI YALIYOTOLEWA NA TUNDU LISSU

Serikali kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa imejibu madai yaliyotolewa jana na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kuwa ndege ya Tanzania, Bombadier kuwa imeshikiliwa nchini Canada kutokana na serikali kudaiwa.

Soma taarifa kamili:

Mnamo tarehe 18 Agosti, 2017 siku ya Ijumaa, kuna taarifa zimetolewa kwenye vyombo vya habari kwamba kuna mgogoro wa utekelezaji wa ununuzi wa ndege ya tatu inayonunuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kampuni ya Bombadier ya nchini Canada.

Taarifa hiyo iliendelea kudai kwamba kuna wanasheria wa Kampuni fulani ya nchini Italia, walioweka zuio la ununuzi wa ndege hiyo kwa maelezo kwamba, wanakamata mali hiyo ya Serikali kwa kuwa kuna Kampuni inayodai Serikali ya Tanzania.

Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali inapenda kuufahamisha Umma kuwa mgogoro huo upo ila kimsingi ni mgogoro ambao umetengenezwa na Watanzania wenzetu ambao kwa bahati mbaya sana wameweka maslahi ya kisiasa na ya binafsi mbele zaidi ya maslahi ya Taifa.

MADIWANI WAMWAJIBISHA MHANDISI IDARA YA MAJI MBINGA

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, wakisikiliza kwa makini maamuzi yaliyochukuliwa katika kikao chao cha baraza la Madiwani kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa Umati mjini hapa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mbinga, Ambrose Nchimbi akitangaza maamuzi yaliyochukuliwa na baraza la Madiwani wake dhidi ya Mhandisi wa idara ya maji wa halmashauri hiyo Vivian Mndolwa mara baada ya kuketi juzi katika kikao cha baraza la Madiwani kupitia kamati yake ya mamlaka ya nidhamu, upande wa kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Gombo Samandito.
Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imemrejesha kazini Mhandisi wa idara ya maji wilayani humo Vivian Mndolwa huku akipewa adhabu ya kukatwa na kupokea nusu ya sehemu ya mshahara wake katika kipindi cha mwaka mmoja.

Adhabu hiyo imetolewa juzi na baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo katika kikao chao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Umati mjini hapa ambapo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ambrose Nchimbi alisema hayo mbele ya baraza hilo mara baada ya kuketi kikao cha kamati ya mamlaka ya nidhamu kwa muda wa zaidi ya masaa matatu na kufikia muafaka wa kutoa adhabu hiyo.

Nchimbi alisema kuwa utekelezaji wa adhabu hiyo unaanza mapema kuanzia sasa mwezi Agosti mwaka huu na kwamba inafuatia baada ya Mhandisi huyo kupatikana na tuhuma ya kushindwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa mradi wa maji uliopo katika kitongoji cha Mnazi mmoja, kijiji cha Mkako kata ya Mkako ambao unadaiwa kujengwa chini ya kiwango na kushindwa kuwafikishia maji ipasavyo wananchi katika maeneo husika ndani ya kata hiyo.

BARAZA LA MADIWANI MBINGA LAMALIZA MVUTANO UJENZI WA MAKAO MAKUU OFISI ZA HALMASHAURI YA WILAYA

Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga wakiwa katika kikao chao cha baraza la madiwani.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Gombo Samandito aliyesimama amevaa joho rangi nyekundu, akisimamia zoezi la kuhesabu kura ni wapi Madiwani wa wilaya hiyo wamechagua sehemu ambayo kutajengwa Ofisi za makao makuu ya halmashauri hiyo.
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma limepitisha kwa pamoja na kukubaliana kwamba, ujenzi wa Ofisi za makao makuu ya wilaya hiyo zitajengwa katika eneo maarufu linalofahamika kwa jina la Ndengu lililopo katika kata Nyoni wilayani humo.

Maamuzi hayo yalifikiwa juzi katika kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa, baada ya uwepo wa mvutano mkubwa uliodumu kwa masaa kadhaa kati ya Madiwani hao na Watendaji wa halmashauri hiyo juu ya wapi Ofisi hizo zitajengwa.

Awali zilipopigwa kura kwa lengo la kukubaliana kwamba ujenzi huo ukafanyike katika eneo la Kiamili lililopo katika kata ya Kigonsera, Madiwani hao walikataa na kukubaliana kwamba zipigwe kura kwa mara ya pili kwa kuchagua kati ya eneo la Maguu, Ndengu na Matiri.

Friday, August 18, 2017

IDARA ZA SERIKALI MANISPAA SONGEA ZAINGIA KATIKA KASHFA NZITO

Mhasibu wa Mamlaka ya Maji safi na Uhifadhi Mazingira (SOUWASA) Leonard Luhagila akiwaonesha baadhi ya Waandishi wa habari mitambo mipya ya kusukumia maji katika chanzo cha mto Luhira katika Manispaa ya Songea jana ambapo gharama za uendeshaji wake kwa mwezi ni kati ya shilingi milioni 20 hadi 25.
Na Mwandishi wetu,       
Songea.

MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (SOUWASA) katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, inazidai baadhi ya taasisi na idara za serikali fedha zaidi ya shilingi milioni 794,118,058.38 ikiwa ni malimbikizo ya ankra ya maji hadi kufikia Julai 30 mwaka huu baada ya kusambaza huduma ya maji kwa taasisi hizo.

Aidha licha ya mamlaka hiyo kutoa notisi kwa idara na taasisi hizo ikizitaka kulipa deni hilo kuanzia Juni 28 mwaka huu hali imekuwa kinyume na kwamba ni taasisi mbili tu ambazo ni shule ya sekondari ya wasichana Songea iliyopo mjini hapa iliyokuwa inadaiwa shilingi 6,295,128.00 ambayo imelipa deni lake kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Chuo cha waganga wasaidizi Songea ambacho kimepunguza shilingi milioni 10 kati ya shilingi milioni 30,209,469.22 ambazo kilikuwa kinadaiwa.

Kaimu Mkurugenzi wa SOUWASA Mhandisi John Kapinga alisema kuwa Hospitali ya rufaa Songea ndiyo inayoongoza kwa kudaiwa shilingi milioni 276,233,440.73, ikifuatiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) shilingi 126,690,090.10, Magereza ya mkoa shilingi 153,594,369.55 na Polisi inayodaiwa shilingi 101,229,537.40.

MANISPAA YA SONGEA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE

Na Muhidin Amri,         
Songea.

MANISPAA ya Songea mkoani Ruvuma imenunua mtambo wa kisasa wa kuzolea taka (Kijiko) ambacho kitaalamu kinafahamika kwa jina la Back hoe loader kilichogharimu zaidi ya shilingi milioni 170 kutoka kampuni ya Hansom Tanzania Limited ambapo Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoani humo amekagua mtambo huo na kuthibitisha kuwa upo salama.

Afisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alimweleza mwandishi wetu kuwa tayari mtambo huo umeanza kufanya kazi ya ukusanyaji wa taka ngumu katika viunga vya Songea, hivyo kuweza kupunguza muda wa kuzoa taka kwa kutumia nguvu kazi hali ambayo imesaidia kuufanya mji wa Songea kuonekana kuwa wa kuvutia kutokana na kasi ya kuondoa taka hizo zilizokuwa kero kubwa katika maeneo mbalimbali ya mji huo.

Midelo alisema kuwa kwa wastani Manispaa ya Songea imekuwa ikizalisha taka kiasi cha tani 71.5 kwa siku ambapo uwezo wa Manispaa hiyo kuzoa taka hizo kwa siku ni kati ya tani 35 hadi 40 na kwamba hivi sasa inatarajia kuongeza uwezo wake wa kuzoa taka hizo kwa siku kutokana na kununua mtambo huo.

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUHAMASISHA UWEKEZAJI MKOANI RUVUMA

Na Muhidin Amri,        
Songea.

IKIWA uchumi wa mkoa wa Ruvuma unatajwa kukua kwa kasi kwa wastani wa pato la mwananchi wa kawaida linalofikia shilingi milioni 2.6 mwaka 2016 hadi 2017 kutoka shilingi milioni 2.2 mwaka 2013, wito umetolewa kwa waandishi wa habari wa mkoa huo kutumia kalamu zao kuandika habari zinazohamasisha watu wenye uwezo na makampuni mbalimbali kwenda kuwekeza katika sekta ya kilimo kutokana na maeneo mengi mkoani humo hufaa kwa kilimo.

Aidha serikali imeombwa kutenga fedha za kutosha kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NRFA) Kanda ya Songea ili aweze kununua kiasi kikubwa cha mahindi ambacho kimezalishwa kwa wingi katika maeneo ya mkoa huo ili kuepusha uwezekano wa wananchi kupata hasara.

Hayo yalisemwa jana na baadhi ya wakulima wanaoendelea na maonesho yao ya bidhaa za kilimo katika viwanja vya nane nane kata ya Msamala Manispaa ya Songea mjini hapa huku wakisisitiza kuwa ni vyema sasa waandishi wa habari wakawa wazalendo kwa kuandika habari hizo zenye kuchochea uwekezaji na shughuli zote za maendeleo ya wananchi.

Wednesday, August 16, 2017

RC RUVUMA AZIJIA JUU TAASISI ZA UMMA ZISIZOLIPA BILI ZA MAJI SONGEA AAGIZA KUSITISHA HUDUMA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge akitoa maagizo juu ya kusitisha huduma ya maji kwa idara na taasisi zote za umma zilizopo katika Manispaa ya Songea.
Na Muhidin Amri,       
Songea.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Songea (SOUWASA) kusitisha mara moja huduma ya maji kwa idara na taasisi zote za umma zilizopo chini ya Manispaa ya Songea kutokana na deni kubwa la huduma ya maji, lililofikia zaidi ya shilingi milioni 6,574,686.79 ambazo Manispaa hiyo haijaonesha dalili za kulipa deni hilo.

Akizungumza juzi katika kikao maalumu kati  ya viongozi wa SOUWASA na uongozi wa Manispaa hiyo uliowakilishwa na Mhandisi wa maji, Samwel Sanya Dokta Mahenge alisema kuwa amelazimika kutoa agizo hilo  baada ya kuchoshwa na tabia ya viongozi wake kutoonesha ushirikiano licha ya kupewa taarifa ya kuwataka kulipa fedha kwa mamlaka hiyo.

Dokta Mahenge alisema kuwa amechoshwa na tabia ya uongozi wa Manispaa ya Songea chini ya Mkurugenzi wake Tina Sekambo, ambaye mara kwa mara ameonekana kukaidi na kudharau hata maagizo ya viongozi wake wa juu ikiwemo juu ya kulipa madeni ya Wenyeviti wa mitaa ambao wamekuwa msaada mkubwa katika shughuli za kukusanya mapato na ulinzi katika mitaa yao.

UGONJWA WA AJABU WASUMBUA WANAFUNZI SONGEA

Baadhi ya Wanafunzi wa shule ya msingi Subira katika Manispaa ya Songea wakiwa katika hofu kutokana na ugonjwa wa ajabu ulioikumba shule hiyo.
Na Mwandishi wetu,      
Songea.

UGONJWA wa ajabu ambao haujafahamika jina lake, umezuka shule ya msingi Subira iliyopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma na kusababisha wanafunzi 335 kutohudhuria masomo yao darasani tangu mwezi Machi mwaka huu.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Majidu Ngonyani alisema kuwa shule ina jumla ya wanafunzi 578 lakini wanafunzi wanaohudhuria masomo mpaka sasa ni 243 tu ambao ni sawa na asilimia 42 kutokana na tatizo hilo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Ngonyani alisema kuwa wanafunzi wanaopata ugonjwa huo hasa ni wa kike na kwamba hadi sasa licha ya madaktari kuchukua vipimo kwa wanafunzi wanaougua bado haijafahamika ni ugonjwa wa aina gani.

Monday, August 14, 2017

KITUO CHA AFYA MJIMWEMA SONGEA KIMEANZA KUTOA HUDUMA YA UPASUAJI AKINA MAMA WAJAWAZITO

Mganga mkuu wa Manispaa ya Songea, Mameritha Basike akimjulia hali mgonjwa Mary Lupindu ambapo mgonjwa huyo ni wa kwanza kufanyiwa upasuaji katika kituo cha afya Mjimwema Songea.
Na Mwandishi wetu,   
Songea.

UTEKELEZAJI wa sera ya afya katika kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma ya afya kwa wananchi kituo cha afya Mjimwema kilichopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma umeanza kufanyika, ambapo kituo hicho kimeanza kutoa huduma ya upasuaji kwa akinamama wajawazito.
Mary Lupindu akiwa amewashika watoto wake mapacha.

Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dokta Mameritha Basike alisema kuwa wameanza kutoa huduma hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dokta Khamis Kigwangala ambaye aliagiza huduma ya upasuaji ianze kutolewa mara moja katika kituo hicho ili kuweza kunusuru afya za akinamama hao.

Dokta Basike alisema kuwa kitengo hicho cha upasuaji hivi sasa kinao uwezo wa kufanya hadi Operesheni saba kwa siku na kwamba wakiongezeka madaktari watakuwa na uwezo wa kufanya upasuaji kati ya watu 10 hadi 15 kwa siku.

Alisema wana madaktari wa upasuaji watatu na kwamba wanahitaji madaktari wengine nane, wauguzi 12 na kuongezewa vifaa vya upasuaji ili kuhakikisha kwamba wanafanyakazi zao kwa ufanisi zaidi.

Friday, August 11, 2017

SONGEA YAKABILIWA NA TISHIO LA KUGEUKA KUWA JANGWA

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

WILAYA ya Songea mkoani Ruvuma inakabiliwa na tishio la kugeuka kuwa jangwa kutokana na wananchi wanaoishi wilayani humo kukata miti hovyo huku wengine wakichoma misitu moto na baadhi ya watumishi wa serikali wasiokuwa waadilifu kuruhusu wafugaji kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini kuingiza idadi kubwa ya mifugo bila kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.

Mkuu wa wilaya hiyo, Pololet Mgema alisema hayo jana wakati akitoa salamu za serikali katika kikao cha baraza la Madiwani halmashauri wilaya ya Songea kilichofanyika katika kijiji cha Lundusi kata ya Maposeni wilayani humo.

“Kuna uharibifu mkubwa katika mlima Lihanje na nimekuwa nikitoa maagizo kwa watendaji wetu mara kwa mara kusitisha shughuli za kilimo katika mlima ule hata hivyo bado imeonekana baadhi ya wananchi wanaendelea kukata miti hovyo na kuendesha shughuli zao za kibinadamu, kuna watumishi pia ambao ni wagumu kutekeleza maagizo ya serikali sasa mimi mwenyewe nitaanza operesheni ya kuwaondoa ndugu zenu lakini msije kunilaumu kwa hatua nitakayochukua”, alisisitiza Mgema.

WAKULIMA WAILILIA SERIKALI WAIOMBA IWARUHUSU KUUZA MAHINDI YAO NJE YA NCHI

Na Mwandishi wetu,     
Songea.

LICHA ya serikali kuwataka wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya chakula kama vile mahindi kutopeleka nje ya nchi kwa ajili ya kuyauza, baadhi ya wakulima mkoani Ruvuma wameiomba serikali kuwaruhusu kupeleka huko kwa ajili ya kutafuta soko ili kunusuru hasara itakayoweza kuwapata kutokana na wengi wao kuwa na mahindi mengi.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa baadhi yao Cosmas Ndunguru na Iman Mapunda walisema kuwa serikali haina budi kuwaonea huruma na kulegeza masharti iliyoweka ili kuweza kutoa fursa kwao kwa lengo la kuweza kupata soko la uhakika.

Walisema kuwa lengo la serikali kuzuia mahindi yasiuzwe nje ya nchi ni jambo zuri kwani linalenga kuchukua tahadhari ya kutokea kwa tatizo la njaa hasa katika mikoa yenye upungufu mkubwa wa chakula lakini waliongeza kuwa kutokana na uzalishaji kuwa mkubwa hata wakiruhusu kuuza mahindi nje bado taifa litakuwa na akiba ya kutosha ya chakula.

Thursday, August 10, 2017

MAKALA: MAMLAKA YA MAJI SAFI NA USAFI WA MAZINGIRA MBINGA NA MIKAKATI YA KUBORESHA HUDUMA ZAKE


Pichani ni tanki kubwa la maji ambalo limejengwa na Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) mji wa Mbinga mkoani Ruvuma ambapo hivi karibuni, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Amour Hamad Amour alikagua mradi huo na kuufungua tayari kwa kuanza matumizi kwa wakazi wa mji huo na kwamba tayari tanki hilo limekuwa likitumika kusambaza maji kwa wakazi wa mji wa Mbinga.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour akiwa amepanda juu ya tanki hilo kubwa la maji ambalo limejengwa na Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, kwa lengo la kuukagua mradi huo ambapo kiongozi huyo wa mbio za Mwenge alipongeza ujenzi huo umefanyika kwa ubora unaotakiwa na kwamba hivi sasa tayari tanki hilo limekuwa likitumika kusambaza maji kwa wakazi wa mji huo. (Picha zote na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,

UMUHIMU wa maji katika maisha ya binadamu au kiumbe chochote kile kilichokuwa hai hapa duniani ni jambo ambalo halina mjadala, kutokana na hilo ndio maana serikali mara zote imekuwa ikihimiza umuhimu wa kutunza mazingira ili kunusuru vyanzo vya maji vilivyopo viweze kuwa endelevu katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Tatizo la kukosekana kwa maji linaweza kusababisha matatizo mengi katika jamii ikiwemo kutokea kwa magonjwa ya mlipuko na maji  hayo endapo yanapatikana kwa shida, hugeuka na kuwa karaha  hasa kwa akinamama ambao ndio watu wanaohusika kwa kiasi kikubwa kuyatafuta.

Baada ya kuona umuhimu huo, serikali imeamua kuanzisha Mamlaka za maji ambazo zimekuwa zikisaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza au kuondoa tatizo la upatikanaji wa maji katika maeneo ya miji.

Halmashauri ya mji wa Mbinga iliyopo mkoani Ruvuma, kuna Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) ambayo hivi sasa imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mji huo, katika kuendeleza huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Mwandishi wa makala haya kwa kushirikiana na vyanzo mbalimbali vya habari amebaini kuwa katika mji huo kumekuwa na vyanzo sita vya maji, ambavyo vimeainishwa kwa ajili ya kuhudumia wananchi ili waweze kuondokana na tatizo la upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Wednesday, August 9, 2017

MANISPAA YA SONGEA WAPO HATARINI KUUGUA MAGONJWA YATOKANAYO NA MIFUGO


Mkaguzi wa mifugo katika machinjio ya Msamala Manispaa ya Songea, Angela Mbata upande wa kulia akiwaonesha juzi baadhi ya wananchi waliofika kwenye banda hilo la mifugo la nyama ya ng'ombe zilizopatwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo majipu kwenye ini na mapafu ambayo endapo binadamu akila kuna hatari kubwa ya kuambukizwa magonjwa hayo.
Na Muhidin Amri,      
Songea.

IMEELEZWA kuwa wakazi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wapo hatarini kuugua magonjwa yatokanayo na mifugo ikiwemo ugonjwa wa majipu na TB baada ya kubainika kwamba, baadhi ya wafanyabiashara wachache wamekuwa wakichinja na kuuza nyama bila kukaguliwa na madaktari wa mifugo.

Hayo yalisemwa juzi na mkaguzi wa mifugo katika machinjio ya Msamala katika Manispaa hiyo, Angela Mbata wakati alipokuwa akitoa elimu ya mifugo na umuhimu wa kula nyama iliyopimwa kwa wananchi waliohudhuria kwenye maonesho ya wakulima maarufu kwa jina la nanenane mkoani hapa yaliyofanyika katika kata ya Masamala.

Mbata alifafanua kuwa uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa ng’ombe 15 kati ya 30 wanaoletwa na wafugaji mkoani humo kutoka katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kuchinjwa, imebainika kuwa na ugonjwa wa minyoo kwenye ini na mapafu ambayo husababisha majipu jambo ambalo ni hatari kubwa kwa walaji.

TASAF SONGEA YAANZA NA MFUMO WA MALIPO KWA NJIA YA MTANDAO KAYA MASKINI


Wataalamu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakiwa pamoja na wanufaika wa mfuko huo wakati wakikagua manufaa ya matumizi ya mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao.
Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, umeanza kutoa malipo kwa njia ya mtandao kwa kaya maskini 4,959 zilizopo katika mpango wa kunusuru kaya hizo katika Manispaa hiyo.

Christopher Ngonyani ambaye ni Mratibu wa TASAF katika Manispaa ya Songea alisema kuwa wanufaika 604 tayari wamesajiliwa kwa ajili ya kulipwa kwa njia ya mitandao ya simu, ambapo kati yao wanufaika 475 wameingiziwa fedha zao katika malipo ya mwezi Julai hadi Agosti mwaka huu.

Alisema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba wanufaika wote wanaingizwa kwenye mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao ambapo malipo yatakuwa yanalipwa moja kwa moja na TASAF kutoka makao makuu ya mfuko huo badala ya fedha za wanufaika hao kutumwa kupitia halmashauri husika kama ilivyokuwa hapo awali.

Monday, August 7, 2017

DOKTA MAGUFULI AREJEA JIJINI DAR ES SALAAM NA KUHUTUBIA UMATI WA WANANCHI ULIOMSIMAMISHA BAADA YA KUMALIZA ZIARA YAKE MKOANI TANGA

Baadhi ya wananchi wa eneo la Bunju wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli, wakati alipokuwa akizungumza aliposimama kwenye eneo hilo kuwasalimia wananchi hao wakati akirejea jioni ya leo Jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku tano mkoa wa Tanga.  
Watu wenye ujumbe wenye maneno ya aina mbalimbali nao hawakuwa mbali. 
Rais Dokta John Pombe Magufuli akimfariji mmoja wa wafanyabiashara wadogo waliopata changamoto eneo la Bunju A wilaya ya Kinondoni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Rais Dokta John Pombe Magufuli akishangiliwa na umati wa wananchi uliomsimamisha leo maeneo ya Bunju A wilaya ya Kinondoni nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam.
Rais Dokta John Pombe Magufuli akiagana na umati wa wananchi uliomsimamisha leo maeneo ya Bunju A wilaya ya Kinondoni nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam.
(Picha zote na Ikulu)