Mfugaji wa jamii ya kisukuma ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake, akiwa na mifugo yake katika kijiji cha Masonya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma. (Picha zote na Steven Augustino) |
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
SERIKALI imeombwa
kutengeneza utaratibu wa kudumu, wa kuijengea sekta ya ufugaji miundombinu ya
uhakika jambo ambalo litaifanya iweze kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la
taifa, tofauti na ilivyo sasa sekta hiyo imekuwa ikichangia wastani wa asilimia
6 tu, kiasi ambacho imeelezwa kuwa ni kidogo.
Hayo yalibainishwa na
wafugaji waliopo katika maeneo mbalimbali wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,
wakati walipokuwa wakizungumza na Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho pamoja na
Mkurugenzi mtendaji, Tina Sekambo wakati wakipinga amri ya kuondolewa katika
maeneo ya vijiji wanavyoishi na kufanyia shughuli za ufugaji.
Wafugaji hao walisema,
ni jambo la muhimu kwa serikali kutilia mkazo juu ya maoni yao, ikiwemo kuacha
tabia ya kunyanyasa wafugaji ili kuweza kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya
mifugo.
Rugwashi Mtegwambuli na
Leleshi Latu ni miongoni mwa wazee wafugaji, ambao walivunja ukimya na
kuilalamikia serikali kuwa hali hiyo inatokana na kutotekeleza makubaliano
husika, huku akisema kuwa serikali imewasahau wafugaji na kuwafanya kama sio
watanzania ambao wanapaswa kuishi na kupewa haki zao za msingi, kama ilivyo kwa
watu wengine.
Walisema wao ni
watanzania ambao ni miongoni mwa wafugaji walioondolewa katika bonde la Ihefu
kutokana na kuwa na makundi makubwa ya ng’ombe, lakini walipofika maeneo ya
Tunduru lilitolewa tamko kwamba waweke makazi yao huko, hali ambayo iliwafanya
wajisajili katika vijiji vya wilaya hiyo na kusomesha watoto wao hivyo sasa
wanashangaa pale wanapoambiwa tena kwamba wahame bila kupewa maelekezo
wanakwenda kuishi wapi na watoto hao watasoma wapi.
“Sisi ni watanzania na
kazi ya ufugaji tunayofanya ni halali kama zilivyo kazi zingine, hatukatai
kuondoka kwenye maeneo haya lakini tunaiomba serikali inapotoa amri ya kututaka
tuondoke, itoe maelekeo wapi tunakwenda”, alisisitiza mzee Leleshi.
Mzee huyo aliendelea
kufafanua kuwa, msimamo wao umetokana na kuchoshwa na utaratibu mbovu wa
serikali kuwaonea mara kwa mara wafugaji na kuonekana ni watu wa kuhama hama.
Wafugaji wengine ambao
nao walizungumzia juu ya hali hiyo, ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji
(CCW) wilayani Tunduru, Othuman Marhaja kutokana na wao kutii mamlaka husika
walikubali kuondoka kwenye bonde la Ihefu mkoani Mbeya, kupitia tamko
lililotolewa na serikali mwaka 2006/2007 na kutakiwa kwenda katika mikoa ya
Lindi na Mtwara lakini wakiwa njiani mifugo yao ilianza kufa kutokana na homa
ya bonde la ufa, hali ambayo serikali ilitoa tena tamko jipya la kusitisha
zoezi hilo la kusafirisha mifugo ili ugonjwa huo usiweze kusambaa.
Naye Nandala Samwel
alieleza kuwa kinachowashangaza ni utaratibu wa serikali, kuendelea
kuwanyanyasa na kuwafukuza kwenye maeneo ambayo tayari walikwisha jisajili
katika vijiji, huku wakiwachangisha michango na kuwatoza ushuru wa aina
mbalimbali ambao sasa imekuwa ni kero kwao.
Akizungumzia juu ya
tamko hilo la kuwaondoa wafugaji hao, Mwenyekiti wa Halmashauri wilaya ya
Tunduru, Faridu Khamis alisema maamuzi hayo yametokana na uwepo wa uvamizi
mkubwa unaofanywa na wafugaji hao ikiwa ni tofauti na maelekezo yaliyotolewa
katika vikao vya baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo.
Khamis alisema wakati
wafugaji hao wanaingia wilayani humo, hawakuzidi 10 lakini tawimu alizonazo
sasa zinaonesha makundi ya wafugaji ni zaidi ya 52 yameonekana yakifanya
shughuli za ufugaji ndani ya wilaya.
Mwenyekiuti huyo
alivitaja vijiji ambavyo vimevamiwa na makundi hayo kuwa ni Misechela, Sauti
moja, Mkowela, Tulieni, Nakapanya, Songambele, Mchangani, Machemba, Liwangula,
Mbuyuni, Twendembele, Kindamba na Jakika kwa kile alichodai kuwa maeneo hayo ni
maalumu kwa ajili ya hifadhi ya misitu.
Alisema kumbukumbu
zilizopo katika ofisi yake zinafafanua kuwa wafugaji hao waliruhusiwa kukaa
katika vijiji vya Musonya, Muhuwesi na Ngapa lakini kutokana na wafugaji kuwa
na tabia ya kuwaita wenzao kutoka maeneo mengine nje ya wilaya, wameendelea
kuongezeka hali ambayo sasa inahatarisha usalama na amani ndani ya wilaya ya
Tunduru.
1 comment:
Kuna kila sababu kwa serikali kumaliza mgogoro huu, kabla haujafikia mahali pabaya.
Post a Comment