Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani
Ruvuma, Gombo Samandito amesema kuwa amesikitishwa na utendaji kazi wa Ofisi ya
Msimamizi na mdhibiti ubora wa elimu Wilayani humo kwamba Watendaji wa Ofisi
hiyo, wamekuwa hawatekelezi majukumu yao ya kazi ipasavyo.
Gombo Samandito. |
Samandito alieleza kuwa kutokana na hali hiyo anajiona kama
vile anapwaya katika utendaji wake, hivyo atatoa kibano kwa wale wote ambao ni
wazembe katika kazi.
Mkururugenzi huyo alisema hayo juzi baada ya kupokea taarifa
ya hali ya ukaguzi wa maendeleo ya elimu ya Msingi na Sekondari katika kikao
cha tathimini ya elimu kilichofanyika mjini hapa.
Alisema kuwa kumekuwa na visingizio ambavyo havina msingi
wowote kwamba Ofisi hiyo inashindwa kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya kazi
kutokana na kukosa fedha na gari ili waweze kutimiza ipasavyo uendeshaji wa
shughuli zao za kila siku.