Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WALIMU wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi zao
ikiwemo kuacha vitendo vya ulevi na utoro kazini.
Aidha wamesisitizwa kuwahi na kuwa katika mazingira ya kazi
wakati wote na kufuata taratibu za kazi zao kwa mujibu wa nafasi walizonazo
kazini.
Gombo Samandito. |
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya hiyo, Gombo Samandito wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha
tathimini ya maendeleo ya elimu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki
Jimbo la Mbinga mjini hapa.
“Walimu mnatabia ya kuwa watoro kazini natambua mnajua kwamba
zikipita siku tano haupo kazini nakufukuza kazi, wakati wa kazi fanyeni kazi zenu
kwa kutekeleza ipasavyo majukumu mliyopewa mkayasimamie haya vizuri msiwe
sehemu ya matatizo”, alisisitiza Samandito.
Samandito alisisitiza pia kwa atakayepuuza maagizo yake hatua
kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufukuzwa kazi huku
akiongeza kuwa adui mkubwa wa maendeleo katika maisha ya kila siku ya binadamu
ni tabia ya mtu husika hivyo walimu hao wanapaswa kujiangalia kwanza wenyewe na
kubadilika mara moja kuwa na tabia nzuri kazini.